Misri na Kenya: Mahusiano ya Kihistoria ya Karibu na Ushirikiano Unaokua

Misri na Kenya: Mahusiano ya Kihistoria ya Karibu na Ushirikiano Unaokua

Imetafsiriwa na: Mariam Mohamad said na Marwa Yasser Mahmoud 
Imehaririwa na:  Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr


Rais Jomo Kenyatta amewahi kutoa kauli maarufu akisema: "Tutamkumbuka Nasser daima kwa kuwa msaada wake kwa Afrika uliwezesha uhuru wa mataifa mengi barani humo."

Mahusiano ya kidiplomasia ni mojawapo ya vipengele muhimu zaidi vya mahusiano ya kimataifa, kwani ni mojawapo ya njia kuu za mwingiliano na ushirikiano kati ya mataifa. Misri na Kenya zina mahusiano ya kihistoria ya karibu, ambapo kila moja ni muhimu kwa nyingine. Misri inategemea Mto Nile kama chanzo chake kikuu cha maji, wakati Kenya inaihitaji Misri kama lango muhimu la biashara kuelekea Bahari ya Mediterania.

Historia ya mahusiano kati ya Misri na Kenya inaanzia kabla ya uhuru wa Kenya. Wakati wa utawala wa Rais Gamal Abdel Nasser, Misri iliunga mkono vuguvugu la Mau Mau la Kenya kupitia kampeni za vyombo vya habari na diplomasia dhidi ya ukoloni wa Uingereza nchini Kenya. Vilevile, Misri ilianzisha redio iliyoitwa Sauti ya Afrika, iliyikuwa kituo cha kwanza cha Kiswahili kurushwa kutoka nchi ya Kiafrika kwa lengo la kuiunga mkono Kenya katika harakati zake za uhuru.

Misri ilifanya suala la Mau Mau kuwa ajenda ya Afrika na ilijitahidi kushinikiza kuachiliwa kwa kiongozi wa Kenya, Jomo Kenyatta, aliyekamatwa na wakoloni wa Uingereza mnamo mwaka 1961.

Ikumbukwe kuwa harakati ya Mau Mau (1952-1960), inayojulikana pia kama Mapinduzi ya Mau Mau nchini Kenya, ilikuwa vita katika koloni la Uingereza la Kenya (1920-1963) kati ya Jeshi la Uhuru na Ardhi la Kenya (KLFA), linalojulikana pia kama Mau Mau, na utawala wa kikoloni wa Uingereza. Wengi wa wapiganaji wa KLFA walitoka katika kabila la Wakikuyu, lakini vikosi hivi pia vilijumuisha wapiganaji kutoka makabila ya Wakamba na Wamaasai, waliopigana dhidi ya wakoloni wa Ulaya, jeshi la Uingereza, na vikosi vya wenyeji waliounga mkono utawala wa kikoloni, ikiwa ni pamoja na baadhi ya Wakikuyu waliokuwa waaminifu kwa Waingereza.

Kairo ilikuwa mji mkuu wa kwanza kuwakaribisha wapigania uhuru wa Kenya na kuwapa msaada wa kila aina ili kuimarisha harakati zao nchini Kenya. Misri pia ilitoa msaada kwa viongozi wa vyama viwili vikuu vya kisiasa vya Kenya, KANU na KADU, ambapo vilifungua ofisi zao mjini Kairo katika kipindi hicho. Hatimaye, juhudi za Misri zilichangia mafanikio ya Kenya katika kupata uhuru wake mnamo mwaka 1963.

Mnamo mwaka 1964, Kenya ikawa jamhuri na ikaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Misri kwa kufungua ubalozi wake mjini Kairo. Wakati wa uteuzi wa balozi wa kwanza wa Kenya nchini Misri, Rais Gamal Abdel Nasser alieleza kuvutiwa kwake na harakati za wananchi wa Kenya kupigania uhuru wao chini ya uongozi wa Jomo Kenyatta, ambaye baadaye alikua Rais wa kwanza wa Kenya baada ya uhuru. Nasser alionesha utayari wake wa kushirikiana na Kenya pamoja na mataifa yote ya Afrika ili kuimarisha nguvu ya bara hilo na kutumia rasilimali zake kwa ajili ya mshikamano wake.

Pia, mnamo mwaka 1964, Misri iliandaa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi za Afrika mjini Kairo. Katika mkutano huo, Rais Gamal Abdel Nasser alieleza utayari wake wa kushirikiana kijeshi na Kenya, huku Rais Jomo Kenyatta akieleza azma yake ya kuwaondoa wanajeshi wa Uingereza waliokuwa bado nchini Kenya na akaomba msaada wa Misri katika kujenga jeshi la kitaifa la Kenya. Waziri wa Habari wa Misri, Mohamed Fayek, alitumwa Nairobi kwa mazungumzo rasmi, ambapo walikubaliana kutoa mafunzo kwa kikosi cha wanajeshi wa anga na kutuma wataalamu wa kijeshi wa Misri kuwafundisha wanajeshi wa Kenya baada ya maafisa wa Uingereza kuondolewa. Maafisa kadhaa wa Kikenya pia walitumwa kupata mafunzo nchini Misri.

