Sera za Uwezeshaji wa Kiuchumi Familia Nchini Misri

Sera za Uwezeshaji wa Kiuchumi Familia Nchini Misri

Imeandikwa na: Abdallah Yassin

Imetafsiriwa na: Hagar Elsopky

Imehaririwa na: Mervat Sakr

Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Serikali ya Misri, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi, inatekeleza kwa dhati sera za umma zinazolenga kuwawezesha familia za Misri, jambo linalodhihirisha nia ya kweli ya serikali katika kuimarisha ustawi wa familia hizi kiuchumi na kijamii. Serikali inaendelea kupanua na kuimarisha utekelezaji wa programu mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Uthibitisho wa jitihada hizi ulionekana mnamo mwaka 2022 ulipotangazwa kuwa Mwaka wa Asasi za Kiraia nchini Misri, hatua iliyolenga kuandaa familia za Misri kupitia mfumo wa kisayansi uliojengwa juu ya misingi ya kitaifa. Hatua hii ilianza kwa kuzinduliwa kwa programu za kuunga mkono mashirika na taasisi za kiraia, ikiwa ni pamoja na mpango wa kitaifa wa “Maisha Bora” (Hayah Karima).

Mipango hii inalenga kuwa msingi wa kuondoa umaskini na utegemezi, kwa kuwaandaa wananchi wa kawaida kufikia hali ya kujitegemea kiuchumi na kijamii, bila kutegemea misaada kutoka kwa wengine. Uwezeshaji huu huwasaidia wananchi kubadilika kutoka hali ya watumiaji wa bidhaa hadi kuwa wazalishaji wa mahitaji yao na ya jamii zao kwa ujumla.

Ili kuhakikisha utekelezaji bora wa sera hizi, kunahitajika mshikamano na ushirikiano baina ya taasisi zote za serikali, kwa kushirikiana kwa karibu na mashirika ya kiraia, ili kuendeleza gurudumu la maendeleo ya taifa na kuinua hali ya familia za Misri kwa kiwango cha juu.

Bila shaka, mashirika yasiyo ya kiserikali yana mchango mkubwa katika mchakato wa kuwawezesha familia kiuchumi, kwani yamekuwa chombo muhimu cha kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo. Hili limesisitizwa katika nyaraka mbalimbali za kimataifa za Umoja wa Mataifa na limeungwa mkono na hotuba za viongozi wa serikali nyingi duniani, hasa zile za nchi zinazoendelea.

Vilevile, Tamko la Haki ya Maendeleo linaweka wajibu kwa serikali kuhamasisha ushiriki na kuhakikisha upatikanaji wa haki za msingi, jambo linaloashiria majukumu makubwa ya serikali katika kuwezesha ushiriki wa wananchi, hasa kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali.

Maeneo makuu ya kuwawezesha familia za Misri kiuchumi ni pamoja na: mafunzo na ajira, ujenzi wa uwezo, na ujumuishaji wa kijamii. Ingawa dhana ya uwezeshaji ni pana na jumuishi, kiini chake kinajikita katika vipengele viwili muhimu: kuwawezesha familia kiuchumi na kukomesha hali ya umaskini na utegemezi.

Kwanza: Kuimarisha familia kiuchumi.

Pili: Kuondoa hatua ya umaskini na uhitaji.

Hii ina maana ya kuendeleza uwezo wa mtu binafsi na kutumia uwezo huo kupitia ushiriki hai. Uwezeshaji unahusisha pia uwezo wa kubadilisha na kuleta athari. Kwa kuwa dhana ya uwezeshaji ni ya kina na jumuishi, inatumika kama muongozo wa kuweka mipango na sera katika viwango vya mtu binafsi na jamii, na katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kijamii.

Uwezeshaji wa kiuchumi na kijamii ni mojawapo ya sifa kuu za mfumo wa haki unaolenga usawa kwa wote na kuwawezesha makundi yaliyotengwa. Ukuaji na maendeleo ya jamii yoyote yanategemea kwa kiasi kikubwa kiwango cha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya jamii na kuitambua haki hiyo kuwa ni mojawapo ya haki za msingi kwa kila mtu katika jamii.

Aidha, ni kielelezo cha mafanikio ya serikali katika kuondoa au kupunguza pengo kati ya makundi yanayohitaji msaada mkubwa na yale yaliyo juu kiuchumi. Uwezeshaji wa kiuchumi ni moja ya nguzo kuu za maendeleo, na ajenda ya kiuchumi ya Misri inaweka katika kipaumbele chake kufanikisha hali ya kujitegemea kiuchumi, kuondoa umaskini na uhitaji, na kubadilisha familia ya Misri kutoka kuwa watumiaji wa bidhaa kuwa wazalishaji wanaochangia katika kuimarisha uchumi wa taifa.