Dkt. Saeed Al-Batouti aandika: Utalii wa kupita kiasi

Dkt. Saeed Al-Batouti aandika: Utalii wa kupita kiasi

Imetafsiriwa na: Basmala El-Ghazaly
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Tunaiweza kuielezea kwa urahisi kama “Athari mbaya za utalii kwa eneo la utalii au sehemu zake, na kwa ubora wa maisha ya wananchi au aina na ubora wa uzoefu wa wageni.”

Utalii wa kupita kiasi (Overtourism) ni kinyume cha utalii wa kuwajibika (Responsible Tourism), ambao unahusu kutumia utalii kuunda maeneo na jamii bora zaidi kwa wenyeji na ziara bora zaidi kwa wageni.

Kuna changamoto kubwa zinazokabili maeneo mengi ya utalii, na mojawapo ya changamoto kuu ni usimamizi wa mitiririko ya kiutalii inayoongezeka katika maeneo ya mijini na athari za utalii kwa miji na wakazi wake.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni za sehemu ya Idadi ya Watu ya Idara ya Kiuchumi na Kijamii cha Umoja wa Mataifa (UN), asilimia 55 ya watu duniani wanaishi katika maeneo ya mijini, na ifikapo mwaka 2050, inatarajiwa kwamba asilimia hii itaongezeka hadi 68%.

Takwimu zinaonesha kuwa upanuzi wa miji na uhamaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini unaweza kuongeza takriban watu bilioni 2.5 katika maeneo ya mijini ifikapo mwaka 2050, huku takriban asilimia 90 ya ongezeko hili hutokea barani Asia na Afrika.

Ongezeko la idadi ya watalii zaidi kuliko uwezo wa eneo lolote kwa hakika linaathiri vibaya rasilimali za asili, pamoja na athari zingine za kijamii. Pia, linazidisha shinikizo kwa miundombinu, usafiri, na huduma nyingine za msingi.

Kwa hiyo, usimamizi mzuri wa maeneo ya utalii, tathmini zilizoendelea za uwezo wa kubeba wageni (Carrying Capacity), na uwiano kati ya maslahi ya wageni na ya wenyeji, ni suala la msingi katika sekta ya utalii. Hili ni jukumu muhimu kwa mamlaka za mitaa katika maeneo ya utalii, wadau wa sekta ya utalii, na serikali.

Uwezo wa kubeba watalii (Tourism’s Carrying Capacity) umeelezewa kama “idadi juu zaidi ya watu wanaoweza kutembelea eneo la utalii kwa wakati mmoja bila kusababisha uharibifu wa mazingira ya kimwili, kiuchumi, kijamii, na kitamaduni, au kuathiri vibaya kiwango cha kuridhika kwa wageni (Quality of visitors’ satisfaction).”
Utalii hauwezi kuwa endelevu isipokuwa ukiboreshwa na kusimamiwa kwa kuzingatia iwe wageni na jamii za wenyeji.

Kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya utalii wa mijini leo ni kazi ngumu zaidi, na kuna haja ya dharura ya kuweka mpango endelevu wa utalii wa mijini na kuingiza sekta hii katika ajenda pana zaidi ya maendeleo ya miji.

Licha ya kuwa utalii unatoa mchango muhimu katika nyanja za kitamaduni na kijamii, na pia huchangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi zinazoendelea na zile zinazoinukia kiuchumi, hatupaswi kusahau kwamba safari za utalii zinachangia takribani asilimia 8 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani na hali hii inaendelea kuongezeka.

Mwaka uliopita, majanga ya asili kama vile Kimbunga Ian huko Florida na ukame uliosababishwa na joto kali barani Ulaya yameongeza changamoto za kimazingira duniani. Kulingana na uchambuzi uliofanywa na kampuni ya bima ya Munich RE ya Ujerumani, uharibifu wa kiuchumi uliosababishwa na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi ulifikia dola bilioni 270 za Marekani mwaka 2022 (sawa na euro bilioni 251.5), na kuna uwezekano mkubwa kwamba hatari na gharama hizi zitaendelea kuongezeka katika siku zijazo.

Kwa mujibu wa jarida la utalii la Marekani (Fodor’s Travel), baadhi ya maeneo maarufu ya utalii duniani yanaathiriwa kwa kiwango kikubwa na wingi wa watalii, hali ambayo imefikia hatua ya overtourism (utalii wa kupita kiasi), yaani kuzidi kwa uwezo wa kubeba wageni kwa njia endelevu. Miongoni mwa athari zake ni upungufu wa maji na uchafuzi wa mazingira. Kwa sababu hiyo, maeneo haya yanashauriwa kuepukwa angalau katika msimu wa kilele cha utalii.

