Aya Chebbi: Mwanaharakati wa Tunisia Anayeongoza Sauti za Vijana na Wanawake Barani Afrika

Aya Chebbi: Mwanaharakati wa Tunisia Anayeongoza Sauti za Vijana na Wanawake Barani Afrika

Imeandikwa na: Basmala El-Ghazaly
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Aya Chebbi, mwanaharakati wa Tunisia na mwanadiplomasia mashuhuri, amejitokeza kama mmoja wa sauti kuu katika kutetea haki za vijana na wanawake barani Afrika. Kupitia safari yake iliyojaa mafanikio, amekuwa alama ya mabadiliko chanya na utendaji bora.

Aya Chebbi alizaliwa katika mji wa Dahmani, mkoa wa El-Kaf nchini Tunisia mnamo mwaka 1988. Alipata shahada ya kwanza katika mahusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Tunis El Manar, kisha akapata shahada ya uzamili katika siasa za Afrika kutoka Chuo Kikuu cha London. Pia alikuwa mtafiti katika Chuo Kikuu cha Georgia Kusini, jambo lililomsaidia kupata uelewa mpana wa masuala ya kimataifa na ya kikanda.

Aya alijitokeza wakati wa mapinduzi ya Tunisia mwaka 2010 kama mwandishi wa kisiasa, akitumia majukwaa yake kuelezea matarajio ya vijana kuhusu demokrasia na uhuru. Aidha, alifanya kazi katika kambi za wakimbizi wakati wa mapinduzi ya Libya mwaka 2011, na mwaka 2012 alishiriki katika uangalizi wa uchaguzi wa rais nchini Misri kwa kushirikiana na Kituo cha Carter, hatua iliyoakisi dhamira yake kubwa kwa masuala ya kisiasa na kijamii.

Mnamo Novemba 2018, aliteuliwa kuwa mjumbe maalum wa vijana katika Umoja wa Afrika, na hivyo kuwa mwanadiplomasia mdogo zaidi katika uongozi wa Tume ya Umoja wa Afrika. Wakati wa muhula wake, alifanya ziara 73 katika nchi 35 za Afrika na kukutana na zaidi ya maafisa wa serikali 160, jambo lililochangia kuimarisha ushiriki wa vijana katika kufanya maamuzi.

Aya alianzisha Harakati za Vijana wa Afrika (AY) mnamo mwaka 2012, zimezokua na kufikia wanaharakati zaidi ya 10,000 kutoka nchi 40. Pia alizindua programu ya “Vijana kwa Ajili ya Kunyamazisha Bunduki”, ambayo imekuwa jukwaa kuu la Umoja wa Afrika katika kuendeleza amani na usalama. Kupitia jitihada hizo, aliandaa zaidi ya mijadala 100 baina ya vizazi, iliyohusisha vijana 150,000 wa Kiafrika, ikiashiria uwezo wake wa kipekee wa kuwaunganisha vijana kwa ajili ya mabadiliko chanya.

Aya Chebbi alitunukiwa Tuzo ya Pioneer kutoka mtandao wa GIMAC mnamo Februari 2022, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuwawezesha wanawake na kukuza usawa wa kijinsia. Pia aliwekwa kwenye orodha ya Forbes ya wanawake 50 wenye nguvu zaidi barani Afrika mwaka 2020, jambo linalodhihirisha ushawishi wake mkubwa katika bara hili.

Aya Chebbi ni mfano wa kuigwa kwa wanawake wa Kiarabu na Kiafrika katika uongozi na mabadiliko ya kijamii. Kupitia mipango yake na ushiriki wake wa kimataifa, ameonesha kuwa vijana wanaweza kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii zao. Safari yake imejaa funzo na hamasa kwa vizazi vijavyo.