Misri yaongoza mkutano wa tatu wa Baraza la Utawala wa Mpango wa Daraja la Biashara kati ya Nchi za Kiarabu na Kiafrika

Misri yaongoza mkutano wa tatu wa Baraza la Utawala wa Mpango wa Daraja la Biashara kati ya Nchi za Kiarabu na Kiafrika

Imetafsiriwa na: Hagar Elsopky 
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Jamhuri ya Kiarabu ya Misri leo imeongoza mkutano wa tatu wa Baraza la Utawala wa Mpango wa Daraja la Biashara kati ya Nchi za Kiarabu na Kiafrika uliofanyika jijini Kairo, ikiwakilishwa na Dkt. Hala El-Saeed, Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kiuchumi na Gavana wa Misri katika Kundi la Benki ya Maendeleo ya Kiislamu. Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mhandisi Hani Sonbol, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kiislamu la Ufadhili wa Biashara na Katibu Mkuu wa Mpango wa Daraja la Biashara, pamoja na mawaziri kutoka Misri na nchi nyingine za Kiarabu na Afrika, mabalozi kadhaa, wakuu wa taasisi za fedha, wabunge kutoka mabunge ya wawakilishi na ya seneti, na wawakilishi wa sekta binafsi.
  
Dkt. Hala El-Saeed alisisitiza katika hotuba yake ya ufunguzi kuwa mkutano huu ni fursa muhimu ya mashauriano, kubadilishana mawazo, mitazamo na uzoefu uliofanikiwa katika kuimarisha juhudi za serikali kukuza biashara kati ya nchi za Afrika na Kiarabu. Alieleza kuwa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri inajivunia ushirikiano wake wa muda mrefu na wenye mafanikio na Shirika la Kimataifa la Kiislamu la Ufadhili wa Biashara, mojawapo ya mashirika yenye shughuli nyingi zaidi katika Kundi la Benki ya Maendeleo ya Kiislamu. Aliongeza kuwa ushirikiano huo umezaa matunda hadi sasa kwa kuundwa kwa mfuko wa ufadhili kati ya Misri na shirika hilo wenye thamani ya jumla ya dola bilioni 13.8.

Dkt. Hala El-Saeed alisisitiza kuwa pande zote mbili zina nia ya dhati ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano huu katika kipindi kijacho, hasa kwa kuzingatia programu za kipekee zinazotekelezwa na shirika hilo, likiwemo kwa namna ya pekee Mpango wa Daraja la Biashara kati ya Nchi za Kiarabu na Kiafrika. Alieleza kuwa mkutano wa tatu wa Baraza la Utawala wa mpango huu umeanzishwa jijini Kairo, ambapo Jamhuri ya Kiarabu ya Misri inaongoza hadi kufanyika kwa mkutano unaofuata mwishoni mwa mwaka huu. Alieleza pia mapokezi ya dhati ya Misri kwa mkutano huu muhimu na shughuli zake sambamba, huku akisisitiza fahari ya Misri kwa utambulisho wake wa kipekee unaochanganya urithi wa Kiarabu na Kiafrika.

Aidha, Dkt. El-Saeed alieleza kujivunia kwake jukumu la kuongoza Baraza la Utawala wa mpango huu muhimu, unaolenga kuhamasisha na kukuza mtiririko wa biashara na uwekezaji kati ya nchi za Kiarabu na Kiafrika, kuendeleza sekta ya biashara, kuimarisha uwezo wa wauzaji wa sasa na kuibua kizazi kipya cha wauzaji, hasa katika nchi wanachama washirika wa mpango huu. Vilevile, mpango huu unalenga kubuni bidhaa mpya za kuuza nje katika masoko ya sasa na kufungua masoko mapya barani Afrika, kupitia kuanzisha ushirikiano mpya kati ya kanda ya Kiarabu na ya Afrika, pamoja na kuongeza manufaa yatokanayo na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika uwanja huu.

Dkt. Hala El-Saeed aliendelea kueleza kuwa malengo haya yanaendana na mwelekeo wa serikali ya Misri wa kupitisha mkakati jumuishi wa kuimarisha mahusiano na nchi za Afrika, hasa katika nyanja za kiuchumi na kibiashara. Hili linahusisha kufanikisha mtangamano na mtandao wa kiuchumi na nchi za Afrika kupitia kuimarisha muunganiko wa kikanda, kuendeleza njia za biashara na usafiri—wa baharini, barabara, na anga—pamoja na njia nyinginezo za kuongeza viwango vya biashara na ushirikiano wa kiuchumi, ambavyo kwa sasa havilingani na matarajio na uwezo wa mataifa ya bara la Afrika, bara lenye soko kubwa linalojumuisha takribani watu bilioni 1.3.

