KISWAHILI NA AFRIKA

Imeandikwa na: William Devis Mbakwa
1.0 UTANGULIZI
Kiswahili ni moja kati ya lugha maarufu itumikayo katika maeneo ya Afrika Mashariki yenye mkusanyiko wa nchi mbalimbali kama vile Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na kadhalika kwa uchache. Afrika ni bara la pili kwa ukubwa wa kilomita za mraba 30,221,532, lenye idadi ya watu zaidi ya bilioni 3.1. Kwa sasa bara hili lina nchi zisizopungua 56. (African Journals)
KWANINI KISWAHILI NA AFRIKA?
Katika makala hii fupi itaangazia mahusiano yaliyopo baina ya maeneo mbalimbali ya Afrika katika kuhusiana (interaction) na matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa upana wake.
2.0 LENZI YA KISWAHILI AFRIKA
Ni ukweli usiopingika kuwa Afrika ina lugha zaidi ya 2000 ambazo zinazungumzwa na makabila mbalimbali yenye mkusanyiko wa mila, desturi na tamaduni za kipekee. Katika jumla ya lugha zote Afrika yaani Afrika Mashariki, Magharibi, Kusini, Kaskazini, na Afrika ya Kati kwa ujumla wake zimetawaliwa na lugha ya Kiswahili ambayo ina zaidi ya wazungumzaji milioni mia mbili. Kwa sababu hiyo, Afrika inatawaliwa na lugha zenye asili ya Kibantu kwa ukubwa wake zinazochukua robo tatu ya Afrika katika nchi mbalimbali. Hii inaakisi kuwa Afrika na lugha ya Kiswahili haviwezi kutengana.
3.0 JICHO PEVU LA UMOJA AFRIKA
Kutokana na ukubwa wa maeneo mengi ya Afrika kuwa na idadi ya wazungumzaji, hii inaonyesha kuwa Kiswahili ni moja kati ya viunganishi vya umoja, mshikamano na ushirikiano wa nchi mbalimbali, zikiongozwa na nchi vinara yaani Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya na Uganda) katika kutanua wigo mpana wa ushirika unaolenga kuleta maendeleo Afrika. Yaani ile ndoto ya Nkwame Nkrumah "Africa must Unite" na ile ndoto ya Muammar Gaddafi "United States of Africa" ichukue nafasi. Inahitaji lugha moja katika kukamilisha mazungumzo, na lugha hiyo ni Kiswahili. Hii, kwa ukubwa wake, itakamilisha ndoto zetu zinazolenga Afrika kwanza katika kuinua uchumi wa nchi mbalimbali zenye rasilimali za kutosha kuifanya Afrika kuwa namba moja duniani.
4.0 HITIMISHO LA MTU MWEUSI NA KISWAHILI
Kiswahili na Afrika, katika kurahisisha mawasiliano kupitia nchi mbalimbali, vinahitaji vitu vifuatavyo:
• Utayari na uthubutu wa nchi zote Afrika katika kuridhia lugha ya mawasiliano ambayo ni Kiswahili.
• Utawala bora wenye kutengeneza amani na mshikamano.
• Matumizi sahihi ya teknolojia yenye kuiweka Afrika wazi kupitia lugha ya Kiswahili.
• Siasa safi kwa Waafrika yenye dhana ya uzalendo wa Mwafrika kwanza.
• Elimu jumuishi ya Mwafrika na asili yake yenye kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa wasomi nchini ili kuondoa dhana potofu ya lugha yetu adhimu.
Kwa pamoja tunaweza kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa chanzo na chachu ya maendeleo Afrika, kama tukikubali yale ya umoja na mshikamano kwa nchi zote Afrika katika matumizi ya njia hii kama mawasiliano tosha yenye uzalendo wa asili yetu Afrika.
MUNGU ibariki Afrika, MUNGU ibariki lugha yetu ya Kiswahili, MUNGU wabariki Waafrika, MUNGU wabariki viongozi wetu.