Mahdi Yacoub: Hadithi ya Matibabu na Mfano wa Ubinadamu

Mahdi Yacoub: Hadithi ya Matibabu na Mfano wa Ubinadamu


Imeandikwa na: Malak Diaa
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Daktari Magdi Yacoub anachukuliwa kuwa mmoja wa majina maarufu zaidi katika nyanja ya upasuaji wa moyo duniani, si tu kwa ustadi wake wa kitabibu, bali pia kwa safari yake ya kibinadamu iliyowahamasisha mamilioni. Alizaliwa nchini Misri, lakini alifikia umaarufu wa kimataifa kwa maarifa yake na juhudi zake katika kutibu magonjwa ya moyo, hasa kwa watoto. Katika makala hii, tunaangazia vituo muhimu katika maisha ya daktari huyu wa kipekee.

Amezaliwa katika mji wa Belbeis, katika mkoa wa Sharqia. Alikulia katika familia iliyothamini elimu, ambapo baba yake alikuwa daktari, jambo lililomjengea upendo wa udaktari tangu akiwa mdogo. Alifanya uamuzi wa kujitolea kwa upasuaji wa moyo baada ya shangazi yake kufariki kwa ugonjwa wa moyo, hivyo akaamua kuokoa maisha ya wengine.

Alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kairo, katika Kitivo cha Tiba mwaka 1957, ambako alibobea katika upasuaji wa moyo. Baadaye alisafiri kwenda Uingereza kuendeleza masomo na mafunzo yake, na jina lake likang'aa haraka katika nyanja za kitabibu kutokana na ustadi na umahiri wake mkubwa.

Alifanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza wa kupandikiza moyo nchini Uingereza mwaka 1980. Kisha alianzisha taasisi ya “Mfululizo wa Tumaini” ambayo ilichangia katika matibabu ya maelfu ya watoto kutoka nchi mbalimbali, bila malipo. Taasisi hii ilikuwa na athari kubwa kimataifa, hasa katika hospitali ya Harfield mjini London.

Licha ya mafanikio yake ya kimataifa, Daktari Magdi Yacoub hakusahau nchi yake ya asili. Mnamo mwaka 2009, alianzisha Taasisi ya Magdi Yacoub ya Magonjwa na Utafiti wa Moyo huko Aswan, imeyokuwa miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya matibabu ya moyo katika Mashariki ya Kati, na inatoa huduma za matibabu bure kabisa.

Daktari Magdi Yacoub amepokea tuzo nyingi, kama vile medali ya heshima ya Uingereza kutoka kwa Malkia Elizabeth, pamoja na cheo cha Knight katika Ufalme wa Muingereza. Pia alikabidhiwa Taji la Nile kutoka Misri, ambayo ni tuzo ya heshima ya juu zaidi nchini humo.

Magdi Yacoub anajulikana kwa unyenyekevu wake mkubwa na roho yake ya kibinadamu. Hafuatilii umaarufu au utajiri, bali hutafuta kuokoa maisha. Amejitolea maisha yake kwa ajili ya kutibu maskini na wahitaji.

Daktari Magdi Yacoub si daktari tu, bali ni hadithi ya maisha na mfano wa kuigwa katika elimu na ubinadamu. Hadithi yake inaonyesha jinsi sayansi inavyoweza kuwa njia ya kuleta wema na kubadilisha dunia. Jina lake litaendelea kubaki limeandikwa moyoni mwa mamilioni aliowaokoa, na katika kumbukumbu ya wanadamu wote.