Wanawake Katika Zama za Gamal Abdel Nasser

Wanawake Katika Zama za Gamal Abdel Nasser

Imeandikwa na: Radwa Ahmed

Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na maafisa huru kuondoa mfumo wa kifalme na kukomesha ukoloni wa Uingereza na kuanzisha mfumo wa jamuhuri mnamo tarehe Julai 23, 1952 chini ya uongozi wa Gamal Abdel Nasser, nchi ya Misri ilianza safari mpya ya maendeleo. Nasser aliacha mradi ulio na nguzo nane muhimu zilizowakilisha sekta mbalimbali kama vile kijeshi, kisiasa, kiviwanda, kiroho na kidini, haki ya kijamii, upande wa kisanaa na ubunifu, nafasi ya mwanamke katika jamii, na utaifa wa Kiarabu pamoja na upanuzi wa Afrika.

Mapinduzi ya Julai 23 yalileta mabadiliko makubwa katika nyanja nyingi za maisha ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii nchini Misri. Miongoni mwa mabadiliko hayo, athari kubwa zaidi ilikuwa ni kuimarishwa kwa nafasi ya wanawake wa Misri baada ya miaka mingi ya kupuuzwa. Wanawake walipata haki zao za msingi na nafasi muhimu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, na kijamii.

Katika uwanja wa kisiasa, Katiba ya Misri ya mwaka 1956 ilimpa mwanamke haki ya kugombea, kupiga kura, na kutekeleza kanuni ya usawa na mwanamume, hususan katika mishahara na malipo. Kufikia mwaka 1957, mwanamke wa Misri aliweza kushika nyadhifa katika Bunge, kuwa mawaziri, na hata pia kuwa majaji. Miongoni mwa wanawake hawa ni:

- Bi. Rawiya Attiya: Aliyepewa jina la utani la “Mama wa Wapiganaji wa Mashahidi” baada ya uchokozi wa Utatu. Aliwahi kuwa afisa katika jeshi la Misri na ndiye mwanamke wa kwanza aliyeingia katika uchaguzi wa Bunge la Misri na kuwa mbunge.

- Bi. Hakmat Abu Zeid: Aliyeteuliwa na Rais Gamal Abdel Nasser kupitia uamuzi wa rais kuwa Waziri wa Masuala ya Kijamii. Alianzisha miradi mingi kama vile "Waanzilishi wa Vijijini" na "Familia zilizozalisha," na pia aliweka sheria ya kwanza inayodhibiti shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali.

- Aisha Rateb, Aziza Hussein, na wanawake wengine: Walihusika katika kuandika rasimu za mkataba wa kimataifa wa wanawake.

Kijamii, Rais marehemu Gamal Abdel Nasser alikiri haki ya mwanamke kupata elimu. Alifanya elimu kuwa bure na kufungua fursa kwa wanawake kujiunga na shule, wakati ambapo hapo awali elimu ilikuwa ikipatikana zaidi kwa wavulana kutokana na gharama zake za juu.

Kitamaduni, Bi. Aminah Al-Said alikuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Mhariri Mkuu wa jarida la Misri baada ya mapinduzi. Alikuwa pia mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa waandishi wa habari, na zaidi ya hayo, alikuwa Naibu Mkuu wa bodi hiyo na kufanya kazi kama mjumbe wa Baraza la Shura. Aidha, alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake ulioanzishwa na Huda Sharawy.

Hatupaswi kusahau mchango wa mwanamke wa Sinai baada ya Vita ya 1967. Wanawake wa Sinai walikuwa na jukumu kubwa na chanya katika upinzani na pia katika Vita ya Oktoba kwa kusaidia kusafirisha wapiganaji, kuwaponya na kuwasaidia kufika kwenye ardhi za Misri. Hawa wanawake hawakuwa na elimu rasmi au mafunzo, lakini kilichowachochea ni upendo wa nchi. Kila mwanamke alikuwa akiwahamasisha watoto wake kutetea ardhi yao.