Aliongeza kuwa Afrika ina utajiri mkubwa wa rasilimali za asili na watu, sambamba na utambulisho wa kiutamaduni, mahusiano ya kisiasa, na historia ya pamoja ya harakati za ukombozi ambazo zinaunganisha Misri na mataifa mengine ya Afrika, katika muktadha wa maslahi ya pamoja ya kimkakati na hatima ya pamoja ya watu wa bara hili.

Dkt. El-Saeed pia alisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri imekuwa ikijitahidi, katika historia yake yote, kusaini mikataba mingi ya biashara ya pande mbili na nchi mbalimbali za Afrika, pamoja na mikataba ya pande nyingi ambayo imejiunga nayo kupitia miungano ya kiuchumi ya kikanda. Aliongeza kuwa Misri inatilia mkazo mkubwa ushirikiano wa Kusini-Kusini kupitia Wakala wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Misri, sambamba na ushirikiano wa pande tatu wenye mafanikio na washirika wa maendeleo wa kimataifa, hasa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu, ambayo ni taasisi ya maendeleo ya kikanda ya pande nyingi inayoongoza katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi wanachama wa Kiislamu barani Afrika na Kiarabu.

Dkt. Hala El-Saeed aliongeza kuwa katika muktadha wa nia ya Misri kuimarisha juhudi za ushirikiano na mtangamano wa kikanda, Misri iliwakaribisha wajumbe wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) mnamo mwaka 2022 katika mji wa Sharm El-Sheikh. Alifafanua kuwa Misri ililenga kufanya mkutano huo kuwa jukwaa kwa nchi zinazoendelea kuwasilisha mahitaji yao, hasa upatikanaji wa fedha za moja kwa moja, uhamishaji wa teknolojia yenye utoaji mdogo wa kaboni, na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa kitaifa katika serikali na sekta binafsi, pamoja na kusaidia katika maandalizi ya tafiti za uwezekano wa miradi ya maendeleo endelevu kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Pia, Dkt. El-Saeed alieleza kuhusu uzinduzi wa Misri wa “Kituo cha Ushirikiano wa Kiwanda kwa Nchi za Kusini,” ambacho kinachochea uhamishaji wa teknolojia na kukuza maendeleo ya viwanda yanayozingatia ubunifu kati ya nchi za Afrika. Hii inaonesha nafasi ya Misri kama mdhamini mkuu wa ushirikiano kati ya nchi za Kusini katika nyanja za teknolojia ya habari na mawasiliano, pamoja na dhamira yake ya kushiriki uzoefu wake mkubwa katika kutumia sekta hii kuendeleza jamii na kuboresha sekta za kilimo, elimu, afya, na maendeleo ya biashara ndogo, za kati na ndogo sana.

Vilevile, Dkt. El-Saeed alitaja kuwa Misri ilihifadhi mkutano wa wataalam wa Mfumo wa Afrika wa Mapitio ya Kila Mmoja (APRM) mnamo mwezi Januari 2020 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Kusini barani Afrika. Mkutano huo unalenga kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2030 ya Umoja wa Mataifa na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika. Hili linaonesha hatua thabiti za Misri katika kutekeleza Ajenda ya Afrika ya 2063 kuhusu maendeleo endelevu. Aliongeza kuwa Misri ilishiriki, pamoja na nchi nyingine 38 za Afrika, katika maandalizi ya ripoti yake ya mwaka 2021 kuhusu utekelezaji wa Ajenda ya Afrika, inayochangia maandalizi ya ripoti ya bara kuhusu utekelezaji wa Ajenda 2063, inayozinduliwa kila Februari katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika. Aidha, Misri inashiriki katika Jukwaa la Afrika la Maendeleo Endelevu, linaloandaliwa na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kiuchumi kwa Afrika.

Dkt. Hala El-Saeed pia alieleza kuwa Misri ilikaribisha kongamano la pili la Biashara kati ya Nchi za Kiarabu na Afrika, lililoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Kiarabu barani Afrika (BADEA) kwa kushirikiana na Mpango wa Daraja la Biashara kati ya Nchi za Kiarabu na Kiafrika mnamo mwezi Novemba iliyopita. Kongamano hilo liliangazia nafasi kubwa ya mpango huo katika kukabiliana na changamoto zilizotokana na janga la virusi vya Korona.

