Juhudi za Maendeleo ya Misri katika Sekta ya Uchumi

Imeandikwa na: Saga Ashraf
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Misri imepitia mabadiliko makubwa yaliyoiweka katika njia ya maendeleo endelevu, licha ya changamoto za kimataifa zilizozikumba nchi nyingi duniani. Hata hivyo, Misri imetekeleza mageuzi katika sekta mbalimbali: kiafya, kisiasa, na hasa kiuchumi. Mageuzi haya yamesaidia kufanya marekebisho mapya ya uchumi wa nchi hiyo. Sasa, tuangalie mafanikio makuu ya Misri katika sekta ya uchumi:
Uboreshaji wa Miundombinu na Uvutaji wa Uwekezaji
Misri, chini ya uongozi wa Rais Abdel Fattah El-Sisi, imefanikiwa kuimarisha miundombinu, kutoa fursa za uwekezaji zilizo tayari pamoja na leseni kamili, na pia kutoa ardhi kwa bei za ushindani sambamba na motisha za kikodi. Hatua hizi zimevutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) uliogharimu dola bilioni 10 mwaka 2023, huku ikitarajiwa kuzidi dola bilioni 40 kufikia mwisho wa mwaka 2024 kutokana na mikataba ya miradi ya Ras El Hekma na miradi ya hidrojeni ya kijani.
Marekebisho ya Kiuchumi na Mfumo Bora wa Kazi
Serikali imejikita katika kuboresha uchumi wa kisasa kwa kuimarisha sekta binafsi na kusimamia kwa ufanisi mali za serikali, sambamba na kuendeleza uchumi wa kijani na kuwawezesha vijana pamoja na wanawake. Mageuzi haya yamejumuisha kurahisisha uanzishaji wa kampuni, kupunguza mzigo wa kodi, na kutoa "Leseni ya Dhahabu" kwa wawekezaji wakuu.
Kuwezesha Taratibu na Kupunguza Urasimu wa Serikali
Serikali imechukua hatua madhubuti kama vile kupunguza muda wa uidhinishaji hadi siku 10, na kuanzisha mfumo wa kielektroniki kurahisisha taratibu za kuanzisha na kuendesha biashara. Aidha, mageuzi ya kisheria yamefanyika ili kuwawezesha wawekezaji wa kigeni kumiliki ardhi na mali isiyohamishika.
Kuimarisha Uwazi na Usawa wa Ushindani
Mageuzi haya yamejumuisha kuanzishwa kwa kitengo maalum cha kufuatilia kampuni za sekta ya umma na kuhakikisha usawa kwa wawekezaji wote. Serikali imezuia mashirika kuweka gharama za ziada bila idhini ya taasisi kuu za uwekezaji.
Motisha za Kisekta
Serikali imetoa motisha kwa sekta muhimu kama vile kilimo, viwanda, na nishati mbadala (hususan hidrojeni ya kijani). Aidha, imeunganisha mikakati ya bei na uwazi wa ada za forodha, na kuunga mkono kampuni changa zinazoanzishwa na vijana.
Utendaji wa Uwekezaji wa Moja kwa Moja kutoka Nje
Mtiririko wa uwekezaji wa kigeni uliathiriwa na mizozo ya kimataifa, ambapo ulipungua hadi dola bilioni 5.2 mwaka 2020/2021. Hata hivyo, uliongezeka hadi kufikia dola bilioni 10 mwaka 2022/2023, na matarajio ni kuona ongezeko kubwa lisilowahi kushuhudiwa – hadi dola bilioni 40 – kufikia mwishoni mwa mwaka 2024 kutokana na mikataba mikubwa ya kimkakati.
Misri inaonesha mfano wa kipekee kwa nchi zinazoendelea, ikifanikiwa kufikia maendeleo ya kiuchumi ya kipekee, hasa katika kipindi kigumu cha changamoto za kimataifa zilizoathiri hata mataifa makubwa kiuchumi.