Dkt. Said Al-Battuti aandika: Utalii Endelevu na Utalii Wenye Kuwajibika

Dkt. Said Al-Battuti aandika: Utalii Endelevu na Utalii Wenye Kuwajibika

Imetafsiriwa na: Malak Azhary 

Imehaririwa na: Mervat Sakr 

Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Uendelevu ni matarajio, na utalii wenye kuwajibika ndio tunachokifanya kama wazalishaji, watumiaji, serikali, na wasimamizi wa maeneo ya utalii ili kufanikisha matarajio hayo. Mara nyingi, neno "uendelevu" hutumiwa kwa maana ya jumla tu bila utekelezaji wa kweli, ilhali linahitaji kuwajibika na kusema kwa uwazi kile kinachofanywa ili kuufanya utalii kuwa bora zaidi na kwa uwazi kuhusu mafanikio yetu.

Utalii endelevu (Sustainable Tourism) ni usimamizi wa shughuli za utalii kwa namna inayozingatia kikamilifu athari za kiuchumi, kijamii, na kimazingira, za sasa na zijazo, na kukidhi mahitaji ya wageni, sekta ya utalii, mazingira na jamii zinazoukaribisha utalii.

Utalii endelevu si aina maalum ya utalii, bali ni mchakato wa kugeuza aina zote za utalii kuwa endelevu zaidi. Ni sehemu muhimu ya maendeleo endelevu, kwa malengo yake 17 kulingana na Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 iliyopitishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2015. Malengo hayo ni:

• Kutokomeza umaskini

• Kutokomeza njaa

• Afya bora na ustawi

• Elimu bora

• Usawa wa kijinsia

• Maji safi na usafi wa mazingira

• Nishati nafuu na safi

• Kazi yenye hadhi na ukuaji wa uchumi

• Viwanda, ubunifu na miundombinu

• Kupunguza tofauti

• Miji na jamii endelevu

• Matumizi na uzalishaji wenye kuwajibika

• Hatua kuhusu mabadiliko ya tabianchi

• Maisha chini ya maji

• Maisha juu ya ardhi

• Amani, haki na taasisi imara

• Ushirikiano kwa ajili ya kutimiza malengo

Inapaswa kuwepo tofauti ya wazi kati ya dhana ya utalii wa mazingira na utalii endelevu. Utalii wa mazingira ni tawi maalum ndani ya sekta ya utalii linalozingatia ulinzi wa mazingira, wakati huo huo kanuni za uendelevu zinapaswa kutekelezwa katika shughuli zote, taratibu, taasisi na miradi ya utalii, zikiwemo aina zote za utalii wa jadi na wa mbadala.

Utalii endelevu unaelezea sera, mazoea, na programu ambazo haziangalii tu matarajio ya watalii kuhusu usimamizi wa rasilimali za asili kwa njia ya kuwajibika (upande wa mahitaji), bali pia huzingatia mahitaji ya jamii zinazosaidia au kuathiriwa na miradi ya utalii na mazingira (upande wa usambazaji). Kwa hivyo, utalii endelevu unalenga kuwa bora zaidi katika matumizi ya nishati na kuwa rafiki kwa tabianchi (kwa mfano kutumia nishati mbadala), kutumia maji kidogo, kupunguza taka, kulinda bioanuwai, urithi wa kitamaduni na maadili ya kijadi, kukuza uelewa na uvumilivu baina ya tamaduni, kuzalisha kipato cha ndani, na kushirikisha jamii katika kuboresha maisha na kupunguza umaskini.

Utalii Wenye Kuwajibika (Responsible Tourism)

ulifafanuliwa kwa mara ya kwanza kupitia Tamko la Cape Town mnamo mwaka 2002, pembeni ya Mkutano wa Dunia kuhusu Maendeleo Endelevu (WSSD), kama “kuunda maeneo bora kwa jamii za wenyeji kuishi na kwa wageni kutembelea.” Utalii wenye kuwajibika si bidhaa maalumu – bali aina zote za utalii zinaweza kuwa zenye kuwajibika zaidi au pungufu, na unahitaji wamiliki wa miradi ya utalii, waendeshaji, serikali, jamii za wenyeji, pamoja na watalii kuwajibika na kuchukua hatua ili kufanya sekta ya utalii kuwa endelevu zaidi kwa kijamii, kimazingira, na kiuchumi.

