Siku ya Kiswahili Duniani

Imeandikwa na: Fatma Ebrahim
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili/ Mervat Sakr
Kiswahili ni lugha ya asili ya Kibantu, inayozungumzwa katika nchi za Afrika Mashariki kama Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na nchi nyingine, ikiwa na lahaja zaidi ya 16. Lugha ya Kiswahili imekuwa njia ya mawasiliano kati ya watu katika maeneo mengi ya Afrika na pia katika Mashariki ya Kati.
Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kiafrika zenye wazungumzaji zaidi ya milioni 200 na kinatambuliwa miongoni mwa lugha kumi zinazozungumzwa sana duniani. Lugha hizi zimekubaliwa kutumiwa katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na zina jukumu muhimu katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Lugha ya Kiswahili imepata umaarufu zaidi ya mipaka yake ya jadi barani Afrika na inazidi kupata umaarufu na kuungwa mkono katika nchi za Amerika, Ulaya, na Mashariki ya Mbali, ambako inafundishwa katika vyuo vikuu vingi. Pia, lugha ya Kiswahili hutumika kimataifa katika utangazaji na uchapishaji, hivyo Kiswahili ni njia muhimu ya kusambaza muundo na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Mnamo mwaka 2021, Mkutano Mkuu wa UNESCO ulitangaza Julai 7 kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Sherehe za ufunguzi wa Siku ya Kiswahili Duniani mnamo mwaka 2022 zilifanyika Makao Makuu ya UNESCO na duniani kote, chini ya kauli mbiu isemayo “Kiswahili kwa Amani na Ustawi”.
Katika Siku hii ya Kiswahili Duniani, tusherehekee urithi wa lugha na tujitolee kulinda utofauti wa lugha tunazotumia kuelezea tunu na maono yetu ya dunia katika ngazi binafsi, ili kuimarisha amani na kuwezesha ushirikiano wa kijamii.