Lugha ya Kiswahili Kutoka Kitaifa Hadi Kimataifa

Imeandikwa na/ Radwa Ahmed
Kwa miaka kadhaa, lugha ya Kiswahili imebaki haikutambuliwa kwenye mikutano ya kimataifa au ya Kiafrika, bali ilikuwa ikitumika na raia wa nchi zinazoongea Kiswahili tu. Lakini baadaye, idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili imeongezeka kufikia milioni 200 duniani kote. Jambo hili limefanya Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha kumi zinazozungumzwa zaidi duniani.
Kiswahili hakikuibuka ghafla, bali kimeendelezwa kwa miaka 2000 kukabiliana na mabadiliko mengi. Kwani eneo la pwani hii ni kama njia panda ya kimataifa ya biashara na harakati za binadamu, Kiswahili kilitumika na wengi kama Waafrika katika uhamaji wao wa ndani, wafanyabiashara wa Kiarabu, walowezi wa Kihindi na wazungu, hata kikajulikana katika nchi nyingine.
Mnamo tarehe Septemba 11, 2017, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio la kutenga siku kwa kila lugha rasmi zinazokuwepo barazani kwa ajili ya kuhabarisha na kuelimisha kuhusu historia, utamaduni na matumizi ya kila lugha. Kwa hivyo, Shirika la UNESCO tarehe Novemba 23, 2021, lilitangaza kuwa siku ya saba Julai kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani.
Siku hii imechaguliwa hasa kwani Umoja wa Taifa wa Tanganyika wa Afrika chini ya kiongozi Julius Nyerere kupitia mkutano wa vijana wa Tanzania uliofanyika Dar-es-Salaam, siku ya saba Julai mwaka 1954 ulitangaza kwamba Kiswahili ni nguzo muhimu kwenye mapambano ya uhuru.
Lugha ya Kiswahili ikawa na athari kubwa kwenye majukwaa ya kimataifa kama mashirika na vyeo vikuu vya kimataifa, kwani ikawa ikifundishwa katika vyuo vikuu vingi vya Misri na Libya. Kiswahili inatumika pia katika idhaa kadhaa za kimataifa kama vile: BBC, DW, VOA na idhaa zinazolenga Kairo, Beijing, na Moscow. Siyo hayo tu, pia maneno ya Kiswahili yametumika kwenye filamu na vipindi kama vile: “Bibo na Bashir”, filamu ya “Out of Africa” iliyoigizwa na Meryl Streep, filamu ya “Lara Croft: Tomb Raider” iliyoigizwa na Angelina Jolie na hatimaye filamu maarufu ya Disney “The Lion King” yenye msemo maarufu zaidi “Hakuna Matata” unaomaanisha hakuna tatizo lolote.
Ama katika Afrika, lugha ya Kiswahili imeshuhudia maendeleo mengi: mnamo tarehe Februari 10, 2022, Shirika la Umoja wa Afrika lilitoa tamko kuwa Kiswahili ni lugha rasmi ya kazi. Tamko hilo lilitangazwa kufuatia ombi la Naibu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango, wakati wa mkutano wa kilele wa 35 wa Marais na Serikali za nchi za Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, akisema: “Lugha ya Kiswahili ndiyo inatumika katika jamii nyingi pamoja na kufundishwa katika nchi kadhaa za Kiafrika”.
Mnamo mwaka 2017, Bunge la Rwanda lilipitia na kupitisha kufanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kazi, pamoja na kufundishwa katika shule. Mwaka 2020, Afrika Kusini ilitekeleza azimio la kufundisha Kiswahili shuleni kama somo la hiari. Jambo hilo ni kama fursa ya kuwaandaa wanafunzi wa Afrika Kusini kwa mwingiliano na mawasiliano kwenye uwanja wa biashara.
Mnamo mwaka 2019, Serikali ya Uganda ilikubali kuanzisha Baraza la Kiswahili la Taifa, ambapo katiba ya Uganda imeeleza kwamba Kiswahili ni lugha rasmi ya pili nchini Uganda. Lakini matumizi yake yanategemea masharti yanayowekwa na bunge. Mwaka huo huo, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ilitangaza Kiswahili kama lugha rasmi ya nne.
Teknolojia imechangia sana kuenea kwa Kiswahili pamoja na mchango wa taasisi za kisayansi na kitamaduni. Jambo hilo limesaidia kurahisisha mawasiliano na kukuza mahusiano baina ya watu mbalimbali.