Umoja wa Mataifa wazindua mradi wa kuzisaidia nchi 8 za Afrika kuwezesha eneo huru la biashara barani Afrika

Imetafsiriwa na: Menna Ahmed Sallam
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA) na Shirika la Kimataifa la Fedha za Biashara ya Kiislamu (ITFC) wamezindua mradi mpya wa kusaidia nchi nane za Afrika katika uendeshaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Mradi huo utasaidia utekelezaji wa shughuli zaidi ya 30 katika mikakati ya nchi nane za eneo huru la biashara - Tunisia, Burkina Faso, Côte d'Ivoire, Guinea, Mauritania, Niger, Senegal na Togo, kulingana na taarifa iliyotolewa na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika.
Kwa kusaidia kutekeleza shughuli za kipaumbele zilizoandaliwa na Tume ya Uchumi kwa Afrika (ECA), mradi huo utachangia kujenga mazingira ya kufanya biashara iwe bora zaidi na jumuishi katika nchi nane za walengwa, kulingana na waandishi.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Uchumi kwa Afrika Vera Songwe alisema mradi huo mpya una uwezo wa kuongeza viwango vya biashara vya kikanda kutoka asilimia 18 hadi asilimia 25 ndani ya muongo mmoja.
Utekelezaji bora wa mradi huo unaweza kusababisha kupunguzwa kwa dola bilioni 10 kwa uagizaji kutoka nje ya bara, wakati wa kuongeza mauzo ya kilimo na viwanda kwa dola bilioni 45, au asilimia 7, na dola bilioni 21, au asilimia 5 kila mwaka, kwa mtiririko huo.
Hani Salem Sonbol, Mkurugenzi Mtendaji wa ITFC, alisema: "Tunatambua umuhimu wa kuwezesha biashara kupitia hatua za kifedha na maendeleo ya biashara. Tangu 2008, Foundation imetoa karibu dola bilioni 61, ikiwa ni pamoja na dola bilioni 30 kwa Afrika.
Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) linalenga kuunda mfumo wa pamoja na kuweka viwango kote barani ili kuhakikisha ushirikiano wa biashara, uratibu na ufanisi.