Mnamo mwaka 1967, mradi wa Hydromet ulianza kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Misri na Kenya pamoja na nchi nyingine tano za Bonde la Nile, kisha nchi nne zaidi ziliungana baadaye. Mradi huu ulilenga kuchunguza hali ya hewa na maji katika Bonde la Maziwa ya Ikweta, kuandaa mipango ya maendeleo ya rasilimali za maji, na kuchunguza uwiano wa maji wa Mto Nile. Sehemu ya mradi huu ilihusisha uanzishwaji wa vituo vya uchunguzi katika maziwa ya Viktoria, Kyoga, na Albert. Mradi huu ulifadhiliwa na mataifa mbalimbali wahisani, Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, na Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

Kenya pia ilikuwa miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyovunja uhusiano wa kidiplomasia na Israeli baada ya Vita vya Oktoba 1973. Mnamo Februari 1984, rais wa zamani wa Misri alifanya ziara nchini Kenya na pia alitembelea Zaire, Somalia, na Tanzania. Alipendekeza kwamba Misri iwe daraja kati ya mataifa ya Kiarabu na mataifa ya Afrika, na kuwa mpatanishi wa uwezekano katika utatuzi wa migogoro ya bara hilo.

Mnamo mwaka 1998, Misri ilijiunga na mkataba wa COMESA unaojumuisha mataifa 22 ya Afrika. Kenya ilikuwa imesaini hati za makubaliano hayo wakati wa mkutano wa mawaziri huko Lilongwe. COMESA ina umuhimu wa kipekee kwa Misri kutokana na nafasi yake ya kijiografia, kwani inapakana na ulimwengu wa Kiarabu, eneo la Pembe ya Afrika, na mataifa ya Bonde la Nile.

Misri na Kenya zina mahusiano ya kindugu ya kina, umeoonekana wazi katika nyakati tofauti, hasa wakati wa majanga na hali ngumu za asili. Misri daima imetoa msaada wa chakula, matibabu, na msaada wa kiufundi kwa wananchi wa Kenya ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimahakama na kubadilishana uzoefu, Jaji Mkuu wa Kenya, Johnson Evans Gicheru, alifanya ziara nchini Misri mnamo Desemba 2008. Ziara hiyo ilimwezesha kujifunza kuhusu mfumo wa sheria wa Misri na kukutana na wenzake ili kujadili njia za kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mahakama.

Mnamo Juni 2009, Kenneth Marende, Spika wa Bunge la Kenya, alihudhuria kikao cha pili cha Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Bonde la Nile, kilichofanyika nchini Misri.

Mnamo Julai 2009, Kalonzo Musyoka, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, aliongoza ujumbe wa Kenya kushiriki katika Mkutano wa Kundi la Kutofungamana na Upande Wowote, uliofanyika Sharm El-Sheikh. Wakati wa mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Musyoka alieleza shukrani zake kwa undani wa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili na kusisitiza azma ya Kenya kuuimarisha, hasa katika sekta ya biashara.

Mnamo Novemba 2009, Moses Wetang’ula, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alihudhuria Jukwaa la Nne la Mawaziri kuhusu Ushirikiano kati ya China na Afrika, lililofanyika nchini Misri katika mji wa Sharm El-Sheikh. Alifanya mazungumzo na mwenzake wa Misri kuhusu njia za kuimarisha ushirikiano katika sekta ya maendeleo ya rasilimali za maji nchini Kenya, kukabiliana na ukame, kupungua kwa mvua, na kurekebisha misitu ya mvua.

Mnamo Mei 2010, Raila Odinga, Waziri Mkuu wa Kenya, alipokuwa ziarani nchini Misri, alisisitiza kuwa nchi yake haiwezi kuhatarisha maslahi ya Misri kuhusu maji.

Mnamo Aprili 2011, Richard Onyonka, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alitembelea Kairo kwa ajili ya mashauriano ya kisiasa na maafisa mbalimbali wa serikali ya Misri.

Tangu mwaka 2014, mahusiano kati ya Misri na Kenya umepitia maendeleo chanya na ukuaji wa kushangaza katika nyanja zote. Misri imechukua njia mbili katika mahusiano yake na Kenya: ya kwanza ni mahusiano ya pande mbili kupitia ziara na mikutano inayosaidia kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa haya mawili, na ya pili ni ushirikiano katika sekta ya maji, kutokana na umuhimu wa nchi hizi mbili kama sehemu ya Bonde la Nile.

Mikutano Muhimu Kati ya Marais wa Misri na Kenya

Mnamo tarehe Agosti 8 2023: Rais Abdel Fattah El-Sisi na Rais William Ruto wa Jamhuri ya Kenya walifanya mazungumzo kwa njia ya simu, ambapo walithibitisha dhamira yao ya kuimarisha mahusiano ya pande mbili kati ya Misri na Kenya na kukuza ushirikiano wa pamoja. Viongozi hao walikubaliana kuongeza uratibu na mashauriano ili kusaidia maendeleo endelevu katika muktadha wa ushirikiano wa Afrika na kuimarisha ujumuishaji wa bara. Pia walijadili njia za kuimarisha mahusiano ya pande mbili na kubadilishana maoni kuhusu masuala ya Afrika yenye umuhimu wa pamoja, yakiwemo hali ya Sudan na Bonde la Nile.

Mnamo tarehe Julai 15, 2023: Rais Abdel Fattah El-Sisi alitembelea Kenya ili kushiriki katika kikao cha tano cha mkutano wa uratibu wa katikati ya mwaka wa Umoja wa Afrika, ambapo alipokelewa na Rais William Ruto wa Kenya. Ziara hiyo ililenga kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na kujadili masuala mbalimbali ya kikanda na ya bara yenye umuhimu wa pamoja, pamoja na kutathmini njia za kuimarisha juhudi za pamoja za Afrika kwa maendeleo na ujumuishaji wa bara. Katika kitabu cha wageni, Rais El-Sisi alitoa shukrani zake kwa Rais Ruto na wananchi wa Kenya kwa mapokezi mazuri na kueleza furaha yake ya kuwa Nairobi, akiwatakia Kenya maendeleo na ustawi zaidi.

