SHAABAN ROBERT - ALMASI ILIYOTELEKEZWA

Imeandikwa na: Gwamaka Mwamasage
Imepita takribani miaka 63 tangu gwiji wa fasihi, Sheikh Shaaban Robert, afariki dunia. Amezaliwa tarehe Januari 1, 1909 katika Kijiji cha Vibambani na kufariki dunia Juni 22, 1962, kisha akazikwa kijijini Machui.
Watu wengi huchanganyikiwa na mchanganyiko wa majina yake; jina la kwanza linaashiria imani ya Kiislamu, na la pili linaashiria Ukristo. Inasemekana jina la Robert lilitokana na Ofisa mmoja wa Kiitaliano aliyekuwa mwajiri wa babu yake Shaaban.
Pia, inasimuliwa kuwa bibi yake Shaaban alipokuwa mjamzito alipata uchungu akiwa akianika uduvi katika fukwe za Kurasini na kujifungua hapo hapo. Hivyo, mtoto huyo akapewa jina la Ufukwe. Kwa mantiki hiyo, baba yake Shaaban hapo awali aliitwa Ufukwe. Baadaye, mwajiri wa babu yake alipendekeza mtoto aitwe kwa jina lake, yaani Roberto. Hivyo, baba yake akaitwa Roberto, na Shaaban alipozaliwa akaitwa Shaaban Roberto. Alipoanza shule, kwa kuwa alisoma shule za Kiingereza, jina hilo likabadilika kuwa Roberts na kisha Robert.
Kikabila, Shaaban alikuwa Myao, lakini alichagua kujitambulisha kama Mswahili. Historia yake ilichangia msimamo huu kwani aliishi zaidi jijini Dar es Salaam, ambako alipata elimu ya msingi kati ya mwaka 1922 na 1926 katika Shule ya Msingi Msimbazi.
Sheikh Shaaban Robert anatambulika kama gwiji wa ushairi ndani na nje ya Tanzania, hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kutokana na kazi zake zilizolenga kuamsha fikra mpya kuhusu utu, uhuru, usawa wa kijinsia, utawala bora na kukuza Kiswahili.
Katika uhai wake, anakadiriwa kuandika vitabu 24, vikiwemo Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti binti Saad, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Kitabu chake cha Kusadikika ndicho kilichojulikana zaidi. Inadaiwa pia ipo miswada mingi ambayo haijachapishwa hadi leo, na Taasisi ya Uchunguzi na Ukuzaji Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inaendelea kukusanya kazi zake.
Aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (E.A. Swahili Language Committee), mjumbe wa East African Literature Bureau, na pia wa Tanganyika Languages Board. Kutokana na mchango wake mkubwa, alitunukiwa nishani ya MBE (Member of the British Empire) na pia tuzo ya Margareth Memorial Prize. Mwalimu Julius Nyerere naye alimpa tuzo ya fasihi iliyotukuka kutokana na mchango wake katika jamii ya Tanganyika na baadaye Tanzania, japo kwa bahati mbaya wakati huo alikuwa tayari ameshafariki.
Katika maisha yake ya kifamilia, Shaaban Robert alifanikiwa kuoa wake watatu na kubarikiwa watoto kumi. Maradhi ya moyo na upungufu wa damu vilikatisha uhai wake akiwa amestaafu utumishi wa umma. Baada ya kumaliza darasa la 11, alianza kazi ya karani serikalini chini ya utawala wa kikoloni. Kuanzia mwaka 1926 hadi 1944 alihudumu kama afisa wa forodha katika bandari mbalimbali, hasa Pangani na Bagamoyo. Kuanzia mwaka 1944 hadi 1946 alihamishiwa Morogoro katika ofisi ya mbuga za wanyama, na baadaye kuanzia mwaka 1946 hadi 1952 aliendelea Tanga katika ofisi ya kupima ramani hadi alipostaafu.
Licha ya umahiri na mchango mkubwa wa gwiji huyu, malalo yake ya milele yameachwa katika hali duni na isiyo na staha. Kaburi lake lipo kichakani, bila kumbukumbu wala maandishi ya kutosha kumtambulisha. Hata maandishi ya Kiarabu yaliyokuwa na jina na tarehe zake yamefutika. Familia yake mara kadhaa imelalamika kutonufaika na jina la ndugu yao, kwani watu wengi wanaokuja kutalii kaburi hilo hupelekwa kinyemela na wageni kupata kipato bila kushirikisha familia. Maktaba iliyopo ni banda dogo lisilo na hadhi, lililojengwa na mtu mmoja mwenye mapenzi mema kwa mwanafasihi huyo, anayeitwa Semfuko.
Ndugu wa Shaaban Robert wanatoa wito kwa serikali na wanazuoni kulitazama upya suala hili, kwani kazi zake zimewazalisha wasomi wengi na mchango wake katika taifa ni mkubwa.