MWANAMKE WA KIAFRIKA NA USAWA WA KIJINSIA

Imeandikwa na: Eva Mrema
Usawa wa kijinsia si jambo baya, vivyo hivyo kuamini katika haki sawa za kibinadamu si kosa. Changamoto kubwa kwa baadhi ya nchi barani Afrika ni utoaji wa elimu sahihi inayooana na tamaduni na asili yetu.
Hapo awali, mwanamke wa Kiafrika alikuwa moyo wa jamii yake. Huwezi kugawanya moyo vipande, hivyo ilikuwa fahari kwake kuwa mlezi wa maadili, mwalimu wa kwanza, mkulima, mtunzaji wa nyumba, mhifadhi wa utamaduni na mama wa wote.
Leo hii, katika baadhi ya jamii, majukumu haya yanaonekana kama aina ya utumwa. Hali hii imesababisha mmomonyoko wa maadili na familia nyingi kukosa uwiano. Ninasisitiza daima: mwanaume ana majukumu makubwa, na mwanamke ana majukumu mengi. Hapa tunazungumzia “nguvu” kwa mwanaume na “utayari” kwa mwanamke.
Kukubali kushiriki katika uumbaji pekee ni sababu ya kumbusha kuwa mwanamke hatakiwi kushindana na mwanaume wala kudhani ana nguvu sawa naye. Uwepo wa misuli inayofanana kati ya wanaume na wanawake si ishara ya uwezo sawa. Kuna mipaka iliyokuwepo, na natamani irejee.
Imani ya kwamba wako sawa imesababisha baadhi ya wanawake kuukana utu wao wa asili, na baadhi ya wanaume kuikimbia jinsia yao, kwa sababu ya dhana ya haki sawa. Hivyo kuna haja ya majukwaa ya Kiafrika yanayoshughulikia ustawi wa binti na mwanamke, kurudi nyuma kidogo na kuweka bayana vipengele vinavyohusu usawa huu.
Naam, usawa wa haki za kibinadamu upo, lakini mara nyingine hugongana na mitazamo potofu tunayopokezana. Usawa huu unahakikisha kila binadamu ana haki ya kuishi, kupata elimu, kutafuta kipato, kuchagua mwenza na kuishi bila shinikizo. Hata hivyo, kubaki tu katika hoja ya “haki sawa” ni sawa na kila mtu kushindania anachodhani ni chake.
Mwanamke hujitahidi kuonyesha kuwa bora kuliko mwanaume ili athibitishe kuwa wako sawa. Hufanya mambo makubwa kuliko uwezo wake, huumia, na hutumia kila kitu alichonacho kuthibitisha kuwa hana tofauti na mwanaume. Lakini ukweli ni kwamba, tofauti ipo, kubwa sana.
Ni vyema tutambue kwamba mwanamke na mwanaume si wapinzani, bali ni washirika wa asili. Tukigawana majukumu kwa usahihi, kila mmoja akitambua ndoto, maono na wito wake wa kubadili dunia, basi tutaijenga dunia salama kwa vizazi vijavyo.
Wito wangu kama mwanamke kijana ninayetaka Afrika salama ya kesho:
• Elimu sahihi ya jinsi na jinsia: Elimu hii ndiyo nguzo ya kulinda utamaduni, heshima na mipaka isiyomuumiza yeyote. Watoto wa kike na wa kiume wafundishwe kuukubali uumbaji, kukubali jinsia zao na majukumu yake.
• Elimu na hamasa ya kijinsia kwa wote: Si wanawake pekee hupitia ukatili. Katika jamii nyingi, mwanaume akisema amefanyiwa ukatili na mwanamke huonekana fedheha. Elimu jumuishi itakumbusha wote nafasi zao, nguvu zao na namna ya kushirikiana bila mmoja kumwona mwenzake kama tishio.
• Majukwaa ya kumjenga mwanamke yapewe mwongozo: Majukwaa haya yazingatie misingi ya Kiafrika, tamaduni na malengo ya kimaadili.
Kuna usawa wa haki. Kila mmoja ana haki kupata stahiki zake ndani ya mwongozo wa jinsia yake. Hivyo basi, hakuna haja ya kugawana kila mmoja abaki na asilimia mia yake.