Kiswahili ni Mustakbali wa Afrika

Imeandikwa na: Engy Mohammed
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili/ Mervat Sakr
Bila shaka, lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho binadamu hawezi kuacha. Barani mwetu Afrika kuna lugha nyingi sana, na kila lugha ina kisa chake cha kipekee.
Lugha ya Kiswahili ilianza kuenea tangu kuenea kwa Uislamu barani Afrika. Mwanzoni, ilikuwa ikiandikwa kwa herufi za Kiarabu, lakini wakati wa ukoloni, herufi za Kiarabu zilibadilishwa kuwa herufi za Kirumi. Baada ya kumalizika kwa ukoloni hasa katika Mashariki ya Afrika, Kiswahili imekuwa lugha rasmi katika nchi kama Tanzania na Kenya.
Kulingana na takwimu, idadi ya watu wanaozungumza Kiswahili imefikia milioni 200, na idadi hii ni kubwa sana. Pia, lugha ya Kiswahili ni kati ya lugha kumi zinazozungumzwa zaidi duniani. Kiswahili imepata hadhi kubwa zaidi barani Afrika, ambapo imekuwa lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na pia lugha rasmi katika Umoja wa Afrika (AU).
Mnamo tarehe Novemba 23, 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), liliteua Julai 7 kuwa siku rasmi ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani. Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa. Sababu ya kuchagua tarehe Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani ni kwamba Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, mnamo tarehe Julai 7, 1954 alitangaza kuwa Kiswahili kilikuwa chombo muhimu katika harakati za kukabiliana na ukoloni
Kiswahili pia ni lugha ya kwanza ya Kiafrika inayotumika katika kompyuta kote barani Afrika. Watengenezaji programu walichagua lugha ya Kiswahili kwa sababu nyingi na mbalimbali, ikiwemo umaarufu wake, urahisi wa kujifunza, na matumizi yake makubwa barani Afrika. Pia, Kiswahili imepata umaarufu na kuungwa mkono katika Mashariki ya Kati, Amerika, Ulaya, na nchi nyingine.
Ingawa lugha ya Kiswahili haikuwa maarufu sana mwanzoni, leo imekuwa lugha muhimu katika jamii ya kimataifa, na leo tunaadhimisha nayo, mnamo tarehe Julai 7, 2024.