Kuwawezesha wanawake nchini Misri

Imetafsiriwa na: Walaa Marey
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Kwa muda mrefu, wanawake wamekuwa kiungo hai katika ujenzi wa ustaarabu na uundaji wa jamii, lakini kuwawezesha hakujapata uangalizi wa kutosha katika historia. Kwa kasi ya mabadiliko duniani inavyozidi kuongezeka, suala la kuwawezesha wanawake limekuwa miongoni mwa masuala muhimu katika ulingo wa kimataifa, kutokana na athari zake za moja kwa moja kwa maendeleo jumuishi pamoja na uthabiti wa kijamii na kiuchumi.
“Uwezeshaji wa wanawake” unafasiriwa kama mchakato unaowapa wanawake uwezo wa kufanya maamuzi kwa uhuru, kuwa na udhibiti kamili wa maisha yao binafsi na ya kitaaluma, na kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika nyanja zote za maisha. Umoja wa Mataifa umeueleza kuwa ni "kuwaruhusu wanawake kushiriki kikamilifu kwa usawa na wanaume katika maisha ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, pamoja na kuondoa vikwazo vinavyowazuia kufikia fursa."
Katika muktadha huu, mtaalamu wa masuala ya kijinsia Michelle Bachelet – Kamishna Mkuu wa zamani wa Haki za Binadamu – anasisitiza kuwa "kuwawezesha wanawake si tu haki ya binadamu, bali ni njia madhubuti ya kuboresha afya ya jamii, kuimarisha uchumi na kufanikisha maendeleo endelevu." Aidha, mtafiti Amartya Sen, mshindi wa Tuzo ya Nobel katika Uchumi, anaamini kuwa "kuwawezesha wanawake ni nguzo kuu katika kupunguza umaskini na kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha."
Dhima ya kuwawezesha wanawake haibaki tena kuwa kauli mbiu au mipango ya kinadharia pekee, bali imekuwa hitaji la msingi katika ajenda za mataifa, taasisi na mashirika ya kimataifa, ikizingatiwa kuwa ni chombo chenye ufanisi katika kufanikisha usawa na haki, na ni msingi muhimu usioweza kupuuzwa katika safari ya kuendeleza jamii.
Mageuzi Yasiyo na Mwingiliano wa Kihistoria katika Kuwainua Wanawake wa Misri: Kuanzia Katiba ya 2014 hadi Utekelezaji wa Mikakati ya Kitaifa
Katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, ajenda ya kuwawezesha wanawake wa Misri imepata mageuzi yasiyo na kifani, kitaifa na kimataifa. Mabadiliko haya yalianza mwezi Juni 2014 kwa kuingia kwa “enzi ya dhahabu” kwa mwanamke wa Misri, iliyoirudishia hadhi yake kutokana na kuwepo kwa nia ya kisiasa thabiti inayoamini kwamba kuwawezesha wanawake ni jukumu la kitaifa. Kutokana na imani hii, haki za wanawake zilizotamkwa katika Katiba zilitafsiriwa katika sheria, mikakati, na mipango ya utekelezaji inayotekelezwa na taasisi za serikali na zisizo za serikali. Hakuna hotuba rasmi ya kisiasa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri – iwe katika majukwaa ya ndani au ya kimataifa – iliyokosa kupongeza mchango wa mwanamke wa Misri. Hatua hii imeifanya Misri kuwa mfano wa kuigwa duniani katika kuwawezesha wanawake na kufanikisha usawa wa kijinsia.
Mwanzo ulikuwa ni Katiba ya mwaka 2014 iliyojumuisha zaidi ya vifungu 20 vinavyohusiana na uraia, usawa, na uhalalishaji wa vitendo vya ukatili na ubaguzi dhidi ya wanawake. Mnamo Februari 2016, Baraza Kuu la Kitaifa la Wanawake liliundwa upya kama chombo cha kitaifa kinachoshughulikia kuwawezesha wanawake na kusimamia utekelezaji wa usawa wa kijinsia nchini.
