LITTI LERTI KIDANKA – MALKIA WA NYUKI

LITTI LERTI KIDANKA – MALKIA WA NYUKI

Imeandikwa na: Gwamaka Mwamasage

Kihistoria, tunafahamu mashujaa kadhaa waliopigania uhuru dhidi ya ukoloni katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki, hususan nchini Tanzania. Pamoja na jitihada zao za kuzuia uvamizi uliolenga kupora rasilimali na kudhoofisha nguvu zao za kiutawala, simulizi za wengi wao ziliishia kwenye kushindwa kulikosalimisha himaya zao kwa wakoloni. Wengi wa mashujaa hawa walikuwa wanaume, na mbinu zao za mapambano zilikaribiana kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, alikuwepo shujaa maarufu aliyejulikana kama Litti Lerti Kidanka, mwanamke wa kabila la Wanyaturu, aliyeliongoza kabila lake katika mapambano dhidi ya utawala wa Kijerumani kati ya mwaka 1903 na 1908. Inakadiriwa kuwa amezaliwa mnamo mwaka 1860 katika kijiji cha Unyang’ombe, Sekotoure–Ilongero, mkoani Singida. Aliolewa na Nyalandu Mtinangi Njoka wa ukoo wa Lundi.
Inadaiwa wazazi wake walikuwa waganga wa tiba asilia: baba yake Kidanka Jilu Msasu, chifu wa eneo hilo, na mama yake Sitra Mughenyi. Wao walimrithisha binti yao uwezo huo wa jadi.

Harakati zake zilianza rasmi mnamo mwaka 1903, akipinga vitendo vya wakoloni waliokuwa wakikamata vijana kwa ajili ya utumwa na kupora mali za wenyeji. Upekee wa Litti ulikuwa katika mbinu yake: tofauti na wapiganaji wengine waliotumia silaha za jadi pekee, yeye alitumia nyuki kama silaha ya kipekee ya kushambulia wakoloni, jambo lililompa jina la utani “Malkia wa Nyuki”. Mapambano hayo ya miaka mitano yalijulikana kama Maasi ya Litti. Umaarufu wake ulitokana na ujasiri wa kuongoza vita kwa kutumia nyuki, akisaidiwa na mumewe Nyalandu pamoja na shemeji yake Hango Linja waliotumia mikuki na mishale.

Kwa ujasiri usio kifani, Litti mwenyewe aliongoza mapigano akitoa amri kwa washirika wake kuhusu mashambulizi na kusitisha vita. Kihistoria, aliweza kushinda mashambulizi mawili ya kwanza dhidi ya Wajerumani. Hata hivyo, katika shambulio la tatu, Wajerumani waliona haja ya kubadilisha mbinu kwani walihofia kushindwa tena. Walitumia vibaraka, hatua iliyohitimisha zama za mwanamke huyo shujaa.

Mnamo mwaka 1908, Wajerumani walimshawishi kibaraka aitwaye Igwe Yunga, aliyekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Sie Ndinda (wifi yake Litti). Kupitia hila hii, walimshawishi Sie kutoa siri ya nguvu za Litti, ambazo zilihusiana na dawa za jadi alizorithi kutoka kwa wazazi wake. Igwe alipewa jukumu la kuharibu dawa hizo kwa ahadi za malipo. Alitekeleza jukumu hilo kwa siri, akaondoa dawa zote na kutoa taarifa kwa Wajerumani.

Katika shambulio lililofuata, Litti alishindwa vibaya: kila alipowaita nyuki wake hawakumtii. Baada ya majaribio kadhaa yaliyoshindikana, alikamatwa akiwa nyumbani kwake kijijini Matumbo, kitongoji cha Mikuyu, akiwa na mumewe. Wote walipigwa risasi na kufariki papo hapo. Miili yao ilizikwa Mikuyu–Matumbo, kata ya Makuro, na makaburi yao bado yapo yakiwa yamewekewa alama za miti. Wajerumani walikata kichwa cha Litti na kukipeleka Ujerumani.

Litti aliacha watoto wanne: wavulana wawili, Sang’ida na Kidanka, na wasichana wawili, Nyamughenyi na Sitra. Wasichana walitekwa na kupelekwa Dar es Salaam baada ya wazazi wao kuuawa. Baadaye ilifahamika mmoja aliishi Zanzibar na mwingine Tabata, Dar es Salaam. Kidanka, mmoja wa wavulana, alinusurika baada ya kuruka uzio wakati wa shambulio, ingawa alipigwa risasi ubavuni. Alipona kwa tiba asilia na aliendelea na shughuli za uganga hadi alipofariki duniani mnamo mwaka 1980 kijijini Matumbo.

Kwa heshima ya kumbukumbu ya mwanamke huyu shujaa asiyesimuliwa sana katika historia, uwanja wa michezo wa Singida ulibatizwa jina la Litti Stadium.