Utamaduni na Mapinduzi ya Julai ya Misri

Utamaduni na Mapinduzi ya Julai ya Misri

Imeandikwa na: Al-Sayeda Tarek 

Mapinduzi ya Julai 23, 1952 yana umuhimu mkubwa katika historia ya Misri, kwani mapinduzi hayakuacha kuathiri mambo ya kisiasa na kiuchumi tu, lakini athari zake zilienea kujumuisha maisha ya kitamaduni katika vipimo vyake mbalimbali, kwani mabadiliko makubwa yalitokea katika sanaa, fasihi na elimu kufuatia mapinduzi haya, yaliyochangia kuundwa kwa utambulisho mpya wa kitamaduni kwa jamii ya Misri.

Mapinduzi ya Julai 23 hayakuwa tu mapinduzi ya kijeshi, bali pia mapinduzi ya kitamaduni, kwani mapinduzi haya yalichangia kuibuka kwa sauti mpya za fasihi zinazoelezea uzoefu wa makundi yaliyotengwa, kama vile Ihsan Abdul Quddus na Youssef Al-Sibai, pamoja na waandishi wengine waliofuatilia rushwa ya kisiasa na kijamii kabla ya mapinduzi ya Julai 23, kama vile Gamal Hammad katika riwaya yake "Macheo na Machweo(Sunrise and Sunset)", na riwaya "Ardhi" na Abdul Rahman Al-Sharqawi, inayoonesha mateso ya mkulima wa Misri wakati wa kipindi cha uvamizi.

Tamthilia zimekuwa mojawapo ya njia zinazotumiwa kueneza mawazo ya kimapinduzi na kuongeza uelewa wa kitaifa, kwani baadhi ya michezo ilishughulikia masuala ya mapinduzi na mabadiliko ya kijamii, pamoja na kuchukua jukumu kubwa katika kuelimisha umma na kueneza ujumbe wa mapinduzi. Yusuf Wehbe ni mmoja wa watu maarufu waliokuwa wakitumia ukumbi wa michezo kama chombo cha kuelezea matumaini na matarajio ya watu.

Elimu pia ni mojawapo ya mambo ambayo mapinduzi hayo yalijikita zaidi, kwani yalizingatia kueneza elimu bila malipo na kuboresha mfumo wa elimu, pamoja na kuanzisha shule na vyuo vikuu vingi. Hali hii ilichangia kutoa fursa za elimu kwa makundi makubwa ya jamii ambayo hapo awali yalinyimwa fursa hizo, na ilisaidia kuongeza asilimia ya wanafunzi na kuongeza uelewa wa kitamaduni na kisayansi.

Mapinduzi ya Julai 23, 1952, yalikuwa mojawapo ya mambo muhimu zaidi ya kubadilisha utamaduni nchini Misri. Hili lilichangia kufanya Misri iwe mnara kwa taifa la Kiarabu na kuimarisha utambulisho wa kitaifa. Rais Gamal Abdel Nasser alianzisha Wizara ya kwanza inayohusu mambo ya kitamaduni nchini Misri mwaka 1958. Wizara hiyo ilikuwa na jukumu kubwa katika harakati za kutafsiri na uwazi kwa tamaduni za kigeni. Mamlaka ya Jumla ya Kitabu na Ufasiri ni mojawapo ya taasisi zilizoanzishwa ili kukidhi mahitaji ya Wizara ya Utamaduni katika uwanja wa kutafsiri na kuchapisha.