Athari za Mapinduzi Zinan'gaa katika Anga ya Bara la Afrika
Imeandikwa na: Menna Ashraf Farouk
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
"Kama kwa Afrika, hatuwezi kujitenga nayo, hata kama tungetaka, kwa sababu sisi ni sehemu ya bara la Afrika." Hivi ndivyo Hayati Rais Gamal Abdel Nasser alivyoelezea uhusiano wa karibu kati ya Misri na bara la Afrika wakati wa hotuba zake. Misri ilichukua msimamo wazi kuhusu maono yake kwa bara la Afrika.
Mapinduzi hayo yalikuwa na nafasi muhimu katika kuunga mkono harakati za ukombozi wa Afrika, kwani kabla ya mapinduzi, idadi ya nchi zilizokombolewa ilikuwa nne tu. Hadi kufikia mwaka 1963, kutokana na mapinduzi hayo, nchi thelathini zilikuwa zimekombolewa. Mapinduzi hayo pia yalianzisha mahusiano ya karibu na nchi huru kama Guinea, Ghana, na Mali.
Inafaa kukumbuka kuwa wazo la ukombozi wa Kiafrika lilianza huko Kairo katikati ya miaka ya hamsini, ambapo mapinduzi hayo yaliunga mkono sana harakati za Maumau nchini Kenya. Aidha, Misri iliunga mkono juhudi za kudumisha utulivu katika Kongo kwa kutuma vikosi vya kijeshi, na pia ilichangia sana kuunga mkono Mkutano wa Kitaifa wa Afrika unaoongozwa na Nelson Mandela.
Mapinduzi hayo yalicheza jukumu muhimu katika kusaidia nchi za Afrika kupata uhuru wao. Kwa mfano, yaliwaunga mkono wanaharakati wa Algeria, na serikali ya kwanza ya Algeria ilianzishwa mjini Kairo. Mapinduzi hayo yaliendelea kuunga mkono harakati za ukombozi hadi Algeria iliposhinda ukoloni wa Ufaransa mnamo mwaka 1962, hali iliyojirudia pia huko Iraki na Yemen.
Kwa hivyo, mapinduzi hayo yalikuwa na nafasi kubwa katika historia ya nchi za bara la Afrika. Mafanikio yake yalienea kwa kila nchi na yakawa msingi wa uhusiano mzuri kati ya nchi za bara la Afrika na wale waliokuwa waanzilishi wa mafanikio hayo. Mwisho wa yote, mapinduzi hayo yaliweka msingi wa mwendelezo wa ukombozi hadi nchi zote za Afrika zilipopata uhuru kamili, na kuungwa mkono katika kuanzisha taasisi za serikali kwa ajili ya ujenzi wa nchi hizo.