Kiwango cha Kitamaduni na Uhusiano Wake na Mtu Binafsi na Familia

Imeandikwa na:Hussein Abdurabbu
Imetafsiriwa na: Walaa Marey
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Kuna maana nyingi za neno "utamaduni": utamaduni ni tabia ya kijamii ya watu binafsi na unahusisha aina mbalimbali za mienendo inayojifunzwa kupitia mafunzo ya kijamii na mazoea ya kijamii. Vilevile, utamaduni ni kipimo cha ustaarabu na ni jiwe la msingi katika hatua ya maendeleo na kukuza ujuzi wa watu ndani ya jamii.
Hakika, utamaduni humpa mwanadamu uwezo wa kufikiri na kutambua kikamilifu yanayomzunguka. Ni pia uwezo wa mtu kuelewa na kufahamu taaluma zote za kibinadamu, sanaa, na maarifa. Hivyo basi, utamaduni ndio msingi wa kujenga haiba ya mwanadamu na ni kipengele chenye athari kubwa katika uhusiano wake na jamii.
Wanajamii wanapojifunza kuhusu maisha yanayowazunguka, basi huwa wanaishi ndani ya jamii yenye aina fulani ya utamaduni unaoathiri watu wote na kujenga haiba ya wanajamii. Ikiwa jamii ina kiwango cha juu cha utamaduni na ustaarabu, basi tunaona watu wake wakistahili kuwa katika hadhi hiyo ya juu. Kwa hivyo, msingi wa kujenga jamii bora unategemea utamaduni wa watu wake, ambao ni mambo yasiyoonekana kama vile mila, maadili, fikra, na urithi wa pamoja. Hakuna jamii yoyote inayoweza kusonga mbele bila kuwa na kiwango cha juu cha utamaduni katika nyanja zote – iwe kijamii au kimazingira – maana utamaduni unamaanisha maendeleo, ustawi, na mafanikio katika taaluma zote.
Athari za Utamaduni katika Maisha ya Mtu Binafsi katika Jamii
Utamaduni unaathiri fikra za mtu binafsi. Ikiwa mtu anakulia katika jamii ambayo utamaduni wake unathamini masuala ya kisayansi, basi tunaona namna akili yake inavyokua ikiwa na mwelekeo wa kielimu na upendeleo wa kuwa mbunifu katika fikra za kisayansi. Hali hiyo huendelea kuwa sehemu ya maisha yake yote.
Kwa hivyo, watu wenye kiwango cha juu cha utamaduni, ustaarabu, na maendeleo mara nyingi hutokea katika jamii zinazojali sana utamaduni. Miongoni mwa faida kubwa za utamaduni kwa mtu binafsi ni nafasi ya elimu na utamaduni katika jamii yake. Kwa upande mwingine, mtu anayekulia katika jamii isiyo na utamaduni wala ustaarabu na heshima, huwa hana maarifa wala mwamko wa kitamaduni.
Athari za Utamaduni katika Maisha ya Familia
Umuhimu wa kiwango cha kitamaduni katika familia huonekana kupitia kiwango cha elimu na maarifa ya baba na mama. Jukumu la kuwalea watoto vizuri, kuwapa elimu sahihi, na kuwaepusha na mambo yanayoweza kuharibu maisha yao linabebwa na wazazi. Ni wao wanaopaswa kupanda mbegu sahihi katika fikra za watoto kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii.
Familia yenye utamaduni ni msingi wa mafanikio ya watoto wao kitaaluma na ni mwongozo mzuri wa malezi. Tunamwona mtoto aliyelelewa katika familia ya namna hii akiwa na mapenzi makubwa kwa masomo, akijali kwa dhati kuhusu mafanikio yake ya kielimu – hali ambayo hutokana na uangalizi na msaada wa wazazi. Hapo ndipo familia hii huanza safari sahihi ya elimu na malezi bora, na hapo ndipo jamii na taifa huweza kufaidika na watu wenye kiwango cha juu cha utamaduni kutoka familia hiyo.