KULALA HARUSI KUAMKA MSIBA

KULALA HARUSI KUAMKA MSIBA
Funzo la Utu na Huruma katika Jamii Yetu
KULALA HARUSI KUAMKA MSIBA

Makala ya Maadili na Utu katika Jamii ya Kiafrika

Imeandikwa na: Hussein B. Mwinshehe(Mfalme Wa Tungo Tata)

Katika jamii nyingi za Kiafrika, harusi ni tukio la furaha. Lakini je, furaha hiyo inaweza kufunika macho ya huruma na utu? Tukio la kusikitisha lililotokea kijijini kwetu ndilo lililonisukuma kuwaandikia makala hii yenye kichwa:
“Kulala Harusi, Kuamka Msiba.”
Usiwapuuze wahitaji kwa sababu ya shangwe.

Siku moja baada ya harusi ya kijana maarufu kijijini, mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Sengwira alifariki dunia. Sengwira alikuwa mlevi wa muda mrefu, lakini pia alikuwa mjomba wa bwana harusi. Kwa siku kadhaa alikuwa ameugua, lakini hakupata msaada wa matibabu. Familia yake ilishughulika zaidi na maandalizi ya harusi, wakiliona tatizo lake la kiafya kama usumbufu usio na maana kubwa.
Kifo chake kilizua maswali na manung’uniko miongoni mwa wanakijiji. Wengine walilalamika kuwa familia ilimpuuza kwa sababu ya sherehe, wakisema:
• “Kama angekuwa mama yake mzazi bwana harusi, je, wasingetoa pesa kumpeleka hospitalini?”
• “Au wangepiga ngoma huku mjomba akihangaika na roho?”

Maneno ya kijijini yalizua hofu ya laana. Baadhi walidai kuwa Sengwira alikufa na kinyongo, na kwamba ndoa ya mpwa wake haitadumu. Walinukuu methali ya kale isemayo:
“Nyumba inayokesha harusi haifai kuamkia msiba.”
Niliposikia simulizi hilo nilitafakari sana. Nikiwa mtunzi na mwandishi wa vitabu, niliona kuna haja ya kulitazama kisa hiki kwa mtazamo wa kifasihi na kimaadili.

Tazama hali ile: wakati dada mtu akicheza kwa furaha kushuhudia kijana wake anaoa, kaka yake — yaani Sengwira — anahaha kupambana na uhai! Fikiria maumivu aliyopitia mgonjwa ambaye, nyakati za uzima wake, alimpenda sana mpwa wake.
Ndiyo, huo ulikuwa usiku wa mwisho wa Sengwira.
Gumzo likawa kubwa katika mazishi yake. Wengi walishangaa jinsi ilivyowezekana nyumba iliyokuwa na shamrashamra na vifijo iwe pia ndani yake na mgonjwa anayetapa roho tena mtu muhimu wa familia. Je, kwa sababu tu alitazamwa kama mlevi ndiyo maana alipuuzwa? Na mbona hata dada yake naye alikuwa mlevi, lakini hakupuuzwa? Mbona bwana harusi hakukumbuka fadhila za mjomba wake aliyemlea na kumsaidia nyakati nyingi za shida?

Asubuhi ya msiba ilipofika, machozi ya aibu yalitawala. Lakini baada ya mazishi, mikosi ikaanza katika ndoa ya bwana harusi. Biashara yake haikukua, mke wake akaanza kuugua mara kwa mara, na ndoto zake zikaanza kufifia. Miaka mitatu ikapita bila mtoto, na dhiki haikuisha.
Bwana harusi alianza kutafakari. Ndoto za ajabu zikamjia, zikimrudisha kumbukumbu za mjomba wake: jinsi alivyomsimamia jandoni, kumpa nasaha, na hata alipokuwa amelewa kumpa pesa ili akale.
Alikumbuka maneno ya mwisho ya Sengwira kabla hajazidiwa:
“Mjomba, hivi kweli unaweza kuniacha nice ili ukaoe? Naumwa mjomba! Napenda nami nifurahie harusi yako, lakini usiwe siku ya msiba wangu.”
Ndoto hiyo ilimfanya bwana harusi atokwe na machozi na atafakari zaidi juu ya maisha yake.

Hatimaye aliamua kumwendea Mzee Tungo Tata, mzee wa hekima kijijini. Mzee akamshauri afanye tambiko la toba. Watani walikusanyika, sadaka zikatolewa, na bwana harusi akaomba msamaha kwa roho ya mjomba wake. Baada ya hapo maisha yake yakaanza kubadilika. Akamuota tena mjomba wake katika ndoto, safari hii akimwambia kwa furaha:
“Mjomba, wema wa mtu upo moyoni mwake  haijalishi awe mlevi au chizi. Nimekusamehe mjomba.”
Ndoto hiyo ilimfanya atokwe na machozi ya furaha. Kuanzia hapo, afya ya mke wake ikaimarika, biashara ikafufuka, na hatimaye mkewe akashika mimba.

Kisa hiki cha Sengwira kimeacha funzo kubwa:
• Utu hauchagui hali ya mtu. Hata mlevi ana historia, heshima, na haki ya kuangaliwa kwa jicho la huruma.
• Sherehe haipaswi kufunika majukumu ya kifamilia. Furaha ya harusi si kisingizio cha kupuuza wagonjwa au wahitaji.
• Majuto huja baadaye, lakini tambiko la toba huweza kurejesha amani ya roho. Jamii inapaswa kuenzi mila za kuomba radhi na kuondoa kinyongo.

Methali ya kale, niliyoifanyia upya, itusihi kila mara tukumbuke kuwa:
“Nyumba inayokesha harusi haifai kuamkia msiba.”