Mkakati wa Kitaifa wa Kuwainua Wanawake wa Misri 2030
Baraza la Kitaifa la Wanawake lilianza kazi mwaka 2016 kwa kuandaa dira na mpango wa kitaifa kuhusu wanawake nchini Misri. Liliandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kuwainua Wanawake wa Misri 2030, ambapo Misri ikawa nchi ya kwanza duniani kuzindua mkakati wa kitaifa wa kuwawezesha wanawake unaolingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Hatua hii ilithibitisha imani ya dola ya Misri katika mchango wa mwanamke wa Misri katika ustawi wa jamii na umuhimu wa kumwezesha. Rais Abdel Fattah El-Sisi aliridhia mkakati huu mnamo mwaka 2017 kama ramani ya barabara ya serikali katika utekelezaji wa mipango na shughuli zote zinazohusu kuwawezesha wanawake. Mkakati huu una viashiria 34 vinavyohusiana na Malengo ya Maendeleo Endelevu na unajumuisha nguzo kuu nne:
• Uwezeshaji wa kisiasa na uongozi
• Uwezeshaji wa kiuchumi
• Uwezeshaji wa kijamii
• Ulinzi dhidi ya ukatili
Ushiriki wa Misri katika Uwezeshaji wa Wanawake Barani Afrika
Mshauri Amaal Ammar, Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Wanawake, alishiriki katika Mkutano wa 15 wa Afrika wa Viongozi Wanawake katika Biashara na Uwezeshaji wa Kiuchumi, ulioandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika. Alisisitiza kuwa ajenda ya kuwawezesha wanawake barani Afrika inapata msukumo mkubwa kutoka kwa uongozi wa kisiasa wa Misri. Aliongeza kuwa kuwezesha kiuchumi wanawake katika nchi za Afrika ni jambo la lazima na ni nguzo muhimu katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063. Hatua hii huongeza ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini, kuboresha maisha ya familia, na kuongeza fursa ya kupata elimu na huduma za afya.
Aidha, uwezeshaji huu hupunguza pengo la kijinsia katika maeneo kama mishahara, ajira, umiliki wa mali, na kuhifadhi mazingira. Pia huongeza ubunifu na utofauti katika sekta mbalimbali, huku ukiimarisha uhuru binafsi wa wanawake na uwezo wao wa kufanya maamuzi ya kujitegemea. Kwa sababu hiyo, Baraza la Kitaifa la Wanawake limeweka kipaumbele katika kusaidia kuwawezesha wanawake katika ngazi ya Afrika. Mshauri Amaal Ammar alithibitisha kwamba baraza hilo lilizindua mradi wa mafunzo kwa wanawake wa Afrika katika eneo la uwezeshaji wa kiuchumi, katika ushirikiano na Wakala wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Misri wa Wizara ya Mambo ya Nje, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Misri wakati wa Urais wake wa Umoja wa Afrika.
Mafanikio ya Mwanamke wa Misri: Hatua Muhimu katika Kuwezeshwa kwa Wanawake na Ushiriki katika Uamuzi wa Sera
Wanawake wa Misri wamepata mafanikio makubwa na ya kihistoria katika safari yao ya kuwezeshwa na kufikia nafasi za juu katika uongozi na uamuzi wa sera. Miongoni mwa mafanikio haya ni kuteuliwa kwa mwanamke wa kwanza kuwa gavana, mwanamke wa kwanza kuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Rais wa Jamhuri, na naibu wa kwanza mwanamke wa Gavana wa Benki Kuu. Aidha, wanawake sita waliteuliwa kuwa manaibu wa Rais wa Mamlaka ya Mashauri ya Kisheria ya Serikali.
Idadi ya wanawake mawaziri iliongezeka hadi kufikia asilimia 20. Tarehe 14 Juni 2018, serikali iliyoongozwa na Dkt. Mostafa Madbouly iliapishwa mbele ya Rais Abdel Fattah El-Sisi, ikiwa na mawaziri wanawake wanane, jambo linalodhihirisha dhamira ya kisiasa ya kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi.
Vilevile, sheria mbalimbali zilitungwa ili kukomesha aina yoyote ya ubaguzi dhidi ya wanawake, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa adhabu dhidi ya ukeketaji, unyanyasaji wa kingono, na kurithisha wanawake mali. Sheria ya Uwekezaji pia ilijumuisha kifungu kinachohakikisha usawa wa fursa kati ya mwanamume na mwanamke, huku pia ikisaidia miradi midogo na ya kati.
Dhamira ya kisiasa ya serikali ya Misri iliendelea kudhihirika kupitia kutangazwa kwa miradi midogo sana (micro-projects) kama kipaumbele cha kitaifa. Wanawake hasa wale wanaowatunza familia zao na familia masikini walinufaika kwa kiasi kikubwa. Katika robo ya kwanza ya mwaka wa mwanamke 2017, zaidi ya wanawake milioni 1.33 walipata mikopo yenye thamani ya pauni bilioni 4.55 za Kimisri kwa ajili ya miradi midogo sana.
