Maendeleo ya Misri katika Sekta ya Afya: Safari ya Mageuzi kuelekea Huduma Kamili za Afya

Imeandikwa na: Maryam Muhammad Sayed Ibrahem
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika miaka ya hivi karibuni, Misri imepitia mageuzi makubwa katika sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa unaolenga kutoa huduma bora za matibabu kwa wananchi wote. Miradi mikubwa ya kitaifa ya afya, hasa mradi wa kuboresha Taasisi ya Nasser, inadokeza mabadiliko haya makubwa katika mfumo wa afya wa Misri.
Taasisi ya Nasser: Kutoka Hospitali ya Kawaida hadi Jiji la Tiba
Taasisi ya Nasser ni mojawapo ya taasisi mashuhuri za tiba nchini Misri. Kwa sasa, taasisi hiyo inapitia hatua ya maendeleo ya kina ili kuibadilisha kuwa jiji kamili la matibabu. Maboresho hayo yanajumuisha kuongeza idadi ya vitanda kutoka 600 hadi 1,300, kuanzisha kliniki 100 za wagonjwa wa nje, na vyumba 50 vya upasuaji, pamoja na kujenga majengo mapya ya kutibu saratani na kwa upasuaji maalum.
Zaidi ya hayo, kituo kikubwa zaidi cha kupandikiza viungo katika eneo la Mashariki ya Kati kinajengwa katika taasisi hiyo. Aidha, mfumo wa kidijitali umeanzishwa kwa ajili ya kuwaandikisha wahisani wa viungo baada ya kufariki, kwa ushirikiano na Wizara ya Haki.
Mikakati ya Urais: Afya ya Mwananchi ni Kipaumbele
Serikali ya Misri imeanzisha kampeni mbalimbali za kiafya chini ya uongozi wa rais, zenye lengo la kuboresha afya ya wananchi. Mojawapo ya kampeni hizo ni “Afya ya Milioni 100”, iliyolenga kutokomeza virusi vya Hepatitis C na kugundua magonjwa yasiyoambukiza. Takribani watu milioni 52 walifanyiwa uchunguzi.
Pia, kampeni ya kuondoa orodha za wagonjwa waliokuwa wakisubiri huduma ilifanikisha upasuaji kwa zaidi ya wagonjwa 413,000 waliokuwa wakihitaji matibabu ya haraka. Aidha, mpango wa kuboresha afya ya wanawake ulijikita katika uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti na magonjwa sugu.
Bima ya Afya kwa Wote: Kuelekea Huduma ya Kina kwa Kila Mtu
Misri imeanza kutekeleza mfumo wa bima ya afya kwa wote, unaolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma kamili za afya kwa raia wote. Mfumo huu umeanzishwa katika baadhi ya mikoa, na zaidi ya maamuzi milioni 2 ya matibabu yametolewa kwa gharama ya serikali. Hii inaonesha dhamira ya kweli ya serikali kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa kila mtu bila ubaguzi.
Uwekezaji katika Miundombinu ya Afya
Serikali imewekeza zaidi ya pauni bilioni 120 kuboresha miundombinu ya sekta ya afya. Uwekezaji huu umehusisha ujenzi na uboreshaji wa hospitali 40 za mfano, ukarabati wa hospitali kongwe, na usasishaji wa vifaa vya kisasa vya matibabu, hatua imeyochangia kwa kiasi kikubwa kuinua viwango vya huduma zinazotolewa.
Maendeleo haya yanadhihirisha dhamira ya kweli ya serikali ya Misri katika kuboresha mfumo wa afya na kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi wake. Uboreshaji wa Taasisi ya Nasser ni mfano halisi wa dhamira hiyo, na ni hatua kubwa kuelekea kujitegemea katika huduma za matibabu maalumu na kuimarisha nafasi ya Misri kama kitovu cha huduma za afya katika ukanda huu.