Mnamo tarehe Machi 7, 2023: Rais Abdel Fattah El-Sisi alizungumza kwa simu na Rais William Ruto wa Kenya, ambapo walibadilishana maoni kuhusu masuala ya Afrika yenye umuhimu wa pamoja, hasa juhudi za kudumisha amani na usalama na kuimarisha utulivu katika bara la Afrika.

Mnamo Julai 12, 2023: Balozi Wael Nasr Eldin Attia, Balozi wa Misri nchini Kenya, alikutana na Alfred Mutua, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, ambapo walijadili njia za kuimarisha mahusiano ya pande mbili na maandalizi ya ushiriki wa Misri katika kikao cha tano cha mkutano wa uratibu wa katikati ya mwaka wa Umoja wa Afrika, kilichotarajiwa kufanyika Kenya mnamo tarehe Julai 16. Ushiriki huu ulikuwa sehemu ya urais wa Misri wa Kamati ya Mwongozo ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (NEPAD).

Ushirikiano wa Kidiplomasia na Kiuchumi Kati ya Misri na Kenya

Waziri wa Kenya alizungumzia maeneo ya ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili na uratibu wa misimamo kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa yenye umuhimu wa pamoja. Pia, alitoa ujumbe kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry, akieleza matarajio yake ya kukutana naye Nairobi ili kufuatilia mazungumzo kuhusu masuala yaliyotolewa wakati wa ziara yake mjini Kairo mnamo Machi, pamoja na mawasiliano ya hivi karibuni kati ya marais wa mataifa hayo mawili.

Ushiriki wa Misri katika Mkutano wa UN-Habitat

Mnamo tarehe Juni 6, 2023, Dkt. Assem El-Gazzar, Waziri wa Nyumba, Huduma za Umma, na Maendeleo ya Miji wa Jamhuri ya Misri, alihutubia kikao cha pili cha Bunge la Mpango wa Makazi wa Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), kilichofanyika Nairobi, Kenya, kwa kushirikiana na Meja Jenerali Hisham Amna, Waziri wa Maendeleo ya Mitaa wa Misri.

Waziri El-Gazzar alitoa shukrani kwa Rais wa Kenya na serikali ya Kenya kwa mapokezi mazuri na maandalizi ya mkutano huo wa pili wa Bunge la UN-Habitat. Pia alisisitiza dhamira ya Misri ya kusaidia ajenda za maendeleo ya kimataifa na kushirikiana katika juhudi za kikanda na kimataifa za maendeleo ya kitaifa, kikanda, na kimataifa.

Aidha, alitaja kuwa Misri iliandaa Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (COP27) na inaunga mkono masuala yote muhimu katika ajenda ya tabianchi ya kimataifa, yakiwemo maendeleo ya miji endelevu.

Waziri El-Gazzar pia alirudia mwaliko kwa washiriki wa kikao cha pili cha Bunge la UN-Habitat kushiriki kwa ufanisi katika Jukwaa la Kimataifa la Miji (WUF 24), litakalofanyika Kairo mwaka ujao. Alithibitisha kuwa maandalizi yanaendelea ili kuendeleza ajenda na shughuli zitakazochangia juhudi za kimataifa za kurejesha ubinadamu kwenye msingi wake halisi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya miji.

Ushirikiano wa Kiuchumi Kati ya Misri na Kenya

Misri inaendelea kuimarisha mtazamo wake wa Kiafrika na inajitahidi kukuza biashara na nchi za bara la Afrika ili kukidhi mahitaji yake ya bidhaa mbalimbali. Misri inaamini kuwa ushirikiano kati ya nchi za Afrika unawanufaisha watu wake wote, na inafanya juhudi za kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kibiashara ili kufanikisha ujumuishaji wa kiuchumi na maendeleo endelevu barani Afrika. Kuendeleza mahusiano ya kiuchumi na kibiashara na Kenya kunaonyesha dhamira thabiti ya Misri katika kukuza ushirikiano na mataifa ya Afrika na kuimarisha uchumi wa bara kwa ujumla.

Mahusiano ya kiuchumi na kibiashara na Kenya ni mojawapo ya vipaumbele vya kimkakati vya Misri katika juhudi zake za kuongeza ushirikiano na nchi za Afrika. Kwa miongo kadhaa, Misri imejenga ushirikiano wa kiuchumi na Kenya, iwe kwa ngazi ya nchi mbili au kupitia jumuiya za kiuchumi za kikanda zinazoziunganisha nchi hizo.

Katika muktadha huu, mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Misri na Kenya yanaendelea kupewa kipaumbele cha kimkakati kwa lengo la kukuza ushirikiano wa Afrika na uchumi wa bara kwa ujumla. Ushirikiano huu umeimarika zaidi kutokana na uanachama wa nchi hizo katika COMESA, moja ya jumuiya muhimu za kiuchumi katika Afrika Mashariki na Kusini.

Misri na Kenya zinafanya kazi pamoja kuboresha biashara na uwekezaji kati yao, huku zikishirikiana katika sekta mbalimbali kama kilimo, nishati, miundombinu, viwanda, teknolojia, na biashara.

Kwanza: Jumuiya ya COMESA

COMESA (Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini) ni jumuiya ya kikanda yenye mafanikio barani Afrika, iliyoanzishwa mnamo mwaka 1994 kuchukua nafasi ya Eneo la Biashara ya Upendeleo kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kusini, lililoanzishwa mwaka 1981.

