Kusherehekea Siku ya Kiswahili Duniani: Kuimarisha Utambulisho wa Kitamaduni na Kiafrika

Imeandikwa na: Ebrahim Al-Sqqa
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili/ Mervat Sakr
Mnamo tarehe Julai 7 kila mwaka ni siku adhimu sana kwa nchi nyingi za Afrika, basi kwamba siku hii ni nafasi ya kuboresha utambulisho wa kitamaduni na Lugha ya Kiswahili kama lugha ya pamoja inayowaunganisha watu wa Bara hilo la Afrika. Pia, watu wa upande wa Mashariki na Kusini mwa Afrika husherehekea siku hii kila mwaka kwa lengo la kuangazia umuhimu wa kihistoria na kitamaduni wa lugha hii inayozungumzwa na mamilioni ya watu; hasa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Umuhimu wa Kiswahili: Lugha ya Kiswahili si Lugha ya kuwasiliana tu kati ya watu, bali ni upande muhimu sana wa urithi wa utamaduni wa Afrika. Kiswahili ni Lugha rasmi katika nchi nyingi kama Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Congo. Pia, inatumika kama Lugha ya Pamoja kwenye maeneo mapana ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, jambo linaloifanya chombo muhimu sana cha kuwasiliana kati ya asili na utamaduni mbalimbali ndani ya Bara hilo.
Sherehe zake zina shughuli nyingi za kitamaduni na kielimu. Basi siku hii inaanzishwa kwa warsha na mihadhara inayolenga kuelimisha na kuimarisha matumizi yake, pamoja na maonesho ya muziki na tamthilia inayoonesha urithi wa kitamaduni wa jamii zinazozungumza Kiswahili. Matukio haya ni nafasi ya kubadilishana utamaduni na kujua historia ya pamoja. Pia, siku hii inajumuisha tamasha za kitamaduni, mikutano na makongamano, warsha, shughuli za kiadabu pamoja na sherehe kupitia vyombo vya habari.
Siku hii inaimarisha utambulisho wa kitamaduni na Kiafrika kwa njia kadhaa. Lugha ya Kiswahili inachukuliwa kuwa lugha ya pamoja katika Afrika Mashariki, na hivyo inaimarisha umoja na kuelewana kati ya nchi mbalimbali za eneo hilo. Maadhimisho hayo yanachangia katika kuhifadhi urithi wa lugha na utamaduni na kuhamisha maadili na desturi kutoka kizazi kimoja hadi kingine, jambo linaloimarisha utambulisho wa Kiafrika na kuwafanya watu kujivunia na kuhisi kuwa sehemu ya bara lao. Pia ni fursa ya kueneza uelewa kuhusu fasihi, sanaa, na muziki wa Kiswahili, jambo linaloboresha utamaduni wa Kiafrika na kuongeza thamani yake kimataifa. Zaidi ya hayo, yanaimarisha mawasiliano na biashara kati ya nchi za Kiafrika, hivyo kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano wa kikanda. Kuadhimisha siku hii kunadhihirisha umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika kuimarisha umoja wa kitamaduni na maendeleo endelevu katika bara la Afrika.
Mwishoni, siku ya Kiswahili siyo tu sherehe, bali ni ukumbusho wa umuhimu wa kuhifadhi urithi wetu wa lugha na kitamaduni. Pia, siku hii inaimarisha fahari na mshikamano na kuchangia kuboresha maelewano na mawasiliano kati ya watu kupitia lugha inayowaunganisha mamilioni ya nyoyo. Hebu tusherehekee kwa shauku na tuendelee kuunga mkono na kueneza lugha hii nzuri ili iendelee kuwa hai na angavu kwa vizazi vijavyo.