Aidha, serikali inatoa huduma za malezi ya awali ya watoto ili kuwezesha akina mama wa Misri kwenda kazini, huku ikitenga kiasi cha pauni milioni 250 kwa ajili ya kuboresha huduma hizo.
Tukio la “She Can”: Jukwaa la Kuwezesha Wanawake wa Misri Kitaaluma na Kuimarisha Nafasi Zao za Uongozi.
Wanawake wengi mashuhuri katika jamii ya Misri walishiriki katika toleo maalumu la tukio la “She Can” lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Amerika, katikati mwa Kairo. Tukio hili lina nafasi muhimu katika kusaidia maendeleo ya kitaaluma ya wanawake wa Misri kwa kuwapa zana na ujuzi muhimu ili kufanikisha malengo yao ya kikazi, kuwahimiza kupanua wigo wao katika nyanja mbalimbali, na kuimarisha mchango wao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Tukio hilo lilifanyika chini ya udhamini wa Wizara ya Vijana na Michezo, Wizara ya Mambo ya Kijamii, Wizara ya Mipango na Maendeleo ya Kiuchumi na Ushirikiano wa Kimataifa, Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo, na Baraza Kuu la Watu Wenye Ulemavu.
Miongoni mwa waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na:Dkt. Ghada Ali, Mbunge na Mjumbe wa Kikundi cha Kazi cha 2 katika Baraza la Mawaziri kuhusu Ujasiriamali, na Dkt. Iman Karim, Msimamizi Mkuu wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu, na Mbunge Hind Hazem, Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Kijamii katika Bunge, na Dkt. Dalia El-Baz, Mkuu wa Shirika la Posta la Misri, na Lamies Nagm, Mshauri wa Rais wa Mamlaka ya Usimamizi wa Masuala ya Fedha kuhusu Uwajibikaji wa Kijamii, na Dkt. Rasha Ragheb, Mkuu wa Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo
Masuala muhimu yaliyoshughulikiwa katika tukio hilo ni pamoja na:
• Hadithi za mafanikio ya watu wenye ulemavu katika soko la ajira
• Ushiriki wa wanawake katika sekta ya famasia inayohitaji uelewa mpana wa mifumo ya afya na elimu
• Umuhimu wa msaada wa serikali na bunge kwa ujasiriamali
• Nguvu ya mawasiliano na masoko katika kujenga uwepo wa wanawake katika soko la ajira
• Kuwezesha wanawake kupitia majukwaa ya kidijitali kama LinkedIn
• Nafasi ya taasisi za kitaifa katika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi
• Juhudi za kuleta uwiano kati ya kuwa mama na kufanikisha malengo ya kitaaluma
Mkutano wa Viongozi Wanawake wa Misri Wawatunuku Wanawake 50 Wenye Ushawishi Mkubwa kwa Mwaka 2022
Mkutano wa Viongozi Wanawake wa Misri katika toleo lake la pili ulitunuku wanawake 50 wenye ushawishi mkubwa zaidi katika taasisi za biashara kwa mwaka wa 2022, kupitia tuzo za kila mwaka zijulikanazo kama Top 50 Woman. Tuzo hizo zilitolewa na Dkt. Maya Morsi, Rais wa Baraza Kuu la Wanawake la Misri, Balozi Christian Berger, Balozi wa Umoja wa Ulaya mjini Cairo, pamoja na mtangazaji Dina Abdel Fattah, Rais wa Jukwaa la Wanawake 50 Wenye Ushawishi Mkubwa.
Tuzo za Top 50 Woman ni miongoni mwa tuzo kubwa na muhimu zaidi nchini Misri zinazotambua mafanikio ya wanawake katika sekta zote, kwa lengo la kuangazia mifano ya wanawake wanaoweza kutazama na kuunda mustakabali mpya licha ya mabadiliko ya kimataifa, na kuongoza kazi za taasisi, iwe serikalini au katika sekta binafsi.
