Mapinduzi ya Julai 23
Imeandikwa na: Ibrahim Al-Saqqa
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Misri ni nchi tajiri sana kwa historia yake, na kuna kumbukumbu ya kipekee iliyochimbwa ndani ya akili za Wamisri wote. Ni kumbukumbu adhimu ya Mapinduzi ya Julai 23. Mnamo mwaka 1952, Misri ilikuwa bado chini ya utawala wa kifalme, utawala ambao ulijumuisha kila aina ya ufisadi, pamoja na ukoloni wa Uingereza. Hali hiyo ilisababisha kupamba moto kwa mapinduzi yaliyokuwa na matarajio mema katika nyanja mbalimbali, na pia yaliisaidia nchi nyingine kupata uhuru wao.
Matarajio na Maono ya Mapinduzi ya Julai 23
Mapinduzi hayo yaliyoanzishwa na maafisa wa kijeshi wa mapinduzi kwa njia ya siri, waliweza kupindukia huduma ya ujasusi ya Uingereza kwa ufanisi. Wanajeshi na raia walishiriki pamoja kwa mara ya kwanza katika mapinduzi hayo, na kusababisha gumzo kubwa duniani ambalo halina mfanano. Yalikuwa na matarajio mengi kama:
1. Kusitisha Uwepo wa Uingereza na Kuanzisha Utawala wa Jamhuri: Lengo kuu la tukio hilo adhimu lilikuwa ni kuondosha ukoloni ambao ulikuwa umeipora mali za nchi na kuharibu kila kitu. Kwa hiyo, mapinduzi yalifanya juu chini kuhakikisha kuanzisha nchi yenye uhuru kwenye ardhi zake. Pia, maafisa hao waliamua kuanzisha mfumo wa jamhuri kwa kumchagua "Mohammad Nagibu" kama Rais wa kwanza wa Misri.
2. Kuboresha Hali ya Kijamii: Hali za Wamisri katika kipindi hiki ziliporomoka sana kutokana na vitendo viovu vya Waingereza na Mfalme Farouk. Kwa hiyo, uamuzi wa kuanzisha mapinduzi kama hayo ulikuwa na mpango mkubwa wa kuimarisha hali za kijamii nchini Misri. Mapinduzi hayo yalilenga kuhakikisha uwiano wa kijamii kwa kumaliza utawala wa ardhi wa kikabila, kugawa mali bila kudhulumu mtu yeyote, kutokomeza umasikini pamoja na kuboresha viwango vya maisha ya raia. Pia, Uingereza ilizuia elimu katika kipindi hicho na kuharibisha mfumo wake; kwa hiyo, miongoni mwa mipango ya mapinduzi ilikuwa ni kuimarisha mfumo mpya wa elimu kwa watu wote. Aidha, mapinduzi hayo yalilenga kuboresha huduma za afya na kuzitoa kwa wote.
Kwa kutaja matarajio ya mapinduzi ya Julai 23, hatuwezi kumaliza, kwani yalikuwa na matarajio mengi na tumetaja ya muhimu zaidi. Pia, kwa kuzungumzia siku hiyo, hana budi kuonesha nafasi kubwa ya mapinduzi hayo katika kusaidia nchi nyingi za Kiafrika kupata uhuru wao. Lakini vipi mapinduzi hayo yalifanya hivyo?
1. Msaada wa Kisiasa na Kifedha: Misri ilitoa silaha na vifaa vya kijeshi kwa Chama cha Ukombozi wa Kitaifa cha Algeria, pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa wao wa kijeshi. Pia, Misri iliwapokea maelfu ya wakimbizi wa Algeria na kuwapa makazi na huduma za matunzo. Wakati wa mgogoro wa Congo, Misri ilipeleka vikosi vya kulinda amani nchini Congo kusaidia serikali halali na kupambana na waasi walioungwa mkono na mataifa ya kigeni. Vilevile, ilitoa msaada wa kifedha na kijeshi kwa Harakati ya Mkutano wa Kitaifa ya Congress (ANC), na iliwakaribisha viongozi wengi wa chama hicho kwenye ardhi yake.
2. Uongozi wa Kiroho: Hotuba ya Bandung: Hotuba ya Rais Gamal Abdel Nasser katika Mkutano wa Bandung mwaka 1955 ilikuwa tangazo la kupanda kwa nguvu mpya ulimwenguni, ambayo ni nguvu ya mataifa mapya yaliyojipatia uhuru na yanayoendelea. Hotuba hii iliwaongoza watu wa Afrika na kuwapa matumaini ya siku zijazo.
Ziara za Viongozi wa Afrika: Misri iliwakaribisha viongozi wengi wa Afrika kama Nelson Mandela na Kwame Nkrumah, jambo ambalo liliongeza hadhi ya Misri kama nguvu yenye ushawishi barani.
3. Kuanzisha Mashirika ya Mshikamano na Ushirikiano wa Kiuchumi: Misri ilikuwa miongoni mwa wale walioongoza wito wa kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Afrika, ambalo lilicheza jukumu muhimu katika kuratibu juhudi za Afrika kufikia umoja na maendeleo. Pia, Misri imesaini mikataba mingi ya biashara na nchi za Afrika, jambo ambalo limechangia kuimarisha biashara kati ya nchi za Afrika. Vilevile, imetoa msaada wa kiufundi na kifedha kutekeleza miradi ya maendeleo katika nchi nyingi za Afrika, kama vile ujenzi wa shule na hospitali.
Mwishoni, mapinduzi hayo hayakuishia kwa kufanikisha matumaini ya watu wake tu, bali pia yalipanua malengo yake kwa kutoa msaada kwa nchi jirani, zikiwapa fedha na vifaa vyote muhimu ili kupata uhuru kamili. Ilikuwa kama mwanga uliokuja baada ya miaka ya giza totoro, ukamaliza ufisadi na vurugu na kuhifadhi heshima ya mataifa mengine. Mapinduzi haya yalitoa mengi na bado yamechongwa mioyoni mwetu kabla ya akili zetu.