Makubaliano ya COMESA yalianza kama eneo la biashara ya upendeleo likiwa na lengo la kuanzisha eneo la biashara huria kati ya wanachama wake. Hatimaye, makubaliano haya yalikua na kuwa umoja wa forodha, kisha soko la pamoja. Misri ilijiunga na COMESA mnamo tarehe Juni 29, 1998 na kuanza kutekeleza msamaha wa kodi kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka kwa wanachama wengine mnamo tarehe Februari 27, 1999. Msamaha huu unatolewa kwa mujibu wa mkataba wa biashara ya pande zote, kwa bidhaa zinazoambatana na cheti rasmi cha asili kutoka mamlaka husika katika kila nchi.

Mnamo tarehe Oktoba 31, 2000, nchi tisa wanachama wa COMESA, zikiwemo Misri na Kenya, zilitia saini makubaliano ya kuunda eneo la biashara huria kati yao. Rwanda na Burundi zilijiunga na makubaliano haya mnamo tarehe Januari 1, 2004. Kwa mujibu wa makubaliano haya, nchi husika zinatoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazosafirishwa kati yao, mradi bidhaa hizo ziwe na cheti rasmi cha asili cha COMESA.

Jumuiya ya COMESA inaonyesha dhamira ya wanachama wake katika kukuza biashara na kuimarisha ujumuishaji wa kiuchumi katika kanda hii. Pia, inatoa fursa za ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa wanachama kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Pili: Biashara kati ya Misri na Kenya

Thamani ya biashara kati ya Misri na Kenya imekuwa ikibadilika kwa vipindi tofauti. Mnamo mwaka 2020, biashara kati ya nchi hizo iliongezeka kwa 3.58%, ikifikia dola milioni 635.8, ikilinganishwa na dola milioni 613.8 mnamo mwaka 2019. Mizania ya biashara kwa manufaa ya Misri iliongezeka kutoka dola milioni 237.6 mwaka 2019 hadi dola milioni 261.2 mnamo mwaka 2020, ongezeko la 9.9%.

Thamani ya mauzo ya Misri kwenda Kenya ilipanda kwa 5.3%, ikifikia dola milioni 448.5 mwaka 2020, ikilinganishwa na dola milioni 425.7 mwaka 2019. Hii inaonyesha umuhimu wa soko la Kenya kwa Misri na imani ya wafanyabiashara na watumiaji wa Kenya kwa bidhaa za Misri.

Licha ya athari za janga la COVID-19 kwa biashara nchini Kenya, nchi hiyo bado ni soko lenye fursa kwa bidhaa za Misri. Mwaka 2020, Misri ilikuwa miongoni mwa nchi 10 bora zinazosafirisha bidhaa kwenda Kenya. Wakati huohuo, uagizaji wa Misri kutoka Kenya ulipungua kwa 0.42%, kutoka dola milioni 188.1 hadi dola milioni 187.3.

Bidhaa Kuu Zinazosafirishwa kati ya Misri na Kenya

Bidhaa kuu zinazosafirishwa kutoka Misri kwenda Kenya: Sukari, bidhaa za chuma na chuma cha pua, matairi na betri za magari, bidhaa za karatasi, kemikali, sabuni za viwandani, nyaya za umeme, vifaa vya umeme, madawa, vifaa vya uhandisi, vifaa vya insulation, vifaa vya nyumbani, mazulia na zulia, mafuta ya petroli, nta ya parafini, viyoyozi, vitanda, mitambo ya simu, plastiki za viwandani, rangi, vigae, vifaa vya afya, televisheni, saruji, sabuni, mbolea, unga, chokoleti, pipi, juisi na jamu.

Bidhaa kuu zinazoagizwa na Misri kutoka Kenya: Chai, tumbaku, sisal, kemikali, mafuta, matunda na mboga mbichi, maua ya mapambo, maua makavu, na baadhi ya malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa wino wa uchapishaji.

Tatu: Uwekezaji

Kuna shughuli nyingi za uwekezaji kati ya Misri na Kenya, hasa kupitia wawekezaji wa Misri. Kulingana na takwimu rasmi, uwekezaji wa Misri unashikilia nafasi ya 24 katika soko la Kenya, ukiwa na thamani ya dola milioni 36.6. Kwa upande mwingine, uwekezaji wa Kenya nchini Misri unashika nafasi ya 80, ukiwa na thamani ya dola milioni 7.7 na ukihusisha kampuni 22.

Miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa Misri nchini Kenya, kampuni ya Citadel Capital inamiliki 85% ya hisa za Rift Valley Railways, kampuni inayosimamia reli kati ya Mombasa na Kampala.

Juhudi za pamoja kati ya Misri na Kenya zinalenga kukuza ushirikiano wa viwanda, hasa katika sekta zinazohusiana na uzalishaji wa kilimo na mifugo. Sekta hizi zinajumuisha uchakataji wa nyama, ngozi, na juisi. Vilevile, nchi hizo zinashirikiana katika matumizi ya utaalamu wa viwanda wa Misri ili kusaidia sekta ya viwanda ya Kenya kwa mafunzo na msaada wa kiufundi.

Pande zote mbili pia zinachunguza uwezekano wa kushirikiana katika usajili wa dawa, kwa kurahisisha taratibu za usajili na kupunguza gharama kwa upande wa Kenya.

Juhudi hizi zinaonesha dhamira ya nchi hizo mbili katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupanua uwekezaji wa pande zote.

