ZIWA LINALOLINDWA NA JOKA

ZIWA LINALOLINDWA NA JOKA

Imeandikwa na: Gwamaka Mwamasage

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, Tanzania ina takribani maziwa makubwa kumi na tatu, yanayoshikilia rekodi mbalimbali za juu barani Afrika na duniani. Mbali na hayo, kuna pia maziwa madogo zaidi ya tisini yaliyosambaa kote nchini.

Miongoni mwa maziwa hayo, leo tunalielezea Ziwa Kisiba (au Kisibha kwa lahaja ya Kinyakyusa). Neno "Kisiba" linamaanisha “kisima” kwa lugha ya Kinyakyusa, na ndilo lililotumika pia kutaja eneo hili kutokana na uwepo wa ziwa hilo.

Ziwa Kisiba liko Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, katika nyanda za juu kusini mwa Tanzania. Lipo ndani ya Tarafa ya Masoko, jambo linalosababisha wengine kulita Ziwa Masoko. Kutoka mjini Tukuyu hadi tarafa hiyo ni safari ya chini ya nusu saa.

Ziwa hili ni kivutio kizuri cha utalii kwa kuwa, mbali na mito inayolishibisha na kulitoa maji, limezungukwa na msitu mnene uliohifadhiwa vizuri. Kwa sababu hiyo, hutembelewa na watalii wa kigeni kwa madhumuni ya mapumziko na tafiti mbalimbali.

Eneo maarufu kwa kuogelea linaitwa Lwifwa, lenye maji yenye kina kifupi na uwanda tambarare unaomruhusu mwogeleaji kusogea kwa uhuru. Wageni kutoka mataifa kama Ujerumani, Uingereza na Marekani wamewahi kufika hapo.

Kwa wenyeji, Ziwa Kisiba si tu eneo la burudani bali pia chanzo cha maji kwa matumizi ya nyumbani, uvuvi, na wakati mwingine hutumika kwa imani za jadi au tiba asilia. Kando ya ziwa, kuna makaburi matatu ya Wajerumani waliopoteza maisha wakati wa vita kati ya Ujerumani na Uingereza.

Hadithi za kienyeji zinasema katikati ya ziwa kuna hazina kubwa, sarafu za Kijerumani (Rupia) na madini ya thamani, zilizofichwa na Wajerumani waliposhindwa vita. Hazina hiyo, inadaiwa, inalindwa na joka kubwa lenye vichwa viwili, linaloaminika kuwa mzimu wa kulinda ziwa.

Rupia hizo hupendwa na waganga wa kienyeji kwa madai kuwa na nguvu za kimiujiza. Wenyeji wanasimulia kuwa watafiti wa kigeni, wakiwemo Wajerumani mnamo Agosti 1996, walipofika kuchunguza, walikimbia baada ya joka hilo kuonekana ghafla.

Kuna pia tukio la ajabu linalotokea kila siku saa kumi na mbili jioni: mstari mrefu hujitokeza juu ya maji kutoka Lwifwa kuelekea Bomani, karibu na makaburi hayo. Chanzo cha tukio hili bado hakijulikani huenda ni la kisayansi au kiimani.

Pamoja na masimulizi haya ya kutisha, Ziwa Kisiba linabaki kuwa kivutio kizuri cha utalii. Mwandishi anashauri wageni kuwasiliana vizuri na wenyeji ili kuepuka matatizo, kwani maeneo kama haya yana taratibu na mila maalumu za kufuatwa.