Mapinduzi ya Julai 23: Mwanzo wa Enzi ya Uhuru na Mwisho wa Dhuluma

Imeandikwa na: Esmaa Hagag
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Jumanne iliyopita ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzuka kwa mapinduzi ya Julai 23, miaka 72 iliyopita, ambapo yaliitwa “Harakati yenye Baraka” na jina hilo lilidumu. "Maafisa Huru" waliamua kubadilisha historia ya Misri na kurejesha uhuru wa taifa. Mapinduzi hayo yalizuka pamoja na watu waliojitokeza kufanya maandamano, wakilenga kubadilisha Misri na kuifanya kuwa na nafasi muhimu katika eneo la Kiarabu na Afrika.
Mapinduzi matukufu ya Julai 23 yanawakilisha kilele cha mapambano ya muda mrefu yaliyoongozwa na wananchi wa Misri, wakiitetea haki yao ya kuwa na nchi huru. Mojawapo ya sababu za mapinduzi haya ilikuwa kuendelea kwa Mfalme Farouk kutowajali walio wengi na kutegemea vyama vya wachache. Hali mbaya ya kiuchumi, kuzuka kwa Vita vya Palestina, na ushiriki wa Mfalme Farouk katika vita hivyo bila silaha na risasi zinazofaa, pia vilichangia kwa kiasi kikubwa. Hii ilipelekea kushindwa kwa Misri na hali mbaya zaidi ya kiuchumi nchini.
Miongoni mwa mafanikio ya mapinduzi nchini Misri ni kutaifishwa kwa Mfereji wa Suez, kurejeshwa kwa heshima na uhuru uliokuwa umeporwa na wakoloni wanyanyasaji, na kuanzishwa kwa utawala wa serikali ya Misri. Pia, mapinduzi haya yalivunja utawala wa kifalme, yakaanzisha jamhuri, na kusainiwa kwa mkataba wa uokoaji baada ya miaka 74 ya dhuluma, ufisadi, na utumwa. Huu ulikuwa mwanzo wa safari ya Misri kuelekea uhuru, usawa, na demokrasia.
Tukiangalia mapinduzi hayo kwa mtazamo wa Uingereza, tutagundua kuwa hayakutegemea mapinduzi yatokee, lakini nyaraka za Uingereza zilibainisha kuwa licha ya ushawishi wa Uingereza, kama nchi ya Magharibi, serikali yake ya kifalme mjini London ilishangazwa na mapinduzi yaliyopokea msaada wa watu wa Misri, na kuongozwa baada ya miaka 4 kuondoka kwa Uingereza kutoka Misri.
Kwa mujibu wa nyaraka za Uingereza, Kamati ya Ujasusi ya Pamoja iliandika ripoti muda mfupi kabla ya mapinduzi, ikieleza kwamba haikuwa na uwezekano wa Wamisri kufanya mapinduzi yoyote ambayo yangebadilisha hali ya Misri. Kazi muhimu zaidi ya Kamati ya Ujasusi ya Pamoja, inayofuatia moja kwa moja kwa Urais wa Baraza la Mawaziri, ilikuwa ni ufuatiliaji wa matukio ya kimataifa yanayoathiri maslahi ya kitaifa nje ya nchi. Hata hivyo, kamati hiyo haikufanya kazi yake kikamilifu.
Lakini Ujasusi wa Majini wa Uingereza uliwahi kuonya kwamba huenda jeshi lilikuwa linapanga jambo kubwa. Mnamo tarehe Julai 8, kabla ya "Maafisa Huru" kufanya mapinduzi hayo kwa siku kumi na tano, kamanda wa Ofisi ya Ujasusi wa Majini katika Mashariki ya Kati aliandika ripoti kwa uongozi wake, akieleza mzozo unaozidi kuwa mbaya nchini Misri na ukosefu wa uwezo wa Mfalme kudhibiti hali hiyo. Hata hivyo, habari hii haikufika London kwa wakati. Kwa hivyo, Uingereza haikuweza kuzuia mapinduzi hayo.