Nne: Kamati ya Pamoja kati ya Misri na Kenya

Kamati ya Pamoja kati ya Misri na Kenya ni mpango unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili. Kamati hii ilianzishwa mnamo Desemba 2016 wakati wa mikutano ya Baraza la Pamoja la Misri na Kenya, linalojumuisha mawaziri na wawakilishi wa sekta mbalimbali za kiuchumi kutoka pande zote mbili.

Vikundi vya kazi viliundwa ili kuimarisha biashara na uwekezaji katika sekta kama uhandisi, petrokemia, kilimo, afya, nishati, na chakula. Miradi na mipango maalum ilikubaliwa katika sekta hizi ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Ujumbe wa Misri ulioshiriki katika Baraza la Biashara la Misri na Kenya uliona fursa kubwa za ushirikiano katika sekta ya afya. Katika jitihada za kuboresha huduma za afya, kifaa cha maabara kinachohamishika kwa ajili ya uchunguzi wa damu na kituo cha matibabu cha kutibu maambukizi ya virusi vya Hepatitis C vilitolewa kama msaada. Aidha, makubaliano yalifikiwa kuhusu usimamizi wa hospitali moja kwa usimamizi wa madaktari wa Kimasri.

Katika sekta ya nishati, barua za dhamira ziliwasilishwa kwa ajili ya kuanzisha mitambo ya nishati ya jua kwa kushirikiana na serikali ya Kenya. Vilevile, makubaliano yalifikiwa kuhusu uwekezaji wa kilimo katika mazao kama mahindi ya njano, soya, na mpunga.

Mikutano ya pamoja hufanyika kila robo mwaka ili kufuatilia maendeleo ya miradi. Maghala ya bidhaa za Misri yalijengwa Mombasa, na kampuni maalum ilianzishwa nchini Kenya kwa ajili ya kukuza na kusambaza bidhaa za Misri katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Zaidi ya hayo, kiwanda cha kufungasha na kupakia chai kilianzishwa katika eneo la Ain Sokhna kwa ajili ya kuuza bidhaa hizo kwa masoko ya Ulaya, Ghuba ya Kiarabu, na Asia ya Kati.

Kwa kifupi, Kamati ya Pamoja kati ya Misri na Kenya ina jukumu la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizi mbili kupitia miradi na mipango mbalimbali inayolenga kukuza biashara na uwekezaji.

Kupitia njia hizi, Misri inaimarisha nafasi yake katika kanda na bara la Afrika kwa kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi zote mbili na bara kwa ujumla. Ushirikiano huu wa kiuchumi na kibiashara ni sehemu muhimu ya mkakati wa Misri wa maendeleo endelevu na ujumuishaji wa kikanda barani Afrika.

Tano: Ushirikiano wa Kisheria
Mahusiano ya pande mbili kati ya Misri na Kenya ni imara na ya kihistoria, ambapo makubaliano na hati nyingi za maelewano zimesainiwa kwa miaka mingi. Hapa kuna orodha ya baadhi ya makubaliano hayo:

• Mkataba wa Biashara – 28/11/1980
• Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kiufundi – 28/11/1980
• Mkataba wa Ushirikiano wa Utalii – 25/6/1987
• Mkataba wa Ushirikiano wa Utamaduni – 25/6/1987
• Mkataba wa Ushirikiano kati ya Vyama vya Wafanyabiashara wa nchi zote mbili – 13/1/1996
• Mpango wa Utekelezaji wa Ushirikiano wa Kisayansi, Kitamaduni, na Kielimu – 13/1/1996
• Mpango wa Utekelezaji wa Ushirikiano katika Sekta ya Utalii – 13/1/1996
• Hati ya Maelewano kuhusu Mashauriano kati ya Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo mbili – 19/1/2007
• Hati ya Maelewano ya Ushirikiano katika Mafunzo ya Kidiplomasia kati ya Wizara za Mambo ya Nje – 19/1/2007
• Hati ya Maelewano kuhusu Ushirikiano katika Sekta ya Habari, Mawasiliano, na Vyombo vya Habari – 29/1/2002
• Mpango wa Utekelezaji wa Ushirikiano wa Kitamaduni, Kielimu, na Kisayansi kwa miaka 2010-2013 – 3/2/2010
• Hati ya Maelewano kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Vijana – 3/2/2010
• Hati ya Maelewano kati ya Wizara ya Kilimo na Ustawi wa Ardhi ya Misri na Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi ya Kenya kuhusu Ushirikiano katika Sekta ya Uvuvi – 3/2/2010
• Hati ya Maelewano ya Ushirikiano katika Elimu ya Juu, Sayansi, na Teknolojia – 3/2/2010
• Hati tatu za Maelewano na Programu za Utekelezaji katika Uwekezaji, Maktaba na Kumbukumbu, na Ushirikiano wa Kitamaduni kwa miaka 2015-2017
• Makubaliano ya Biashara kati ya nchi hizo mbili
• Makubaliano ya Biashara ya Pande Mbili kati ya Misri na Kenya – 2015
• Hati ya Maelewano ya Utekelezaji wa Mradi wa Maendeleo na Usimamizi wa Rasilimali za Maji (WRDMP) – Agosti 2016
• Mkataba wa ununuzi wa bidhaa za Misri wenye thamani ya dola milioni 10 katika sekta mbalimbali kama uhandisi, kemikali, vifaa vya ujenzi, chakula, na afya
• Mkataba wa Ushirikiano wa Kiufundi katika Sekta ya Ulinzi kati ya Wizara za Ulinzi za nchi zote mbili – Mei 2021

Ushirikiano kati ya Misri na Kenya kuhusu Mto Nile

Misri na Kenya zina mahusiano ya kihistoria na ushirikiano wenye tija kwa miaka mingi kutokana na rasilimali yao ya pamoja—Mto Nile—ambao ni kiunganishi muhimu kati ya nchi hizo mbili. Mto huu unatokana na Ziwa Viktoria nchini Kenya na kupitia Misri kabla ya kuishia katika Bahari ya Mediterania. Nchi hizi zina maslahi ya pamoja katika matumizi na usimamizi wa maji ya Nile.

