AKILI ASILIA: UKWELI NDANI YA AFRIKA

Imeandikwa na: William Devis Mbakwa
1.0 UTANGULIZI
Akili asilia ni utafiti yakinifu uliochukua taswira ya Bara la Afrika katika upembuzi wa masuala ya mienendo na mtindo wa maisha kwa Mwafrika kabla na baada ya ujio wa walowezi, yaani wazungu, Waarabu, na wa Asiya watu wa Mashariki ya Mbali. Makala hii, iliyoundwa na Mwafrika halisi ndani ya Bara tajiri duniani, imeangazia maeneo tofauti, ikiitazama Afrika kama Bara Mama katika dhana ya maendeleo duniani. Hebu tusonge kwa undani wa habari na mtiririko wa historia.
2.0 MAARIFA YALIYOFICHWA
Kutokana na Waafrika kupandikiziwa dhana mbalimbali potofu, hali hiyo imekuwa na athari kubwa sana kwa jamii ya Waafrika. Utamaduni, lugha, na dini, kama miongoni mwa dhana alizopandikiziwa Mwafrika, zimedhihirisha athari mbalimbali, yaani kiuchumi, kijamii, kisiasa, kitamaduni, na pia kimtazamo (Malugu, A., 2019).
Historia ya Bara la Afrika imebeba sura mbili zinazokinzana, yaani:
• (a) Mtazamo wa Kimagharibi (Euro-centric view)
• (b) Mtazamo wa Ndani ya Afrika (Afro-centric view)
Katika kujinasibu kifikra na kimtazamo, Afrika imekumbwa na wimbi kubwa la kutawaliwa, na mtazamo hasi wa Kimagharibi hapa umechukua mawazo ya wazungu kama vile George Hegel, Profesa Hughs, Henry Stanley, Rosa Luxemburg, na kadhalika, ambao wote kwa pamoja wanaamini Afrika kama eneo lililokuwa na kiza kinene, kwani wanaamini kuwa Afrika ilikuwa haijastaarabika katika matendo.
Kwa mfano, Henry Stanley anasema katika machapisho yake kuwa: "Afrika haikuwa na ustaarabu wa aina yeyote kwani aliwakuta Waafrika wanashea maji na wanyama, wanaoga uchi bila kujali uwepo wa mama na dada zao. Waafrika walikuwa na kiu ya damu (bloodthirsty) kwani waliuwana wao kwa wao." Dhana hii ya Stanley inaonyesha jinsi ambavyo Afrika ilichukuliwa vibaya na ni udhaifu wa kielimu juu ya asili ya Afrika, kwani kipindi alichoingia Stanley, maeneo ya Afrika ya Kusini yalikuwa katika kipindi cha Vita za Mfecane (Mfecane wars) miaka ya 1820s. Hivyo, mtazamo wake hauna ukweli wowote wa Afrika kama eneo lililokuwa haijastaarabika.
3.0 UKWELI MTUPU
Mtazamo wa Ndani ya Afrika (Afro-centric view), unaosapotiwa na wataalamu mbalimbali kama vile Walter Rodney, Frantz Fanon, Samir Amin, na kadhalika, unaonyesha jitihada za wazi katika Bara la Afrika kimaendeleo. Kwa mfano, Walter Rodney katika kitabu chake maarufu "How Europe Underdeveloped Africa" anasema kabla ya kuja kwa walowezi, Afrika ilikuwa na maendeleo yanayoshabihiana na Ulaya mpaka karne ya 15, ambapo utengano wa kimaendeleo ulianza hapo.
Kwa mfano, suala la elimu Afrika lilikuwepo kabla ya ujio wa walowezi. Ushahidi unaonesha kupitia uwepo wa Chuo Kikuu cha Fez (Fez University in Morocco), kilichohusika katika kutoa elimu rasmi (formal education) kwa Waafrika. Uwepo wa teknolojia ya ujenzi wa miundombinu unaonekana Afrika kupitia Piramidi za Misri, Nubia, Ethiopia, na kadhalika, ambazo kimsingi hadi leo wazungu wanakuna vichwa kwa elimu hii kubwa katika uhandisi wa majengo yale marefu duniani.
Uwepo wa falme za Kiafrika zenye nguvu na tajiri, kama Falme ya Mali (Mali Empire), iliyokuwa na utajiri mkubwa chini ya mtawala maarufu Mansa Kankan Musa, anaekadiriwa kuwa kama angekuwa hai, utajiri wake ungekuwa zaidi ya Dola Bilioni 400 (Forbes Africa, Feb 2015). Haya yote ni makadirio yanayoonyesha jinsi gani Afrika ilivyo na utajiri wa kutosha. Hivyo basi, pamoja na yote hayo, ukweli unabaki: Afrika ni sehemu ya historia ya dunia katika kutoa mwanga, wala sio kuiweka Afrika kama Bara Jeusi (Dark Continent), na mitazamo hasi juu ya kutokuwepo kwa historia ya Afrika (kama ilivoripotiwa na Profesa Hughs na George Hegel, wasioamini historia ya Afrika kwa kigezo cha kukosekana kwa taarifa za njia ya kimaandishi).
