Kamati ya Olimpiki ya Misri

Kamati ya Olimpiki ya Misri

Imetafsiriwa na/ Kamal Elshawadfy
Imehaririwa na kukaguliwa na/ Fatma Elsayed

Karibu mwishoni mwa karne ya kumi na tisa, wazo la kuunda vilabu lilianza kuota mizizi akilini mwa jumuiya za  kigeni nchini Misri, na hivyo wakajenga vilabu kadhaa vya michezo na kijamii. Mfumo huu ulienea katika muktadha mkubwa mwanzoni mwa karne ya ishirini katika miji ya Alexandria, Port Said, na Kairo. Miongoni mwa vilabu hivyo;  klabu ya Alsilah – klabu ya Ugiriki ya Kichezo – klabu ya El-Million ya Kigiriki kwa Gimnastiki – klabu ya Kikundi cha Wapenda baiskeli – klabu ya Muungano ya Italia ya kitaifa– klabu ya AS Roma - Klabu ya Masumbwi ya Kleopatra - Savoia ya Italia kwa Soka – klabu ya Alsilah ya Suffolk ya Kiingereza - klabu ya Alsilah ya Kimisri – klabu ya Almukhtalat ya Kiitaliano. Kisha, ilikuwa zamu ya Wamisri kuunda vilabu kadhaa huko Kairo na Alexandria, kama vile; klabu ya El-Sekka El-Hadid - Al Ahly - Sporting - El Gezira - Heliopolis - Maadi - na kadhalika. Vilabu vya jamii za wageni vilikuwa vikiongoza kwa idadi, ambapo vilabu 26 vilianzishwa, na pia vilikuwa na rasilimali kubwa na walikuwa na watu tajiri ambao walikuwa wakipata ulinzi kutoka kwa mamlaka na taasisi za kidiplomasia. Pia, miongoni mwao kulikuwa na watu wengi ambao walipata elimu yao huko Ulaya na walikuwa na uhusiano wenye  nguvu na vyama vya michezo nje ya nchi.


   uwepo kwa vilabu hivi ulihitaji uwepo wa mfumo wa kuwakusanya katika mashindano na mechi, na hivyo Chama cha Mchanganyiko cha Vilabu vya Michezo kilianzishwa huko Alexandria mwaka 1908, chini ya uongozi wa Bwana Angelo Paulanaki (raia wa Alexandria mwenye asili ya Kigiriki). Wengi wa wanachama wa klabu hii walikuwa wageni (kutokana na hali ya kisiasa ya Misri wakati huo), na lugha ya Kifaransa ilikuwa lugha ya mawasiliano katika mawasiliano yote, sheria, maamuzi, na kumbukumbu. Chama hiki kilianza kuandaa mashindano ya Misri kati ya mwaka 1908 na 1910, na pia kilishughulikia makubaliano ya kimataifa kati ya Misri na nchi nyingine kama Ufaransa, Norway, na Hungary. Aidha, vyama vingine vya michezo vilianzishwa kama vile mchezo, Kuogelea, na Baiskeli mwaka 1910.

 Angelo Paulanaki alikuwa mchezaji wa kwanza nchini Misri aliyeshiriki katika mashindano ya kimataifa ya michezo nje ya Misri. Baada ya kustaafu kwake kwa  kushiriki katika mashindano ya michezo, Angelo Paulanaki aliunda vilabu vya michezo.Kilabu ya kwanza aliyoanzisha ilikuwa kilabu ya mchezo ya Alexandria, ambayo ilijumuisha michezo yote. Mwaka 1910, klabu hii ilibadilika kuwa Chama cha mchezo cha Misri chini ya ulanguzi wa Mheshimiwa Khedive Abbas Helmi na Mheshimiwa  Mkuu Omar Tousson. Count Pierre de Coubertin, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, alimteua Angelo Paulanaki kuwa mwanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki na mwakilishi wake nchini Misri kutokana na sifa zake zinazofaa kwa jukumu hilo.
   