Tangu enzi za kale, Misri imekuwa na shauku kubwa ya kushirikiana na nchi za Bonde la Nile, zikiwemo Kenya, ili kudhibiti matumizi ya maji ya mto huu kwa njia yenye uwiano inayowanufaisha wote. Ushirikiano huu umeendelea kwa karne nyingi na umejikita katika sekta mbalimbali.

Katika muktadha wa usimamizi wa rasilimali za maji, Misri na Kenya zilisaini Hati ya Makubaliano (MoU) mnamo mwaka 2016 kwa ajili ya mradi wa maendeleo ya rasilimali za maji nchini Kenya. Mradi huu unahusisha ujenzi wa mabwawa sita ya kuhifadhi maji, uchimbaji wa visima ishirini, na utekelezaji wa mradi wa majaribio wa mfumo wa kisasa wa umwagiliaji katika kilimo. Aidha, unajumuisha mafunzo kwa wataalamu wa Kenya nchini Misri na Kenya.

Vilevile, Misri na Kenya zilisaini mikataba kadhaa kwa ajili ya uchimbaji na uboreshaji wa visima 180 vya maji chini ya ardhi ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi ya kunywa kwa maeneo yenye ukame nchini Kenya. Miradi hii ilitekelezwa kwa msaada wa kifedha kutoka Bajeti ya Wizara ya Umwagiliaji ya Misri na ilikamilika mnamo mwaka 2009.

Mnamo mwaka 2017, Rais Abdel Fattah El-Sisi, katika mkutano wake na Rais Uhuru Kenyatta, alitangaza dhamira ya Misri kusaidia maendeleo katika nchi za Bonde la Nile ili kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali zake kwa manufaa ya nchi zote zinazotegemea mto huu.

Ushirikiano wa Usalama

Ushirikiano wa usalama kati ya Misri na Kenya katika mapambano dhidi ya ugaidi na misimamo mikali ni moja ya nyanja muhimu za mahusiano kati ya mataifa haya mawili. Nchi hizi zinakabiliwa na changamoto zinazofanana kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayolenga maeneo ya kijeshi na kiraia kutoka kwa makundi yenye misimamo mikali. Kenya imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya kigaidi yanayohusika na vurugu.

Mnamo Februari 2017, Rais Abdel Fattah El-Sisi na Rais Uhuru Kenyatta walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa usalama kati ya Misri na Kenya, hasa katika mapambano dhidi ya ugaidi na changamoto zinazotokana na kuongezeka kwa vitisho vya makundi ya kigaidi. Katika muktadha huu, Rais El-Sisi alisisitiza nafasi muhimu ya Al-Azhar Sharif katika kueneza mafundisho sahihi ya Uislamu na kupambana na itikadi kali za kigaidi.

Aidha, Rais El-Sisi alipokea kwa furaha ombi la Rais Kenyatta la kuongeza idadi ya maimamu na wahubiri wa Kiislamu wa Kenya wanaopata mafunzo kutoka Al-Azhar kwa ajili ya kuimarisha uelewa wa dini na kupambana na misimamo mikali nchini Kenya.

Msimamo wa Al-Azhar Sharif kuhusu Ugaidi nchini Kenya

Mnamo tarehe Aprili 26, 2018, mji wa Malindi, Kenya, uliandaa mkutano wa siku nne wa Msafara wa Amani, ulioandaliwa na Baraza la Wazee wa Waislamu kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya pamoja na wawakilishi wa madhehebu mbalimbali na mwakilishi wa serikali ya Kenya anayehusika na mazungumzo ya kidini. Katika kikao hicho, wajumbe wa msafara walitoa utangulizi kuhusu Al-Azhar Sharif kama taasisi ya kidini, kielimu na ya kiutume, pamoja na nafasi ya Baraza la Wazee wa Waislamu katika kueneza utamaduni wa mazungumzo na kukuza amani duniani.

Mnamo tarehe Novemba 2, 2018, kikundi cha Jil Al-Salama nchini Kenya, kwa kushirikiana na misheni ya wanazuoni wa Al-Azhar Sharif nchini humo, kiliandaa kongamano la maimamu na wahubiri chini ya kaulimbiu: "Nafasi ya Maimamu na Wahubiri katika Kukuza Amani ya Kijamii."

Mnamo tarehe Februari 27, 2018, Sheikh Ahmad Al-Tayyeb, Imamu Mkuu wa Al-Azhar Sharif, alimpokea Sheikh Yusuf Nzibo, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya. Katika mkutano huo, Sheikh Al-Tayyeb alieleza kuwa Al-Azhar iko tayari kuongeza juhudi zake na kuunga mkono Waislamu wa Kenya kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa Kiislamu wa Kenya wanaopewa ufadhili wa masomo katika Al-Azhar, pamoja na kutoa mafunzo kwa maimamu wa Kenya kuhusu changamoto za kisasa.