Miongoni mwa waliotunukiwa walikuwa: Dkt. Jehan Saleh, mshauri wa kiuchumi wa Waziri Mkuu, na Dkt. Hoda Baraka, mshauri wa Waziri wa Mawasiliano kuhusu maendeleo ya ujuzi wa kiteknolojia na Profesa wa Uhandisi wa Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Kairo, na Balozi Muna Omar, aliyewahi kuwa Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje, na Hebatullah El-Sirfy, Naibu Rais wa Soko la Hisa la Misri, na Dkt. Nahla Sabry Kotb El-Saeedy, mshauri wa Imamu Mkuu wa Al-Azhar kuhusu masuala ya wanafunzi wa kimataifa, na Rana Badawy, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Misri anayehusika na maagizo ya udhibiti na Basel, na Dkt. Reem Bassiouney, Profesa na Mkuu wa Idara ya Isimu katika Chuo Kikuu cha Marekani, Kairo.
Orodha ya wanawake waliotunukiwa pia iliwajumuisha:
• Amal El-Sheikh, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya mafuta ya Shell Egypt,
• Dkt. Ola El-Khawaga, Profesa wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Cairo na mshauri mkuu wa mradi wa marekebisho ya uchumi unaofadhiliwa na USAID,
• Dkt. Eman Mansour, Mkuu wa Sera za Uwekezaji na Mkurugenzi wa Kituo cha Utatuzi wa Migogoro ya Wawekezaji katika Mamlaka ya Uwekezaji ya Taifa,
• Dkt. Nevine Abdel Monem Massad, Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Kairo,
• Suzanne Thabet, mchapishaji na mhariri mkuu wa jarida la Passion na mwanzilishi wa Shirika la Mitindo na Ubunifu la Misri,
• Dkt. Kawthar Mahmoud, Rais wa Baraza la Uuguzi la Kitaifa na Naibu wa Waziri wa Afya anayehusika na masuala ya uuguzi.
Pia, viongozi wengine wanawake walioweka historia katika nafasi nyeti za uongozi walipewa heshima zao.
Tamati na Muktadha wa Kidini kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake
Katika hitimisho, uwezeshaji wa wanawake unaendelea kuwa jiwe la msingi katika kufanikisha maendeleo endelevu na mabadiliko chanya duniani kote. Mwanamke si nusu ya jamii tu kwa idadi, bali pia ni mhimili wa maendeleo ya kiakili, kiuchumi na kijamii. Tajiriba ya kimataifa imedhihirisha kuwa kushirikisha wanawake katika nyanja za kazi, siasa, elimu, na sayansi kuna mchango mkubwa katika kuinua ubora wa maisha na kuongeza ubunifu na tija.
Katika Ukristo, Injili inatukuza nafasi ya mwanamke. Yesu Kristo alimpa mwanamke heshima ya juu, licha ya changamoto zilizokuwepo. Katika Waraka wa Paulo kwa Wagalatia 3:28 inasema: "Hakuna Myahudi wala Myunani, hakuna mtumwa wala mtu huru, hakuna mwanamume wala mwanamke, kwa maana nyote ni mmoja katika Kristo Yesu." Hii inaonesha usawa kamili mbele ya Mungu na kuchochea uwezeshaji wa wanawake. Katika Uyahudi, Torati inampa mwanamke hadhi kubwa. Katika Mithali 31:10-31 kuna sifa kwa mwanamke mwema anayeshiriki katika ujenzi wa familia na jamii: "Mwanamke mwema ni nani atakayempata? Maana thamani yake imeshinda marijani..." Hii ni heshima kwa mchango wa mwanamke katika kazi na uzalishaji.
Katika Uislamu, ambao ulikuwa wa mwanzo katika dini zilizoipa mwanamke heshima kamili, mwanamke alipewa haki na nafasi muhimu katika jamii wakati ambapo alidharauliwa na kunyimwa haki. Qur’an inasema: "Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake... Allah amewaandalia msamaha na thawabu kubwa." [Al-Ahzab: 35]. Aya hii inathibitisha usawa wa thamani ya mwanadamu na ujira wake, bila kujali jinsia. Kwa hiyo, wito wa kuendeleza uwezeshaji wa wanawake leo si kwenda kinyume na dini au tamaduni, bali ni mwendelezo wa misingi ya haki, huruma na utu iliyoasisiwa na Uislamu, Ukristo na Uyahudi – dini zinazotufundisha kuheshimu mwanamke, kumuunga mkono na kumjengea mazingira ya kuchangia kwa ufanisi katika maendeleo ya taifa.
Maendeleo ya baadaye hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa wanawake na wanaume, kwa misingi ya dini, haki na maendeleo jumuishi. Kumuwezesha mwanamke ni kuiwezesha jamii nzima – ni ujumbe wa kimaadili, kimaendeleo, na kidini unaopaswa kuchukuliwa kwa dhamira na moyo wa dhati.