Dkt. Saeed Al-Batouti aandika: Utalii wa Fedha

Imetafsiriwa na: Malak Abd-Elnasser Abdelazeim
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Kwa mujibu wa mabadiliko ya kidemografia na dhana mpya ya uchumi wa fedha (Silver Economy), utalii wa fedha ni aina ya utalii inayotoa masomo muhimu kwa sekta ya utalii ili kufaidika na fursa zinazotokana na mwenendo wa kidemografia. Hii inafanikishwa kwa kuendeleza bidhaa na huduma za utalii zilizobuniwa mahsusi ili kukidhi mahitaji ya wazee, sambamba na kutoa mafunzo ya taaluma mbalimbali kwa rasilimali watu. Hatua hii inatoa mtazamo wa kina unaowezesha kuunda bidhaa za utalii zenye ushindani, kuwaweka wazee katikati ya mchakato, na kutoa huduma zinazowaletea uzoefu bora.
Utalii wa fedha unajumuisha shughuli nyingi za kiuchumi, kama vile kazi za mashirika ya usafiri, ofisi za taarifa za utalii, burudani, usafiri, urithi wa kitamaduni, huduma za afya na ustawi, pamoja na shughuli nyingine zinazokamilisha mbinu jumuishi ya utalii wa wazee.
Mwelekeo huu una athari kubwa katika ongezeko la mahitaji ya utalii, jambo linalolazimu sekta kufikiria upya bidhaa, huduma na shughuli zake. Kulingana na Eurostat, mnamo mwaka 2015 watalii wenye umri wa kati ya miaka 55–65 walichangia asilimia 15.3 ya soko la jumla la utalii, huku wale wenye umri wa miaka 65 au zaidi wakichangia asilimia 17.7.
Ni dhahiri kuwa utalii wa fedha utakuwa na nafasi muhimu katika sekta ya utalii duniani kote, ambapo inakadiriwa kwamba kufikia mwaka 2050, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60 watakuwa asilimia 22 ya idadi ya watu duniani, soko linalotarajiwa kufikia zaidi ya watu bilioni 2.
Kundi hili la wasafiri mara nyingi lina uwezo wa kifedha wa kusafiri, likitumia takriban dola bilioni 30 kila mwaka kwa safari na utalii. Zaidi ya hapo, asilimia 70 ya abiria wa meli za kitalii wanatoka katika kundi hili, huku matumizi yao wakati wa kusafiri yakiwa juu kwa asilimia 74 ikilinganishwa na kundi la umri wa miaka 18–49.
Katika jamii nyingi, kundi hili limekuwa likizingatia zaidi elimu binafsi na kuchukulia utalii pamoja na burudani kama zawadi inayostahili baada ya maisha ya kazi yenye kujitolea. Wazee wa sasa husafiri mara kwa mara (kwa wastani mara 4–5 kwa mwaka) na mara nyingi hugharamia safari zao kwa urahisi, kwani wamefikia hatua ambapo watoto wao hawawategemei tena na hawana madeni ya kifedha, bali wana rasilimali za kutosha kugharamia mahitaji yao.
Wasafiri wazee wanabadilika na kuendelea, na kuna uwezekano mkubwa wa kuwa miongoni mwa mabadiliko muhimu ya kijamii kwa sekta mbalimbali, ikiwemo masoko ya ajira, masoko ya kifedha, makazi, usafiri, pamoja na mabadiliko katika muundo wa familia na mahusiano ya vizazi.
Kwa sasa, kundi hili la umri linazingatia zaidi shughuli za kimwili, ambazo ni sehemu muhimu ya mtindo wa maisha wenye afya. Watu wanaishi kwa muda mrefu na wanajiona wakiwa na afya bora zaidi kuliko vizazi vilivyotangulia. Shughuli hizi zinajumuisha si tu kutembea, kuogelea, kupiga mbizi, kupiga makasia na uvuvi, bali pia mazoezi ya viungo, madarasa ya yoga, kumbi za mazoezi zilizo na vifaa kamili pamoja na wakufunzi, kupanda farasi, kucheza dansi na hata kushiriki katika uzoefu wa upishi.
Kwa sasa, katika mitindo mingi ya safari, msafiri mzee amekuwa kichocheo cha kuvutia kwa aina mbalimbali za utalii: utalii wa mazingira, safari za kusisimua, utalii wa tiba, safari za vizazi mbalimbali, pamoja na likizo za shauku na mapendeleo (kuchanganya mapumziko na shauku ya uchoraji, kujifunza lugha, kukusanya vitu vya kale, vyakula na vinywaji, madarasa ya upishi, pamoja na vipengele vya kiroho wakati wa kusafiri).
Utofauti huu wa maslahi unamaanisha kuwa kuna fursa kubwa kwa masoko maalumu ya utalii kutoa huduma kwa soko hili lengwa.