Kwa upande wake, Sheikh Nzibo alitoa shukrani kwa Imamu Mkuu kwa msaada wa Al-Azhar katika sekta za elimu, dawah, na misaada ya kibinadamu kwa Waislamu wa Kenya. Alisisitiza kuwa Al-Azhar ni sauti ya Waislamu duniani na kimbilio la kielimu lililochangia kudumisha utulivu wa kijamii barani Afrika kwa muda mrefu, huku likibaki kuwa ngome muhimu katika kulinda jamii za Kiafrika dhidi ya mawazo yenye misimamo mikali.

Ushirikiano kati ya Misri na Kenya
Mkutano wa Sheikh Ahmad Al-Tayyeb na Viongozi wa Kenya

Mnamo tarehe Oktoba 24, 2016, Sheikh Ahmad Al-Tayyeb alipokea ujumbe wa viongozi wa Kenya wakiongozwa na Sheikh Ahmad Badawi, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya, katika ziara yao jijini Kairo, Misri. Katika mazungumzo hayo, Sheikh Al-Tayyeb alisisitiza kuwa Al-Azhar inafanya kazi kupambana na fikra potofu na misimamo mikali inayoharibu taswira ya Uislamu. Aidha, alifafanua kuwa dini zote, zikiwemo Uislamu, hazina uhusiano wowote na ugaidi, kwani dini zote ziliteremshwa kwa ajili ya ustawi na furaha ya binadamu.

Sheikh Al-Tayyeb pia alionyesha utayari wa Al-Azhar kuongeza msaada wake kwa Waislamu wa Kenya kwa kupanua idadi ya wanafunzi wa Kenya wanaopewa ufadhili wa masomo, pamoja na kutoa mafunzo kwa maimamu wa Kenya kuhusu changamoto za kisasa na mbinu za kuzitatua.

Ushirikiano wa Kibunge

Mnamo tarehe Julai 22, 2019, Dkt. Ali Abdel Aal, Spika wa Bunge la Misri, alitembelea Kenya kwa lengo la kujadili njia za kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili na kubadilishana maoni kuhusu masuala yenye maslahi ya pamoja.

Katika ziara hiyo, Spika wa Bunge la Taifa la Kenya, Justin Muturi, alisisitiza kuwa mahusiano kati ya Misri na Kenya ni ya kimkakati na yanahusisha sekta mbalimbali, zikiwemo siasa, uchumi, utamaduni na ushirikiano wa kibunge. Aidha, alieleza kuwa Kenya ina dhamira ya kuimarisha mahusiano yake na Misri na kunufaika na uzoefu wa Misri katika sekta mbalimbali, kama vile ujenzi wa uwezo kwa vijana, miradi ya miundombinu, pamoja na mbinu za kupambana na ugaidi.

Mahusiano ya Urafiki na Ushirikiano kati ya Misri na Kenya (Maendeleo, Mafunzo, na Misaada)

Mahusiano kati ya Misri na Kenya umeonyesha mshikamano mkubwa wa urafiki na ushirikiano. Misri imejitahidi kutoa msaada wa aina mbalimbali kwa wananchi wa Kenya wakati wa majanga na hali ngumu kama vile ukame na mafuriko. Msaada huu umetolewa kupitia Mfuko wa Kijeshi wa Ushirikiano wa Misri na Afrika pamoja na Wakala wa Ushirikiano wa Misri kwa Maendeleo, taasisi mbili zinazolenga kuimarisha ushirikiano na kutoa msaada wa kiufundi.

Misri na Kenya zimeshirikiana katika sekta mbalimbali kama kilimo, maji, mifugo, ufugaji wa samaki, afya, mawasiliano, usalama, na ujenzi wa uwezo. Aidha, wataalamu wengi wa Kenya wamepata mafunzo nchini Misri katika nyanja kama vile kilimo, uhandisi wa maji, mikakati ya usalama, uuguzi, utalii, huduma za hoteli, anga, diplomasia, masuala ya kijeshi, na usafiri wa anga.

Kituo cha Kimataifa cha Kilimo cha Misri kimetoa mafunzo mengi kuhusu uzalishaji wa kuku, mboga, huduma za kilimo, uchambuzi wa miradi, uzalishaji wa pamba, usimamizi wa wadudu waharibifu, usimamizi wa maji na udongo, pamoja na afya na uzalishaji wa mifugo. Wizara ya Umeme ya Misri pia inatoa ufadhili wa masomo 17 kila mwaka kwa wanafunzi wa Kenya katika sekta ya umeme.
Ushirikiano huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi zote mbili na unachangia maendeleo endelevu na ustawi wa kanda nzima. Miongoni mwa miradi muhimu ni:

Ziara ya Waziri Mkuu wa Misri katika Hospitali ya Kikoptiki ya Misri, Nairobi

Mnamo tarehe Septemba 4, 2023, Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa Madbouly, alitembelea Hospitali ya Kikoptiki ya Misri huko Nairobi, Kenya, wakati wa kushiriki Mkutano wa Tabianchi wa Afrika, akimwakilisha Rais Abdel Fattah El-Sisi. Waziri Mkuu alikagua hospitali hiyo, akitembelea vyumba vya wagonjwa na vifaa vyake, akisisitiza dhamira ya Misri ya kuendelea kusaidia sekta ya afya nchini Kenya.

Hospitali hii ni taasisi ya kiwango cha sita, ambacho ndicho cha juu zaidi nchini Kenya kwa huduma za afya. Ina vitanda vingi, vyumba vya upasuaji vilivyo na vifaa vya kisasa, huduma za wagonjwa mahututi, huduma kwa watoto wachanga, vitengo vya uchunguzi wa mionzi, na maabara yenye cheti cha ISO.