Hebu fikiria, kama Afrika ingebaki kujitawala, je, umasikini na dhana potofu ya kimaendeleo ingeendelea kubaki? Hebu tazama ujio wa Uislamu na Ukristo Afrika; umeleta mpasuko na mchango kiasi gani katika maendeleo? Hebu jiulize babu zetu na bibi zetu waliishije katika imani walizokuwa nazo?
4.0 IMANI NDANI MWA AFRIKA
Afrika imegawanyika katika pande kuu mbili, ambazo ni kundi la wafuasi wa dini ya Kikristo na Kiislamu. Hali hii imeleta mpasuko katika dhana ya kujenga Afrika yenye upendo na mshikamano halisi, yaani machafuko yamekuwa sehemu ya kuua undugu wetu sisi Waafrika. Mfano ni machafuko yaliyotokea Burkina Faso wakati mapadre wanauliwa na waasi wanaoshukiwa kuwa Waislamu. Sisi Waafrika wenyewe tunauwana kisa dini ambazo zililetwa na walowezi (Vatican News, 2019): "Mashambulizi ya kigaidi yanazidi kuongezeka na kuwauwa mapadre, kutekwa nyara wakristo, na wakati huo huo hata makanisa kuharibiwa na kuchomwa moto. Kesi hii imejitokeza nchini Burkina Faso wakati wa kuadhimisha misa Takatifu tarehe 12 Mei 2019."
Hali hii ni ya kukemewa kwa nguvu zote kwani haipaswi kuwa na utengano juu ya dini ambazo kiasili sio chanzo chetu Waafrika. Turejee tulikotoka sisi katika imani zetu za kuamini katika mito, miti, milima, na kadhalika. (Hapa tuelewane, sisizungumzi kwa habari ya kuamini miungu, la hasha!) Katika kuamini vitu hivyo, babu na bibi zetu walikuwa wakitumia kama sehemu ya makutano. Hebu tazama leo hii: waumini hukutana kanisani na misikitini. Hivyo, neno imani ni silaha tosha kwetu Waafrika. Tunaishi katika dhana ile ile ya upendo na ujamaa usiyotahayari. Katika machafuko ya aina yoyote, kwa pamoja tunaweza kurudi katika asili yetu ya kale ili kuondoa ukinzani uliopo kati yetu, kwani sote tunaamini katika Baba Mmoja (MUNGU).
5.0 HITIMISHO MAMA
Tukianzia tulikotoka, asili asilia ya Mwafrika si Uislamu wala Ukristo. Hivyo basi, yatupasa kuondoa tofauti zetu hizi zinazokwamisha maendeleo yetu. Sisi kama Waafrika halisi, mfano, hakuna maana ya kushikilia dini na kunyoosheana vidole katika maana ya yupi ni bora, nani sio bora. Haina maana kabisa. Wewe Mwafrika mwenzangu, amka sasa na tubaki na neno imani kama msingi wa kila kitu. Dini si lolote wala chochote; ni makutano tu yakutuunganisha na Mwenyezi Mungu.
Dhana ya Mwafrika kutazamwa kama mshamba na asiestaarabika haitakiwi ichukue nafasi katika maisha yetu hii. Itaendana sambamba na matumizi sahihi ya mfumo wa kielimu katika kukuza na kutangaza tamaduni zote na asili ya Mwafrika kwa kila eneo la nchi aliyopo, ili kukuza kizazi chenye kuelewa lugha mama za Afrika. Kwa mfano, lugha ya Kiswahili itumike kama alama na lugha ya mawasiliano kwa watu wote. Hii itaondoa lugha tawalishi ambayo ni Kiingereza. Yatupasa kusifu lugha zetu mama na kuamini kuwa kabla ya ujio wa walowezi, Afrika ilikuwa na maendeleo, na chanzo cha matatizo yote Afrika ni wakoloni pamoja na sababu za ndani ya Afrika zenye urithi kutoka kwenye ukoloni (Ngugi wa Thiong’o, Decolonizing the Mind, 1986).
"Afrika na Kiswahili urithi bora kwa vizazi vya sasa na baadae."
Mama wa maendeleo, Afrika ndie jawabu la mafanikio.
Marejeleo
• Berg, L. B. (2001) Qualitative Research Methods for the Social Sciences (4th ed.). Boston and London: Allyn and Bacon.
• Bible Society of Tanzania, (1997) Biblia Maandiko Matakatifu, Mwanzo. Dodoma: Bible Society of Tanzania.
• Hegel, G. F. (1956) The Philosophy of History. New York: Dover Publications.
• Iribemwangi, P. I., na Mukhwana, A. (2011) Isimu Jamii. Nairobi: Focus Publishers Ltd.
• Kezilahabi, E. (1990) Nagona. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
• Malugu, A. (2015) "Nafasi ya Fasihi katika Kusawiri Suala la Dini" katika Kiswahili, Juz. 79. Dar es Salaam: TATAKI.
• Malugu, A. (2019) "Motifu za Dhana Potofu kuhusu Afrika na Mwafrika: Mifano kutoka Riwaya ya Njama (A. E. