Maendeleo Endelevu Nchini Libya

Maendeleo Endelevu Nchini Libya

Imeandikwa na: Balqis Saber Abdelhadi
Mtafiti wa Shahada ya Uzamili, Chuo Kikuu cha Kairo – Kitivo cha Mafunzo ya Afrika
Imetafsiriwa na: Maryam Muhammad Sayed 
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Libya imechukua mkakati wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Endelevu kwa msingi wa uzoefu wake katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Kwa kuwa Wizara ya Mipango ndiyo yenye mamlaka ya kuweka sera na mipango ya maendeleo ya kitaifa, wizara hiyo imejitahidi kuunda mfumo wa taasisi kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Hii ilifanikishwa kupitia kuundwa kwa Kamati ya Maendeleo Endelevu, ambayo inajumuisha wataalamu na wahusika kutoka sekta na taasisi husika. Kamati hii ilipewa majukumu mbalimbali, yakiwemo: Kulinganisha na kuingiza Malengo ya Maendeleo Endelevu katika mikakati na mipango ya maendeleo ya kitaifa kwa kushirikiana na sekta mbalimbali, Kufuatilia maendeleo yaliyopatikana katika kufanikisha malengo haya na Kuandaa na kuwasilisha ripoti za tathmini ya hiari.
Ripoti ya Kitaifa ya Hiari ya Libya mnamo mwaka 2020 iliandaliwa kwa mujibu wa mpango wa utekelezaji uliowekwa kwa ajili ya lengo hili. Mpango huo ulijumuisha utaratibu wa utekelezaji kwa mujibu wa ratiba maalumu. Katika utekelezaji wake, timu ya kazi iliundwa kwa kila lengo lililochaguliwa, na hatimaye kikundi kidogo cha uratibu kilipewa jukumu la kukusanya ripoti kutoka kwa timu mbalimbali na kuziunganisha katika ripoti ya mwisho.

Ripoti ya Kitaifa ya Hiari ya Libya kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu iliandaliwa kwa ushirikishwaji mpana wa jamii chini ya uongozi wa Wizara ya Mipango kupitia Jukwaa la Maendeleo Endelevu la Libya kama jukwaa la mazungumzo, mwingiliano, kubadilishana uzoefu, na uratibu wa juhudi. Lengo lake lilikuwa kujumuisha na kuimarisha ushiriki wa wadau wote. Jukwaa hili lilikuwa chanzo muhimu cha msaada kwa kazi ya Kamati ya Maendeleo Endelevu ili kufanikisha Ajenda ya 2030 kupitia semina, warsha, na mikutano iliyofanyika kwa madhumuni hayo.

Kupitia Wizara ya Mipango, Libya imeandaa mikakati na mipango kadhaa ya kitaifa inayosaidia kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu. Serikali ilihakikisha kuwa mikakati yake ya kitaifa katika sekta mbalimbali inalingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu, kama vile Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Mbadala na Ufanisi wa Nishati (2030) na Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Rasilimali za Maji nchini Libya (2020-2022), miongoni mwa mingine.
Aidha, katika jitihada za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, Wizara ya Mipango ilianzisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu kwa sekta zote za taifa kwa kipindi cha 2020-2022, unajumuisha, hasa, ujumuishaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliopendekezwa uliotajwa.

Kwa kuamini kwamba maendeleo endelevu ni suala la kitaifa linalohitaji ushiriki wa makundi yote yanayohusika na Malengo ya Maendeleo Endelevu, Libya imehimiza mashirika ya kiraia na sekta binafsi kupokea dhana ya uendelevu. Hii ilifanyika kwa msaada wa Wizara ya Mipango, iliyoratibu kuanzishwa kwa Wakala wa Maendeleo wa Libya kama taasisi isiyo ya kiserikali, kwa kushirikiana na jamii ya kiraia na sekta binafsi, ili kuchangia kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa kitaifa unakuwa endelevu.

Vilevile, wajasiriamali vijana na wanawake walihamasishwa kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa njia endelevu kwa kuhimiza ujasiriamali katika miradi midogo na ya kati. Katika muktadha huu, mikutano kadhaa na warsha zilifanyika, pamoja na kuanzishwa kwa jukwaa la kitaifa la ujasiriamali ili kuimarisha mchango wa wajasiriamali vijana na wanawake katika kuchochea ukuaji wa uchumi.

Katika juhudi za kuendeleza ugatuzi na kuimarisha jukumu la manispaa na mamlaka za mitaa katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, majukumu mengi ya wizara yalihamishiwa kwa ngazi ya mitaa katika halmashauri za manispaa.

Ripoti inaonesha kuwa Libya inakabiliwa na changamoto nyingi katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, muhimu zaidi ikiwa ni ukosefu wa utulivu wa kisiasa, hali ya usalama isiyo imara, uhamiaji haramu, na ongezeko la wakimbizi wa ndani na watu waliolazimika kuhama makazi yao, hali ambayo ni changamoto kubwa kwa kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

Aidha, uchumi wa Libya unategemea rasilimali za mafuta na gesi, na katika hali ambapo ugavi wa rasilimali hizi unasitishwa, mapato muhimu kwa ajili ya programu za maendeleo na ujenzi wa upya hukwama. Pia, kuna changamoto ya upungufu wa takwimu, taarifa, na viashiria muhimu vya kupima na kutathmini maendeleo kutokana na mazingira ya sasa, jambo linaloathiri vibaya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

Hatimaye, wakati Libya inawasilisha Ripoti yake ya Kitaifa ya Hiari ya kwanza katika Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu, inatarajia kuonesha juhudi zake katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu. Hata hivyo, inatambua kwamba bado kuna safari ndefu mbele, na mafanikio ya malengo haya yanategemea uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo. Hii inahitaji juhudi za pamoja za kimataifa na kikanda kusaidia juhudi za kitaifa. Ni muhimu pia kuthibitisha dhamira ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ili kuhakikisha ustawi wa Walibya na uhifadhi wa rasilimali kwa vizazi vijavyo.

Maono ya "Ihya Libya 2030" ni mwito wa kuchukua hatua kwa Walibya wote ili kuiweka nchi kwenye njia ya maendeleo endelevu. Utekelezaji wa dira hii utafanyika kwa awamu mbili mfululizo. Awamu ya kwanza, inayohusu kipindi cha 2022-2025, italenga kufanikisha utulivu na ujenzi upya kupitia mazungumzo ya kitaifa na ya ndani, pamoja na maridhiano, sambamba na juhudi za kufanikisha vipaumbele vya maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na mageuzi katika sekta ya umma.
Awamu ya pili, inayohusu kipindi cha 2026-2030, itajikita katika ukuaji endelevu kupitia mbinu thabiti za kusimamia migogoro inayoendelea, kukuza sekta binafsi, kuwekeza katika miradi mikubwa ya miundombinu, na kutekeleza mageuzi ya kimuundo ili kuhakikisha uwepo wa sekta ya umma inayowajibika, inayozingatia sifa na utendaji bora.