Msaada wa Ulaya kwa kufadhili miradi ya maendeleo nchini Tanzania
Imetafsiriwa na: Tarek Said
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa nchi yao imepokea msaada wa Euro milioni 425 kutoka Tume ya Ulaya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Msemaji wa Rais wa Tanzania, Zahra Yunus, amesema msaada huo utatumika kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo nchini katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amefichua msaada huo wakati wa kilele chake na Rais wa Tanzania, Samia Hassan pembezoni mwa kikao cha sita cha Kilele cha Ulaya na Afrika kilichofanyika Brussels, akibainisha kuwa Tanzania inatarajia kutumia Euro milioni 180 za fedha hizo, katika miradi mikubwa mitatu nchini ikiwemo mradi wa kuendeleza mifumo ya kidijitali.
Serikali ya kitaifa pia imepanga kutangaza mradi mpya wa kitaifa wa kukuza ustawi wa Watanzania, usawa wa kijinsia na uanzishwaji wa miji ya kijani katika miji ya Tanga, Mwanza na Pemba.
Katika Kilele cha Ulaya na Afrika, Rais wa Tanzania, Samia Hassan aliahidi kuendelea kushirikiana na Tume ya Ulaya kutambua maeneo ya kipaumbele ya ziada kupitia mashauriano ya baadaye baina ya nchi, ili msaada huo ulete maendeleo endelevu kwa Watanzania.