Baada ya uteuzi wa Bwana Paulanaki katika Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (Juni 1910), alianzisha Kamati ya Olimpiki ya Misri mnamo Juni 13, 1910, huko Alexandria chini ya uhamasishaji wa Khedive Abbas. Kamati hii ilikuwa na Mkuu Omar Tousson kama Mwenyekiti, Amin Yahya Pasha kama Katibu wa Hazina, Angelo Paulanaki kama Katibu Mkuu, na Ahmed Ziyur Pasha, Gavana wa Alexandria wakati huo, kama Mwanachama. Kamati pia ilijumuisha wawakilishi kutoka vyama vya michezo nchini Misri. Misri ilianza kushiriki katika uwanja  wa Olimpiki na kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Stockholm 1912 katika mchezo wa upanga na mchezaji mmoja tu, Ahmed Hassanein, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Oxford. Tangu mwaka 1914, kulikuwa na mwelekeo wa kusimamia vyama vya michezo ambavyo vilikuwa chini ya ulanguzi wa wageni na kuanzisha vyama vya kujitegemea vya Misri; ili kila mchezo uwe na chama chake cha Misri kinachoweza kuendesha mchezo wake bila udhibiti wa Chama cha Mchanganyiko. Mwelekeo huu uliongezeka baada ya timu ya Misri kurudi kutoka Michezo ya Olimpiki ya Antwerp mnamo 1920.

   Na baada ya Michezo ya Olimpiki huko Amsterdam mnamo mwaka 1928, vilabu vya Misri vilifanikiwa kuongezeka na kufanya kazi ya kutwaa uhuru na kujitenga na udhibiti wa Chama cha Mchanganyiko na mfumo wake. Vilabu hivyo vilikataa kujiunga na Kamati ya Olimpiki ya Misri, na hivyo Kamati hiyo ilivunjwa mwaka 1929. Mapema mwaka 1930, Misri ilipokea mwaliko wa kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya kumi huko Los Angeles kuanzia tarehe 30 Julai hadi 14 Agosti 1930 kutoka kwa kamati ya Marekani nchini Misri, ambayo iliiwasilisha kwa Wizara ya Mambo ya Nje, ambayo kwa upande wake iliiwasilisha kwa Wizara ya Elimu ya Umma kama wizara husika. Kwa kuwa Kamati ya Olimpiki ya Misri ilikuwa imevunjwa mwaka 1929, vyama vya michezo vilialikwa kukutana tarehe 18 Februari 1932 ili kujadili mwaliko huo. Baada ya kuchunguza mwaliko huo, vyama vya michezo vilikataa na kuunga mkono uamuzi wao; kwa sababu zinazohusiana na uwakilishi wa Olimpiki nchini Misri kuwa na mtu wa kigeni.

   Baada ya hapo, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki alipenda kuongeza mwanachama wa Misri pamoja na Bwana Angelo Paulanaki. Walakini, pendekezo hilo halikukubaliwa na vyama vya michezo na mashirika yasiyo ya michezo nchini Misri, na serikali ya Misri wakati huo ilichapisha Kitabu Chake Cheupe kinachokataa jambo hilo.
   Maoni ya vyama vya michezo yalitegemea msingi kuwa ushindi uliopatikana na Misri katika uwanja wa kimataifa unawapa vyama haki ya kuomba Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kupata kwa urahisi watu wa Misri wenye sifa za kushikilia nafasi hiyo. Aidha, Kifungu 7 cha Sheria ya Michezo ya Olimpiki na Kifungu 9 cha Kanuni za Jumla kinasisitiza wazi kwamba nchi hiyo haiwezi kuwakilishwa katika Michezo ya Olimpiki na watu ambao sio raia wa nchi hiyo.
   Mzozo huo ulidumu kwa miaka miwili hadi Mkutano wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki uliofanyika huko Athens mnamo tarehe 17 Mei 1934, na tangazo lilichapishwa nchini Misri tarehe 9 Mei 1934, kuhusu uanzishwaji wa mfumo wa Kamati ya Kitaifa ya Michezo ya Misri na Kamati ya Olimpiki ya Misri. Pia, tangazo lingine lilichapishwa kumteua Mohamed Tahir Pasha kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa na Jafar Wali na Sherif Sabri kama manaibu wake kwa kipindi cha miaka minne.
   Katika Mkutano wa Athens, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki iliamua kutambua mfumo wa Kamati hizo mbili, Kamati ya Kitaifa na Kamati ya Olimpiki ya Misri, na kumteua Mohamed Tahir Pasha kuwa mwanachama wa Kamati ya Olimpiki ya Misri na mwakilishi wake nchini Misri.