Mifano Duniani
Venice – Italia
Venice inajulikana kama moja ya maeneo maarufu zaidi ya utalii duniani. Mwaka uliopita, idadi ya wageni ilizidi uwezo wa jiji, hali iliyosababisha hatari ya mafuriko. Katika majira ya joto yaliyopita, Venice ilikuwa inapokea takribani wageni 80,000 kwa siku. Hali hiyo ilisababisha Italia kuweka vikwazo kwa meli kubwa za kitalii kuingia katika Ziwa la Venice. Pia, kulikuwa na mpango wa kutoza ada ya kuingia (kati ya euro 3 hadi 10) kwa wageni wa siku moja kuanzia Januari 16, 2023, lakini utekelezaji wake uliahirishwa kwa miezi sita.

Pwani ya Amalfi – Italia
Katika majira ya kiangazi, miji ya kuvutia ya pwani ya Amalfi hujaa sana watalii kiasi cha kusababisha foleni ndefu za magari kwenye Barabara ya Amalfitana. Hali hii iliwafanya wazima moto na ambulensi kushindwa kupenya. Ili kudhibiti hali hiyo, mamlaka za mitaa zilianzisha kanuni mpya mnamo Juni 2022: magari yenye namba za usajili zinazomalizika kwa tarakimu zisizo za jozi (1,3,5,…) yanaruhusiwa kuendesha tu katika tarehe zisizo za jozi, na yale yenye tarakimu za mwisho za jozi yanaruhusiwa kuendesha katika siku za jozi.

Étretat – Normandy, Ufaransa
Mji huu mdogo wa pwani unajulikana kwa milima yake ya chokaa yenye kuvutia. Mwaka 2021, idadi ya watalii ilikuwa mara tatu ya wakazi. Hali hii ilisababisha mifumo ya maji taka kushindwa kufanya kazi kutokana na wingi wa taka, na hivyo mamlaka za mji zikachukua hatua za kupunguza idadi ya watalii hasa katika msimu wa kilele. Pia, kulikuwa na mporomoko wa ardhi mara kwa mara kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakipanda milimani.

Bali – Indonesia
Kisiwa cha Bali chenye wakazi milioni 4.5 hupokea zaidi ya watalii milioni 6 kwa mwaka. Watalii huchangia hadi 65% ya matumizi ya maji ya kisiwa, hali inayosababisha wakulima kukosa maji ya kutosha kwa kilimo. Aidha, tatizo la taka limekuwa kubwa, na mara nyingi taka hutupwa baharini au kuchomwa, jambo linalosababisha uchafuzi wa mazingira.

Maui – Hawaii
Kisiwa hiki cha kitalii kinapendwa sana lakini kwa sasa kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji. Hoteli zinatumia maji mengi zaidi kwa siku kuliko wenyeji, hali iliyosababisha serikali kuweka vikwazo vya matumizi ya maji na kuanzisha ukomo wa idadi ya watalii.

Thailand
Mnamo mwaka 2019, Thailand ilipokea watalii milioni 40. Baada ya janga la COVID-19, serikali ilitumia fursa ya kupungua kwa watalii kurekebisha maeneo ya utalii. Maya Bay kwenye Kisiwa cha Koh Phi Phi ilifungwa kabisa kuanzia Juni 2018 hadi Desemba 2021 kwa ajili ya urekebishaji. Ilipofunguliwa tena, wingi wa watalii ulisababisha uharibifu upya, hivyo ilifungwa tena Mei 2022. Sasa serikali imeanzisha mfumo wa kufunga maeneo maarufu angalau mwezi mmoja kila mwaka ili mifumo ya ikolojia ipate nafasi ya kupona.

Magharibi ya Marekani
Ukame wa muda mrefu umekumba Magharibi ya Marekani kwa zaidi ya miaka 23. Mto Colorado, uliowahi kufika Bahari ya Pasifiki, sasa unakauka kabla ya kufika baharini. Hii imesababisha kupungua kwa viwango vya maji katika mabwawa makubwa ya Mead na Powell. Wakati huo huo, maeneo kama Ziwa Tahoe yalishuhudia ongezeko kubwa la wageni wakati wa COVID-19, hali iliyosababisha uchafuzi wa hewa na maji. Ili kudhibiti hali hiyo, mamlaka zimeanzisha huduma ya basi bure kuzunguka maeneo ya kitalii ili kupunguza msongamano wa magari.

Utalii ni mojawapo ya sekta chache za kiuchumi zinazokua kwa kasi duniani kote, na huchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ajira, uboreshaji wa miundombinu, na mapato ya biashara ya nje. Hata hivyo, ni muhimu kuweka uwiano kati ya athari chanya na hasi za utalii ili kuhakikisha unalingana na mahitaji na maslahi ya wakazi.

Aidha, Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa lengo la 11 linalosema: “Kuhakikisha miji na makazi yanajumuisha wote, salama, yenye uthabiti na endelevu” linapaswa kuwa kipaumbele cha kila mmoja katika sekta ya utalii.