Dkt. El-Saeed alisisitiza kuwa kuimarisha ushirikiano kati ya Misri na nchi za Afrika ni mojawapo ya vipaumbele vinavyopewa kipaumbele na Wizara ya Mipango na Maendeleo Endelevu, kupitia miradi mbalimbali inayosimamiwa na wizara, iwe ni katika kukuza biashara kati ya Misri na nchi za Afrika, kuongeza kiwango na ukubwa wa biashara ya pande mbili, au katika nyanja za maendeleo endelevu na mada zake mbalimbali, pamoja na ushirikiano katika ujenzi wa uwezo na kuandaa wataalamu wa Kiafrika.

Alibainisha kuwa wizara hiyo imeongeza jitihada zake kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kuanzisha jukwaa la maarifa linalowezesha kubadilishana uzoefu, masomo yaliyopatikana na mbinu bora katika kuunda fursa za ajira, kujenga uwezo wa ustahimilivu, kupanua wigo wa ulinzi wa kijamii, na kufanikisha usalama wa chakula. Alifafanua kuwa jukwaa hilo pia linatoa msaada wa kiufundi katika maandalizi ya ripoti za mapitio ya kitaifa ya hiari, na kuchangia katika kuunda ajira barani Afrika kupitia utekelezaji wa “Mpango wa Milioni Moja ya Ajira,” unaolenga kuzalisha ajira milioni moja mpya barani Afrika.

Dkt. El-Saeed aliongeza kuwa wizara inatekeleza mipango kadhaa kupitia Taasisi ya Kitaifa ya Utawala na Maendeleo Endelevu—taasisi ya mafunzo ya wizara—katika muktadha wa kuimarisha sera ya serikali ya kukuza ushirikiano wa mafunzo na ujenzi wa uwezo na nchi za Afrika. Alitaja miongoni mwa programu hizo kuwa ni "Mpango wa Uongozi kwa Wanawake Waafrika." Pia alieleza kuwa taasisi hiyo, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri na Mtandao wa Mafunzo wa Taasisi za Usimamizi Afrika (TNMIA), ilizindua toleo la pili la programu hiyo mnamo mwaka 2021. Alibainisha kuwa leo hii, toleo la tatu la Mpango wa Viongozi Wanawake Afrika linazinduliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri na washirika mbalimbali, likiwajumuisha wanawake 140 kutoka nchi 45 za Afrika, na wazungumzaji kutoka taasisi nyingi za kimataifa, likiwemo shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD).

Dkt. Hala El-Saeed pia alizungumzia kuhusu programu ya mafunzo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kitaifa ya Utawala na Maendeleo Endelevu kwa kushirikiana na Chama cha Wauzaji Bidhaa Nje wa Misri mnamo mwezi Novemba iliyopita, kama sehemu ya Mpango wa Daraja la Biashara kati ya Nchi za Kiarabu na Kiafrika. Mafunzo hayo yalikuwa chini ya anuani ya "Kuimarisha Uelewa wa Biashara ya Kimataifa kwa Wajasiriamali," na yalilenga kuongeza uelewa wa wajasiriamali 28 wa Misri kuhusu taratibu za forodha zinazohusiana na uagizaji na usafirishaji bidhaa nje ya nchi, sambamba na kuangazia mikataba muhimu ya biashara ya kikanda na kimataifa, na kuchunguza fursa za kukuza biashara ya kimataifa kati ya Misri na nchi mbalimbali duniani.

Alibainisha kuwa kikao cha leo kinashuhudia utoaji wa vyeti vya mafunzo kwa wawakilishi wa washiriki wa programu hiyo.

Katika hitimisho la hotuba yake, Dkt. El-Saeed alisisitiza kuwa Misri inawakaribisha kwa moyo mkunjufu ndugu zake kutoka nchi za Kiarabu na Afrika, sambamba na kuunga mkono mazungumzo ya dhati ya kubadilishana uzoefu na mafanikio, na kutafuta suluhisho zinazosaidia kuimarisha biashara baina ya nchi hizo, pamoja na kuunga mkono juhudi za mataifa kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu.

Aliongeza kuwa mkutano huu unatoa jukwaa la kujadili na kutoa maoni kuhusu mwelekeo wa kimkakati wa siku zijazo wa mpango huu, na mbinu za kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda ili kuongeza mtiririko wa biashara na uwekezaji kati ya nchi za Kiarabu na Afrika. Pia unatoa mapendekezo ya kuongeza ufanisi zaidi katika kusukuma mbele mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo, hasa kwa kuzingatia kuanza kutekelezwa kwa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika tangu mwanzo wa mwaka 2021.