Mhitimu wa Udhamini wa Nasser Achaguliwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Kike wa Kisoshalisti

Jiji kuu la Rabat, Moroko, lilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Vijana wa Kike wa Kisoshalisti-Demokrasia katika Ulimwengu wa Kiarabu, uliofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 30 Mei 2025, kwa kushirikisha wajumbe wa vijana kutoka nchi 16 za Kiarabu na wawakilishi wa mashirika 24 ya kisiasa na kikanda ya vijana. Mkutano huu ulipewa jina la “Kikao cha Palestina” ili kuonyesha mshikamano na kuimarisha msimamo wa vijana wapenda maendeleo katika eneo hilo kuhusu suala la Palestina, kama suala la msingi katika harakati zao. Mkutano huo uliangazia uchaguzi wa uongozi mpya wa umoja huo, ambapo Smiha Laasab alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu, hatua inayoakisi nia ya pamoja ya kuboresha muundo wa uongozi wa umoja huo, kwa kuzingatia usawa wa uwakilishi, uwezo wa kitaaluma, uzoefu, na ushiriki halisi katika masuala ya vijana wa Kiarabu.
Samiha Laasab ni miongoni mwa viongozi chipukizi wenye ushawishi mkubwa katika ulingo wa siasa nchini Moroko. Ni Mjumbe wa Ofisi ya Kitaifa ya Umoja wa Vijana wa Kisoshalisti, na pia Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Kisoshalisti cha Muungano wa Wananchi. Aidha, ni Mhitimu wa kundi la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, mojawapo ya mipango maarufu inayolenga kuwawezesha vijana na kukuza nafasi zao za uongozi. Laasab amejipatia uzoefu mkubwa kwa kushika nafasi mbalimbali katika harakati za wanafunzi, vyama vya wafanyakazi na mashirika ya wanawake. Akiwemo kuwa kiongozi wa kitengo cha wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Ibn Tofail kilichopo Kenitra, mratibu wa wanawake wa ngazi ya mkoa alikotokea, pamoja na majukumu mbalimbali ya kiutawala yameyochangia kukuza uelewa na ustadi wake katika siasa.
Katika hotuba yake mara baada ya kuchaguliwa, Smiha Laassab alisisitiza kuwa kushiriki kwake katika umoja huu wa kikanda kunatokana na asili yake ya kisiasa kama mwanachama wa chama cha mrengo wa kushoto, kinachoamini katika thamani na nafasi ya vijana. Alieleza kuwa Shirikisho la Vijana la Ittihadi nchini Moroko ni sehemu muhimu ya harakati za kijamii za kisoshalisti-demokrasia, katika ngazi ya kitaifa na Kiarabu. Alibainisha kuwa moja ya majukumu yake ya msingi katika nafasi hiyo ni kufungua fursa mpya kwa vijana wa Kiarabu, kuwapatia jukwaa la kweli la kutoa maoni na msimamo wao, pamoja na kulifanya Umoja wa Vijana wa Kisoshalisti Demokrasia katika Ulimwengu wa Kiarabu kuwa jukwaa la maendeleo lenye kuhimiza mazungumzo, kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto na matatizo ya kizazi kipya.
Kikao cha mkutano huo kililenga kuunganisha mitazamo kati ya washiriki wa umoja huo, na kuunda uongozi mpya wa vijana wenye uwezo wa kuendana na mabadiliko ya kisiasa na kijamii katika dunia ya Kiarabu na Afrika. Pia zilijadiliwa njia za kuwawezesha vijana kisiasa, kiuchumi na kijamii, na kuimarisha mchango wao katika kutafuta suluhisho la migogoro iliyopo, hasa ile inayohusiana na mipaka ya baadhi ya nchi. Mkutano ulifanyika katika mazingira ya mazungumzo ya uwajibikaji na majadiliano ya kujenga, yaliyoonesha kiwango cha juu cha uelewa wa changamoto zinazowakabili vijana, pamoja na imani kubwa katika haja ya kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana kikanda ili kufanikisha maendeleo ya haki, na kuhakikisha mustakabali wa utulivu na heshima kwa watu wa eneo hili. Mkutano huu unahesabiwa kuwa hatua muhimu katika historia ya umoja huo, na hatua ya mbele katika kuimarisha mshikamano kati ya vijana wa kisoshalisti wa Kiarabu, sambamba na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kihistoria katika kutetea haki za watu na kujenga mustakabali wenye haki zaidi na usawa.
Katika ujumbe wake kwa vijana, Smiha Laassab – Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Vijana wa Kisoshalisti Demokrasia katika Ulimwengu wa Kiarabu – alisisitiza umuhimu wa kupanua uelewa wa vijana wa siasa na kujifungua kwa uwanja wa kisiasa kama njia kuu ya kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mataifa yao. Alisema: "Sauti ya vijana haisikiki isipokuwa kwa vijana wenzao, na matatizo ya vijana hayaeleweki ila kwao wenyewe." Alieleza kuwa kuwapa vijana nafasi ya kisiasa ni njia ya kuwafikisha katika ngazi za maamuzi na kushiriki katika utungaji wa sera zinazowahusu. Aliongeza kuwa: "Kujihusisha kwa dhati na siasa ndicho kinachowapa vijana uwepo wenye nguvu na athari katika kusanifu mustakabali wa eneo letu." Aliwataka vijana wote – wa kike na wa kiume – kushiriki kwa ufanisi katika maisha ya kisiasa ili kufanikisha mabadiliko ya kweli na endelevu.