Jukumu la Kamati ni:
   Kukuza, kusambaza, na kulinda harakati ya Olimpiki nchini Misri kwa kuzingatia Mkataba wa Olimpiki.

Nafasi ya Kamati ni: 
-Kusambaza kanuni na maadili ya fikra ya Olimpiki nchini Misri, hasa katika uwanja wa michezo na elimu, kwa njia ya kusambaza programu za elimu ya Olimpiki katika ngazi zote, shule, vyuo, na taasisi za elimu ya michezo na afya, pamoja na kukuza uanzishwaji wa taasisi zinazohusika na elimu ya Olimpiki kama vile Akademii za Olimpiki za kibinafsi, Makumbusho ya Olimpiki, na programu nyingine zinazohusiana na harakati ya Olimpiki.
-Kuhakikisha kuzingatiwa kwa Mkataba wa Olimpiki nchini Misri.
-Kuongeza maendeleo ya michezo ya kulipwa na michezo kwa kila mtu.
-Kusaidia mafunzo ya watendaji wa michezo kwa kupanga mafunzo na kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanachangia kusambaza kanuni za msingi za fikra ya Olimpiki.
-Kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya aina yoyote ya ubaguzi wa rangi na vurugu katika uwanja wa michezo.
-Kuunga mkono na kutekeleza sheria za kimataifa za kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini.
-Kuongeza na kusaidia hatua zinazohusiana na huduma ya matibabu na afya kwa wanamichezo.

Maono na Maadili ya Kamati ya Olimpiki ya Misri
Maadili: Lengo la maadili ya Kamati ya Olimpiki ya Misri ni kuwaelimisha wanamichezo na watu kwa ujumla kwamba ujuzi na uzoefu uliopatikana kupitia maandalizi ya michezo, ushiriki katika mashindano ya michezo, kazi ya pamoja, na urafiki ni muhimu zaidi kuliko kupata medali yoyote.
Udhibiti: Tunamwamini kila mtu kuwa na haki ya kutafuta utukufu.

Mila: Tunamwamini kuwa thamani na mila zetu zilizokita mizizi ni nguvu inayotuendesha mbele na urithi ambao tunawaachia wengine.
Furaha: Tunawamini kuwa michezo inapaswa kuwa chanzo cha furaha na kicheko.
Uadilifu: Tunawamini uadilifu ndani na nje ya uwanja. Kwa hivyo; tunasaidia thamani za usawa, haki, kutofautisha au ubaguzi, na imani.
Heshima: Tunamwamini uwazi na heshima: kuheshimu wengine, kuheshimu maoni tofauti, kuheshimu majukumu mbalimbali na michango ya wengine.
Maendeleo ya Binadamu: Tunawamini kuwa michezo na shughuli zinazohusiana zinasaidia maendeleo ya kimwili, kijamii, kiakili, na kiroho ya binadamu wote, ikisababisha kuimarisha tabia chanya na kuwasaidia watu kuwa bora.
Uongozi na Uwajibikaji: Tunawamini kuwa wale wanaoshiriki katika michezo wana jukumu kwa wengine. Wanatarajiwa kuomba maadili ya harakati ya Olimpiki na ujuzi walioupata katika safari yao ya michezo; ili kuelimisha na kuhamasisha wengine.
Kuhamasisha: Tunawamini kuwa michezo inaleta hamasa na inawapa nguvu wale wanaoshiriki na kuwasaidia kufikia kilele.
Amani: Tunachofanya ni kuona michezo kama njia ya kusambaza uelewano, kuishi kwa pamoja, na umoja kati ya watu.