Huduma zinazotolewa ni pamoja na X-ray, MRI, CT scan, matibabu ya saratani, huduma za meno, na tiba ya shinikizo la juu la oksijeni. Hospitali hii imetoa huduma za afya kwa zaidi ya wagonjwa 56,000 wa UKIMWI kupitia Kituo cha Tumaini, huduma ambazo hutolewa bila malipo.

Ushiriki wa Misri katika UN-Habitat

Mnamo tarehe Juni 5, 2023: Waziri wa Nyumba wa Misri, Dkt. Assem El-Gazzar, na Waziri wa Maendeleo ya Mitaa, Luteni Jenerali Hisham Amna, walifungua banda la Misri katika maonesho yaliyoambatana na kikao cha pili cha Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Makazi ya Kibinadamu (UN-Habitat) jijini Nairobi. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Rais wa Kenya, William Ruto, na Dkt. Maimunah Mohd Sharif, Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat.

Ushirikiano wa Teknolojia kati ya Misri na Kenya
Mnamo Machi 2012: Waziri wa Mawasiliano na Habari wa Kenya, Samuel Poghisio, alitembelea Misri kwa ajili ya kusaini makubaliano kadhaa ya ushirikiano katika nyanja za mawasiliano na teknolojia ya habari.

Makubaliano haya yalihusu uanzishwaji na usimamizi wa vijiji vya teknolojia, programu za mafunzo kwa vijana wa Kenya katika sekta ya mawasiliano, na utekelezaji wa mipango ya serikali mtandao (e-government). Mikataba hii ililenga kuboresha miundombinu ya kidigitali, kuhamasisha ujuzi wa Kimasri katika sekta ya teknolojia, na kusaidia mipango ya kikanda ya maendeleo ya sekta ya mawasiliano barani Afrika.

Ushirikiano wa Usafiri na Mawasiliano

Ushirikiano wa usafiri kati ya Misri na Kenya unaonesha dhamira ya mataifa haya mawili katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kuendeleza miundombinu ya usafiri.

Ushirikiano huu unahusisha maeneo kadhaa, yakiwemo maendeleo ya miundombinu, kubadilishana utaalamu na teknolojia, kuimarisha uunganishaji wa kikanda, maendeleo ya miradi mikubwa ya usafiri, na kubadilishana huduma na wataalam.

Mojawapo ya mikutano muhimu katika sekta hii ilifanyika mnamo tarehe Mei 12, 2023, ambapo Balozi Wael Nasr El-Din, balozi wa Misri nchini Kenya, alikutana na Onesmus Kipchumba Murkomen, Waziri wa Barabara, Uchukuzi na Kazi za Umma wa Kenya.

Walijadili njia za ushirikiano wa pamoja na jinsi Kenya inaweza kufaidika na utaalamu wa Misri katika ujenzi wa barabara, uboreshaji wa reli, na maboresho ya usafiri wa umma.

Kwa muhtasari, ushirikiano wa usafiri kati ya Misri na Kenya ni fursa ya kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuboresha mawasiliano kati ya mataifa haya mawili, kuimarisha biashara na kubadilishana utamaduni, na kuchangia maendeleo endelevu.

Ushirikiano wa Mazingira

Ushirikiano wa mazingira kati ya Misri na Kenya ni sehemu muhimu ya uhusiano wao wa pande mbili, kwani mataifa haya mawili yanajitahidi kukuza maendeleo endelevu na kulinda mazingira.

Mkutano muhimu katika sekta hii ulifanyika mnamo tarehe Agosti 19, 2023, ambapo Dkt. Yasmine Fouad, Waziri wa Mazingira wa Misri, alikutana na mwenzake wa Kenya, Soipan Tuya, Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu wa Kenya.

Wakati wa mkutano huo, mawaziri hao waliratibu maandalizi ya Mkutano wa Tabianchi wa Afrika, uliopangwa kufanyika Kenya kati ya Septemba 4 hadi 6, 2023, kwa kushirikisha viongozi na mawaziri kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Kwa muhtasari, ushirikiano wa mazingira kati ya Misri na Kenya ni fursa ya kufanya kazi pamoja katika kulinda mazingira na kukuza maendeleo endelevu, huku ukitoa nafasi ya kubadilishana utaalamu na rasilimali ili kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazofanana.

Kwa kumalizia, ushirikiano kati ya Misri na Kenya umepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uchumi na biashara, utamaduni na elimu, pamoja na ulinzi na usalama.

Mahusiano kati ya Misri na Kenya yanajidhihirisha kama mfano wa ushirikiano wa pande mbili unaojengwa juu ya misingi imara ya imani na kuelewana kwa pande zote. Mahusiano haya pia unaakisi dhamira ya mataifa yote mawili katika kuimarisha amani, utulivu, na maendeleo endelevu.

Kupitia kuendelea kuimarisha mazungumzo yenye kujenga na ushirikiano wa karibu, mataifa haya mawili yanaweza kutazamia mustakabali wenye mafanikio ya pamoja na fursa za maendeleo ya pande zote. Ushirikiano huu pia unadumisha uhusiano wa karibu kati ya wananchi wa mataifa haya mawili na kuweka msingi wa ustawi wa kudumu na utulivu wa kikanda.

Vyanzo

• Mamlaka Kuu kwa Habari 
• Misri na Afrika
• Jarida la Kiuchumi la Kilimo la Misri
• Lango la Habari la Al-Ahram la Kimisri
• Kituo cha Mawazo na Masomo ya Kistratejia cha Misri
• www. Comesa.int
• https://www.bu.edu/africa/outreach/teachingresources/history/colonialism/the-mau-mau-rebellion/