Mafanikio ya Misri katika Nyanja ya Afya: Hatua Hadi Mustakabali Yenye Afya Bora

Imeandikwa na: Hager Ragab Eisobky
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Uwanja wa afya umeshuhudia mafanikio muhimu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita nchini Misri, katika viwango mbalimbali, ndani ya mfumo wa taifa wa 2030 unaolenga kuboresha ubora wa maisha na kutoa huduma kamili za afya kwa raia wote. Mafanikio haya ni kielelezo cha juhudi zinazoendelea kutoka kwa serikali ya Misri ili kuimarisha miundombinu ya afya na kuhakikisha usawa katika usambazaji wa huduma za afya.
Sekta ya afya imepata mafanikio makubwa ya kipekee katika kipindi cha miaka kumi tangu Rais Abdel Fattah El-Sisi alipochukua madaraka. Afya ilikuwa kipaumbele cha juu kwa Rais Sisi, jambo lililodhihirika kupitia mipango mingi ya afya iliyolenga makundi mbalimbali ya watu. Kwa kipindi chote hicho, alijitahidi kutoa huduma za afya zenye ubora wa juu kwa Wamisri wote, sambamba na kuzindua mipango ya dharura ya kiafya ili kuboresha ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Mara baada ya Rais El-Sisi kuchukua madaraka, Misri ilitangaza vita dhidi ya virusi vya "Hepatitis C" kwa kuzindua mpango wa kitaifa wa uchunguzi na matibabu bure. Mpango huo uliwezesha uchunguzi kwa watu milioni 58, na wagonjwa milioni 2.5 waliwekwa kwenye orodha ya matibabu. Lengo kuu lilikuwa kutangaza "Misri haina Hepatitis C", hasa ikizingatiwa kuwa hapo awali ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo.
Mpango huo pia ulilenga kuchunguza magonjwa yasiyoambukiza. Takriban watu milioni 50 walifanyiwa uchunguzi wa kiafya, huku wagonjwa milioni 1.8 wa kisukari na milioni 10 wa shinikizo la damu wakipatiwa dawa.
Mpango huu ulizinduliwa mwezi Julai 2019 kwa lengo la kutoa uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti, magonjwa yasiyoambukiza, na afya ya uzazi kwa wanawake. Pia ulilenga kutoa matibabu bure kwa kutumia miongozo ya kisasa ya kimataifa kwa takriban wanawake milioni 30 kote nchini.
Gharama ya jumla ya mpango huu ilifikia takriban paundi milioni 602 kufikia Juni 2021. Wizara ya Afya na Idadi ya Watu ilitangaza kuwa wanawake 23,906,809 walifanyiwa uchunguzi kama sehemu ya Mpango wa Rais wa Jamhuri wa Kusaidia Afya ya Mwanamke wa Kimasri.
Hospitali za vyuo vikuu pia zimepata maendeleo makubwa katika kipindi cha uongozi wa Rais El-Sisi. Wizara ya Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi ilitangaza maendeleo yasiyo ya kawaida katika hospitali za vyuo vikuu. Mfumo wa huduma za afya uliongezeka ili kuimarisha huduma kwa wananchi, ambapo idadi ya hospitali hizo iliongezeka kutoka 89 mwaka 2014 hadi 120 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 35%.
Katika kauli ya awali ya Waziri wa Afya wa Misri, Dkt. Khaled Abdel Ghaffar, alieleza kuwa hospitali za vyuo vikuu hutoa huduma kwa sehemu kubwa ya wananchi. Aliongeza kuwa sekta ya afya imepewa kipaumbele kikubwa katika bajeti ya serikali, huku idadi ya hospitali hizo ikifikia 115, zikiwa zimesambazwa kote nchini na zinapokea wananchi kila siku kwa ajili ya huduma za kiafya bila malipo. Hospitali hizo hufanya shughuli zao kwa weledi wa hali ya juu na usahihi kamili.
Kuna mafanikio mengine makubwa ambayo hayakutajwa katika makala haya, lakini ni ushahidi halisi unaoonekana nchini Misri. Mafanikio haya katika sekta ya afya ni hatua muhimu kuelekea mfumo wa afya kamili, unaohakikisha maisha bora kwa raia wote na kuakisi juhudi za serikali katika kujenga mustakabali wenye afya bora na utulivu zaidi.