Chuo cha Olimpiki cha Viongozi wa Michezo
  Kituo cha Taifa cha Maandalizi ya Viongozi wa Michezo kilianzishwa kama taasisi ya kitaifa inayohusishwa na Kamati ya Olimpiki ya Misri kulingana na Amri, Na (26) ya mwaka 1987 (tarehe 18/2/1987) iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Michezo.
   Mnamo mwaka 1982, Rais wa Baraza Kuu la Vijana na Michezo alitoa Amri Na. (754) ya mwaka 1982 (tarehe 19/12/1987) kubadilisha jina la Kituo cha Taifa cha Maandalizi ya Viongozi wa Michezo kuwa Chuo cha Olimpiki cha Viongozi wa Michezo, ambalo ndilo jina linalotumiwa sasa.
   Chuo cha Olimpiki cha Viongozi wa Michezo nchini Misri ni moja ya vyuo vikuu vyenye sifa kubwa ulimwenguni na kinafanya kazi chini ya ulanguzi wa Chuo cha Olimpiki cha Kimataifa (IOA). Ni taasisi ya elimu inayotoa programu mbalimbali za masomo zinazotegemea sayansi mbalimbali za kisasa. Chuo hicho kinajaribu kutoa mazingira ya kujifunza ya nadharia na vitendo yaliyoundwa mahsusi kwa wafanyakazi katika uwanja wa michezo. Pia, kinazingatia sera ya tathmini endelevu; ili kufuatilia vipengele vipya katika jamii ya michezo ya Olimpiki au ulimwengu kwa ujumla.

 Makumbusho ya Olimpiki:


   Makumbusho ya Olimpiki (Eng. Ahmed Al-Demardash Tony) yalikuwa yameanzishwa mwaka 1960 ndani ya jengo la Uwanja wa Kimataifa wa Cairo. Mwaka 1993, yalihamishiwa kwenye jengo jipya la Kamati ya Olimpiki ya Misri na kufunguliwa tena mwaka 1994.
   Wazo la makumbusho ni kuonyesha kila kitu kinachohusiana na michezo ya Misri, zamani na za kisasa, kupitia ushiriki katika Michezo ya Olimpiki, kanda, na bara, kwa njia ya mialiko rasmi, faili za uteuzi wa mwenyeji wa michezo, medali za kumbukumbu, zawadi, vyeti, bendera, mabango, tuzo, na zawadi za kumbukumbu, nembo, na alama, pamoja na picha za wanamichezo wa Olimpiki na watu mashuhuri wa michezo ya Misri na kimataifa.
   Makumbusho ya Olimpiki ya Tony ni moja ya makumbusho muhimu ya michezo, siyo tu nchini Misri, lakini pia Mashariki ya Kati na Afrika. Makumbusho hayo ni njia muhimu ya kuhamisha wazo la Olimpiki na dhana sahihi za shughuli za michezo kutokana na kuwa na nyaraka muhimu na habari zinazohusiana na historia ya harakati ya Olimpiki ya zamani na ya kisasa, na historia ya michezo nchini Misri, na jinsi Misri ilivyokuwa na wazo la kufanya michezo ya kanda na bara (Michezo ya Afrika - Michezo ya Kiarabu - Michezo ya Bahari ya Kati).
   Bwana Juan Antonio Samaranch, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, alitoa tamko wakati wa ziara yake kwenye makumbusho kati ya tarehe 17 na 21 Mei 1983, akisema, "Kile nilichoshuhudia leo wakati wa ziara yangu kwenye Makumbusho ya Olimpiki ya Tony ni muujiza ambao unaheshimu kila Mmisri... Kamwe sijashuhudia kitu kama hicho katika maisha yangu ya michezo katika nchi yoyote kati ya nchi 109 nilizozuru ulimwenguni... Kwa kweli, Makumbusho ya Tony ni maonyesho ya kipekee ambayo yanavuka ubunifu na hayawezi kupimwa kwa pesa, na inapaswa kuwa kati ya urithi wa kihistoria wa Misri na kualikwa kuwatembelea wageni wakuu pamoja na eneo la Piramidi.
   Wakati wa ziara ya Bwana Jacques Rogge, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kwenye makao makuu ya Kamati ya Olimpiki ya Misri mwaka 2007, alionyesha sana kuvutiwa na makumbusho na aliweka saini kwenye kitabu cha wageni na kuandika, "Ninasajili kupendezwa kwangu sana na makumbusho haya mazuri na kuwa ni mfano kwa kamati zote za Olimpiki ulimwenguni."
Makumbusho huchukua sehemu kadhaa, ambazo ni:
Sehemu ya Historia ya Misri ya Kale na Michezo
   Sehemu hii inaonyesha michoro na michora ya Farao iliyopo kwenye kuta za mahekalu na makaburi, ambayo inaonyesha kwamba Wamisri wa zamani walikuwa na hamu ya michezo na waliishiriki kwa maelfu ya miaka, kama vile mieleka, ngumi, kunyanyua vitu vizito, gimnastiki, upinde na mishale, mchezo wa upanga, farasi, na mbio.
Sehemu ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki
   Sehemu hii inaonyesha picha za marais mbalimbali wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki tangu mwaka 1896, vikao vya kila mwaka vya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, pamoja na alama, kadi, vipini, medali, na vitu vingine vya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki na Makumbusho ya Olimpiki.

