Misri na Washirika wa Maendeleo: Mfano wa Maendeleo wa Kipekee

Misri na Washirika wa Maendeleo: Mfano wa Maendeleo wa Kipekee

Imetafsiriwa na: Ahmed El-Sayed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Katika ushirikiano wa kimkakati mpya uliozinduliwa na Misri kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2023–2027, inathibitishwa kwamba mfano wa maendeleo wa Misri ni mfano kamili wa pande zote, unaochanganya ngazi za ndani na za kimataifa. Serikali ya Misri inaamini kuwa mafanikio ya maendeleo yanategemea ujenzi wa ushirikiano na maelewano.

Ngazi ya Kitaifa:
Maono ya maendeleo ya Misri yanatokana na ushirikiano kati ya sekta za serikali, sekta binafsi, na taasisi za jamii ya kiraia. Ushirikiano huu unahusisha sekta ya umma, sekta ya kibinafsi, na mashirika ya kiraia yenye maslahi na malengo tofauti, ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanayofaa kila sehemu ya jamii.

Ngazi ya Kimataifa:
Misri ina mahusiano ya muda mrefu na washirika wa maendeleo, wakiwemo Umoja wa Mataifa na mashirika yake ya kitaalamu. Misri ilikuwa miongoni mwa nchi waanzilishi wa Umoja wa Mataifa katikati ya karne ya 20, na hivyo kuunda msingi wa ushirikiano wa kimkakati unaoendeleza maendeleo ya ndani na nje. Mfumo huu unahimiza mwendelezo wa mifumo ya ushirikiano iliyojengeka kati ya Misri na washirika wake wa maendeleo, kwa lengo la kufikia malengo na vipaumbele vya kitaifa.

Mfano wa Maendeleo wa Ushirikiano:
Mfano wa maendeleo wa Misri unajitokeza kama mfano wa ushirikiano, ambapo serikali imefaulu kushughulikia changamoto nyingi za maendeleo kupitia ujenzi wa ushirikiano wa kitaifa na kimataifa. Ushirikiano huu unategemea uzoefu uliopatikana kutoka kwa washirika mbalimbali katika sekta tofauti. Mfumo huu wa kimkakati unajumuisha mhimili mitano ya msingi:
• Maendeleo ya kiuchumi ya pande zote
• Haki ya kijamii
• Uendelevu wa rasilimali za mazingira na asili
• Utawala bora
• Uwezeshaji wa wanawake na wasichana
Hizi mhimili zinajumuika vizuri na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na malengo yake kumi na saba, na pia zinalingana na maono ya kitaifa ya maendeleo endelevu ya 2030, pamoja na mikakati ya kitaifa iliyoanzishwa kwa ushirikiano na mashirika na programu za Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Maono ya Kitaifa ya Rais Abdel Fattah El-Sisi:
Maono ya Misri katika kujenga ustaarabu wa kisasa yanatokana na misingi kadhaa na yanafanya kazi kwa njia nyingi ili kufikia malengo yaliyo wazi, yakiathiri vyema maisha ya raia wa Misri. Raia ndiyo kiini cha maendeleo, lengo, na chombo cha utekelezaji wake.

Mfano wa maendeleo ulioanzishwa na Misri (2022–2027) unathibitisha kuwa maendeleo yanayohitaji ujenzi wa ushirikiano husaidia serikali kushughulikia changamoto za ndani na mizozo ya kimataifa inayohusiana na sekta za kisiasa, kiuchumi, kijamii, na kiusalama. Hali hii inatokana na ukweli kwamba mustakabali wa kimataifa una changamoto nyingi kutokana na mizozo, matatizo changamano, kuibuka upya kwa baadhi ya vitisho vya magonjwa, na mabadiliko ya tabianchi. Ushirikiano wa kitaifa na kimataifa unahitajika ili kukabiliana na changamoto hizi.

Kwa ufupi, jitihada za Misri katika maendeleo zinachora mfano wa kipekee wa maendeleo, unaojumuisha vipimo vya ndani na uhusiano wa kimataifa wa ushirikiano.