Misri na Maendeleo Yake kwa Kujenga Mustakabali Bora

Misri na Maendeleo Yake kwa Kujenga Mustakabali Bora

Imeandikwa na: Marwa Yasser Mahmoud
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Misri imeshuhudia katika miaka ya hivi karibuni maendeleo makubwa yasiyokuwa na mfano katika sekta ya miundombinu, hasa katika sekta ya barabara na njia kuu. Serikali ilizindua miradi mikubwa ya kitaifa inayolenga kufanikisha maendeleo endelevu na kuimarisha uunganishaji kati ya sehemu mbalimbali za nchi. Jitihada hizi zimechangia kuboresha ubora wa maisha ya wananchi na kusaidia uchumi wa kitaifa.

Serikali ya Misri ilizindua Mradi wa Kitaifa wa Barabara mwaka 2014, ikiwa na lengo la kuanzisha mtandao wa kisasa wa barabara utakaosaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Mradi huo ulijumuisha ujenzi wa takriban kilomita 7,000 za barabara mpya, ambapo kilomita 6,300 tayari zimekamilika kwa gharama ya zaidi ya pauni bilioni 155, huku kazi ikiendelea kukamilisha kilomita 700 zilizobaki. Aidha, mtandao wa barabara za zamani umeboreshwa na kuimarishwa kwa urefu wa kilomita 10,000, jambo ambalo limeongeza usalama wa barabara na kurahisisha usafiri kati ya mikoa.

Katika juhudi zake za kuimarisha mahusiano kati ya pande mbili za Mto Nile, serikali ilianzisha ujenzi wa njia kuu mpya 34, na hivyo kuongeza idadi ya njia hizo kutoka 38 kabla ya mwaka 2014 hadi 72 baada ya kutekeleza miradi mipya. Tayari njia 18 zimekamilika, huku kazi ikiendelea kwa njia nyingine 16. Njia hizi zimepunguza umbali kati ya vivuko hadi kilomita 25, jambo ambalo limepunguza muda wa usafiri na kusaidia harakati za biashara pamoja na maendeleo ya miji.

Umakini wa serikali kwa maeneo ya vijijini umejidhihirisha kupitia kuboresha barabara za ndani chini ya Mpango wa Maisha Bora, ambapo kilomita 25,000 za barabara za ndani zimeboreshwa kwa gharama ya pauni bilioni 35.4. Hii ilijumuisha kuboresha barabara katika vijiji na mikoa ya kusini mwa Misri kwa gharama ya zaidi ya pauni bilioni 10, jambo linalosaidia kufikisha huduma kwa maeneo yenye uhitaji mkubwa na kuboresha hali ya maisha ya watu wa vijijini.

Sekta ya madaraja na handaki pia imepata maendeleo makubwa, ambapo idadi ya madaraja nchini kote ilifikia zaidi ya 39,000 hadi kufikia mnamo mwaka 2020. Serikali ilipitisha mpango wa kuanzisha madaraja na handaki 1,000 kwa gharama inayokadiriwa kuwa pauni bilioni 140, ili kurahisisha harakati za magari na kupunguza msongamano katika maeneo ya mijini.

Faida za miradi ya miundombinu hazikubaki katika kuboresha usafiri pekee, bali pia zimechangia kupunguza ajali na kuokoa mabilioni ya pauni kila mwaka kutokana na gharama ya mafuta inayosababishwa na msongamano wa magari. Aidha, miradi hiyo imesaidia kuboresha ubora wa hewa na kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni, jambo ambalo limekuwa na athari chanya kwa afya ya umma. Jitihada hizi zimeongeza nafasi ya Misri duniani katika viashiria vya ubora wa barabara.

Misri inaendelea kwa hatua thabiti kukamilisha miradi mikubwa ya barabara, huku ikilenga kufanikisha muunganisho kamili kati ya njia zote za usafiri wa nchi kavu, baharini na angani. Serikali inalenga kujenga mtandao kamili unaokidhi viwango vya kimataifa, jambo litakalosaidia kufanikisha maendeleo endelevu na kuimarisha nafasi ya Misri kama kituo cha kikanda na kimataifa kwa biashara na huduma za usafirishaji.