Sehemu ya Kamati ya Olimpiki ya Misri
   Sehemu hii inaonyesha historia ya Kamati ya Olimpiki ya Misri kupitia mikutano ya Bodi ya Kamati ya Olimpiki ya Misri tangu mwaka 1910, kwa lugha za Kiarabu na Kifaransa, pamoja na zawadi na vitu vilivyotolewa kwa Kamati ya Olimpiki ya Misri wakati wa sherehe na michezo, pamoja na Ukuta wa Heshima kwa wanamichezo wa Misri waliopata medali za Olimpiki tangu mwaka 1928.
Sehemu ya Michezo ya Olimpiki.
   Sehemu hii inaonyesha vitu vya kumbukumbu kutoka kwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto na Majira ya baridi, kama vile mwaliko rasmi, medali za kumbukumbu, bendera, vipini, kadi, ripoti, na vitu vingine vinavyohusiana na kila michezo tangu Michezo ya Olimpiki ya kwanza mwaka 1896 huko Athens.
Sehemu ya Michezo ya Bahari ya Mediterraneani
   Misri ilikuwa na wazo la kuanzisha Michezo ya Bahari ya Mediterraneani tangu tamasha la kwanza lililofanyika Alexandria mwaka 1951. Sehemu hii inaonyesha vitu vya kumbukumbu kutoka kwa kila tamasha, kama vile mwaliko rasmi, medali za kumbukumbu, vipini, ngao, nk.
Sehemu ya Michezo ya Afrika
   Misri ilikuwa na wazo la kuanzisha Michezo ya Afrika wakati ilijenga Uwanja wa Alexandria;  kwa ajili ya tamasha la kwanza la Michezo ya Afrika. Sehemu hii inaonyesha vitu vya kumbukumbu kutoka kwa tamasha hizo za Afrika tangu tamasha la Brazzaville mwaka 1965.
Sehemu ya Michezo ya Arabuni
   Misri ilikuwa na wazo la kuanzisha Michezo ya Arabuni wakati Bwana Abdel Rahman Azzam, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, alitoa memo ya kuandaa Michezo ya Arabuni. Sehemu hii inaonyesha mali na vitu vya kumbukumbu kutoka kwa Michezo ya Arabuni kama mwaliko rasmi, medali, ngao kutoka michezo ya kwanza iliyofanyika Alexandria mwaka 1953.

Sehemu ya Wanachama wa Kamati ya
Olimpiki ya Kimataifa nchini Misri na Watu wengine wa Misri
   Sehemu hii inaonyesha picha na vitu vya kumbukumbu vya wanachama wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa nchini Misri na watu wengine wa Misri ambao wamechangia katika historia ya michezo ya Misri.

 Maktaba:


   Maktaba ya Kamati ya Olimpiki ya Misri ina mkusanyiko tajiri wa vitabu na majarida ambayo ni vyanzo muhimu vya habari kuhusu Michezo ya Olimpiki na mashindano ya bara tangu kuanzishwa kwake hadi sasa. Pia, maktaba ina ripoti rasmi za matokeo, maandalizi, na machapisho ya michezo maalum ya mashindano haya. Aidha, maktaba ina toleo mbalimbali za Kamati ya Olimpiki ya Misri, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, vyama vya michezo vya kimataifa na vya ndani, nk.
   Maktaba pia ina nyaraka za sekondari kama vile vyanzo vya marejeo, Ensaiklopidia, kamusi, vitabu vya ukweli, Ensaiklopidia za michezo na tamaduni za Olimpiki, na zinginezo.
   Maktaba inatoa uzoefu wake na huduma kwa wote wanaotembelea ikiwa ni pamoja na wanafunzi, watafiti, na wachunguzi bila malipo, na kusaidia kukuza utafiti wa kisayansi na kuongeza ufahamu wa  kitamaduni, michezo, na Olimpiki kwa ujumla kati ya watu.

Vyanzo:
Tovuti ya Kamati ya Olimpiki.

Mratibu wa lugha ya kiswahili/ Tasneem Hamdy