Kulinda Amani na Usalama wa Kimataifa

Kulinda Amani na Usalama wa Kimataifa

Imeandikwa na: Arin Adel Abu Shuqair - Jordan
Imetafsiriwa na: Muhammad Ehab
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Kulinda amani na usalama wa kimataifa ni mojawapo ya malengo ya mataifa yote duniani, kwani ghasia na migogoro hudhoofisha maendeleo endelevu... Ukiukaji wa haki za binadamu ni miongoni mwa sababu kuu za migogoro na hali ya kutoaminiana, jambo ambalo hupelekea ukiukaji zaidi wa haki za binadamu.

Kwa hivyo, mchakato wa kulinda na kuimarisha haki za binadamu ni nyenzo ya kinga, huku mbinu za kuleta amani na usalama zinazotegemea haki za binadamu zikisaidia kufanikisha amani ya kudumu. Vilevile, mfumo wa haki za binadamu hutoa msingi thabiti wa kushughulikia masuala muhimu ndani ya nchi au kati ya mataifa, yanayoweza kusababisha migogoro iwapo hayatashughulikiwa ipasavyo.

Ingawa taarifa na uchambuzi wa haki za binadamu ni nyenzo muhimu za tahadhari ya mapema na hatua za awali za kukabiliana na changamoto, bado hazijatumika ipasavyo.

Kwa kuzingatia hali ya sasa ya ulimwengu, kuna changamoto kadhaa zinazojitokeza, ikiwemo: Kutotekeleza viwango vya kimataifa vya haki za binadamu na kushindwa kuzilinda kunadhoofisha juhudi za kulinda amani, kujenga amani, na kusuluhisha migogoro. Aidha, juhudi za kimataifa za kupambana na ugaidi na kuzuia kuenea kwa msimamo mkali wa vurugu zinakumbwa na changamoto kutokana na kutofuata viwango hivi vya haki za binadamu.

Kudumisha na kulinda amani ni jambo la msingi

• Kusaidia kufanikisha amani na maendeleo endelevu kwa kutekeleza viwango vya haki za binadamu, jambo linalosaidia kushughulikia dhuluma, kupunguza ukosefu wa usawa, na kujenga uimara wa jamii.
• Ni lazima tushughulikie vitisho vya kiusalama vinavyotokana na teknolojia ya kisasa.
• Pande zinazohusika katika migogoro na wadau wa mchakato wa amani wanapaswa kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu ili kulinda raia ipasavyo.
• Kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu unaotokea wakati wa migogoro ya silaha, ikiwa ni pamoja na madhara kwa raia na matukio ya ukatili wa kijinsia.
• Kuwasilisha ukweli na ushahidi kwa pande zinazohusika na kwa umma kwa ujumla, pamoja na kuhamasisha mabadiliko ya sera, tabia na mienendo.
• Kutoa mafunzo na ushauri wa kiufundi ili kuhakikisha kuwa sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu zinajumuishwa katika operesheni za kijeshi na za amani.
• Kuunda ushirikiano wa kimkakati na pande zinazohusika katika migogoro ili kupunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinajumuishwa katika maamuzi na makubaliano ya amani.
• Kuwezesha ushiriki wa makundi mbalimbali, wakiwemo wanawake, katika mazungumzo ya amani.
• Kushirikiana kati ya mataifa na kuongeza idadi ya ujumbe wa amani ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinajumuishwa katika shughuli zao.
• Kuzingatia sheria za kimataifa katika juhudi za kupambana na ugaidi na kuzuia msimamo mkali wa vurugu.
• Kukusanya ushahidi, kufanya utafiti wa kina, na kuimarisha ufuatiliaji na ripoti kuhusu jinsi ukiukwaji wa haki za binadamu unavyochangia kuenea kwa msimamo mkali na ugaidi, na jinsi ulinzi wa haki za binadamu unavyosaidia kuzuia hali hiyo.
• Kujenga uwezo na kuwahimiza viongozi wa serikali na wadau wengine kuheshimu sheria za kimataifa katika juhudi za kupambana na ugaidi na kuzuia misimamo mikali, huku wakihakikisha uwajibikaji na haki kwa waathiriwa wa ukiukwaji wa haki.
• Kujumuisha ulinzi wa haki za binadamu katika mikakati ya kuzuia na kukabiliana na migogoro.
• Kushirikiana kwa karibu na mashirika ya kimataifa na nchi wanachama ili kuonyesha mchango wa haki za binadamu katika kuzuia migogoro, kuishughulikia, na kujenga amani baada ya migogoro, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mikakati husika.
• Kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu hatua muhimu za kuhakikisha ulinzi madhubuti wa haki za binadamu.
• Kutoa mafunzo na mwongozo wa kiufundi kuhusu jinsi ya kuingiza haki za binadamu katika juhudi za kuzuia migogoro na kujenga amani.
• Kuhakikisha haki kwa waathiriwa wa ukiukwaji wa haki ili kusaidia kuzuia machafuko na migogoro mipya.
• Kujumuisha taarifa na uchambuzi wa haki za binadamu katika mifumo ya tahadhari ya mapema, na kushawishi michakato na mikakati ya maamuzi ya kitaifa na kimataifa ili kuzuia, kupunguza au kukabiliana na migogoro mipya, ikiwa ni pamoja na majanga ya kibinadamu na migogoro ya silaha.


Hatupaswi kusahau kwamba mojawapo ya vipengele muhimu vya usalama wa kimataifa, ambacho hatutakipuuza katika mkutano huu muhimu, ni usalama wa tabianchi na usalama wa chakula. Changamoto ya kulisha idadi inayoongezeka ya watu bila kumaliza rasilimali zilizopo inaendelea kuongezeka, huku zaidi ya watu milioni 800 wakikabiliwa na njaa na watu bilioni 2.4 wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa upatikanaji wa chakula cha kutosha.

Hivyo basi, masuala ya mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula hayahusiani na Jordan pekee, bali tumeona mifumo sawa katika nchi nyingine za Kiarabu na za kigeni. Tunahitaji kutafuta suluhisho maalumu kwa changamoto za usalama wa tabianchi na chakula, suluhisho ambazo zinakidhi mahitaji ya jamii za ndani na za kimataifa kwa kutumia mbinu jumuishi ya utekelezaji. Mbinu hii inapaswa kujumuisha dunia nzima na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa nje ya mipaka ya kitaifa, pamoja na ndani kupitia ubia kati ya serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kiraia kwa kushirikiana na taasisi za maendeleo za kimataifa.