Ni vyema kutajwa kuwa utalii wa kupita kiasi (Overtourism) ni kinyume kabisa cha utalii wenye kuwajibika. Wakati utalii wenye kuwajibika unalenga kutumia utalii kuunda maeneo bora kwa wenyeji kuishi na kwa wageni kutembelea, utalii wa kupita kiasi unatokana na kushindwa kusimamia utalii kwa njia endelevu na huwa na athari mbaya kwa maisha ya wenyeji na kwa uzoefu wa wageni.

Kwa mujibu wa Tamko la Cape Town, utalii wenye kuwajibika huchukua aina mbalimbali, zikiwemo:

• Utalii unaopunguza athari mbaya za kiuchumi, kimazingira na kijamii.

• Utalii unaonufaisha jamii kwa kiwango kikubwa zaidi kiuchumi, kuboresha ustawi wa jamii zinazopokea utalii, kuboresha mazingira ya kazi, na kuwajengea uwezo wa kufanya kazi katika sekta hiyo.

• Utalii unaoshirikisha jamii katika maamuzi yanayohusu maisha na mabadiliko yao.

• Utalii unaotoa mchango chanya katika kuhifadhi urithi wa asili na utamaduni, na kulinda utofauti wa dunia.

• Utalii unaotoa uzoefu wa kuridhisha kwa watalii kupitia mwingiliano wa moja kwa moja na jamii zinazopokea utalii, hivyo kuimarisha uelewa wa masuala ya kitamaduni, kijamii, kimazingira na hata kisiasa.

• Utalii unaowezesha watu wenye ulemavu na waliotengwa kupata fursa ya kushiriki.

• Utalii unaojenga heshima kati ya wageni na jamii, kuimarisha uhusiano wa kuaminiana na ujumuishaji kati ya tamaduni mbalimbali, na kukuza maadili ya uvumilivu na amani.

Uwasilishaji wa taarifa kwa uwazi na uwezekano wa kuhakiki maendeleo kuelekea kufikia malengo ya utalii wenye kuwajibika ni jambo la msingi kwa uadilifu na uaminifu wa juhudi zetu. Hili pia linawawezesha washikadau wote kutathmini maendeleo na kuwawezesha watumiaji kufanya maamuzi sahihi.

Kwa muda wa nusu karne tumekuwa wazito na tumeshindwa kutekeleza kanuni ya tahadhari. Wengi bado wanatarajia au wanaamini kuwa suluhisho la kichawi litaibuka bila maumivu. Dunia ina rasilimali chache, na ukuaji usio na kikomo si jambo linalowezekana.

Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) liliripoti tarehe 27 Mei 2021 kuwa kuna uwezekano wa asilimia 40 kuwa joto la wastani la kila mwaka duniani linaweza kufikia nyuzi joto 1.5 juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda katika angalau moja ya miaka mitano ijayo – na uwezekano huu unaendelea kuongezeka. Kuongezeka kwa joto humaanisha kuyeyuka zaidi kwa barafu, kuongezeka kwa kina cha bahari, mawimbi makali ya joto na hali mbaya ya hewa, na athari zaidi kwa usalama wa chakula, afya, mazingira, na maendeleo endelevu.

Hatua madhubuti na za mabadiliko zinahitajika kwa haraka ili kupeleka dunia katika njia endelevu na yenye uimara. Kuna masuala matatu yanayoathiri dunia nzima na kutishia uwepo wetu kama binadamu pamoja na viumbe wote:

• Uzalishaji wa gesi chafu na mabadiliko ya tabianchi

• Kupotea kwa bioanuwai na magonjwa yanayoanzia kwa wanyama (zoonoses)

• Taka za plastiki, ambazo nyingi huingia kwenye mito na hatimaye baharini, ambako huunda mikondo ya takataka (gyros) inayooza na kuingia kwenye mnyororo wa chakula

Uzalishaji wa gesi chafu na kupotea kwa bioanuwai ni vitisho vikubwa kwa uhai wa binadamu. Wanasayansi wengi wanaonya kuwa tunakabiliwa na kutoweka kwa aina ya sita ya viumbe, kunakosababishwa na matumizi yetu kupita kiasi ya ardhi, huku plastiki ikitajwa kama alama kuu ya kihistoria ya enzi ya Anthropocene.

Tupo sasa katika muongo muhimu wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa bioanuwai athari zake zitatuathiri sote kwa kiwango sawa. Kuigeuza sekta ya utalii kuwa endelevu na rafiki kwa tabianchi ni fursa ya kipekee ya kubadilisha uhusiano wa utalii na mazingira, tabianchi na uchumi, kuhakikisha usambazaji sawa wa faida zake, na kuendeleza uchumi wa utalii wenye uimara na usio na kaboni.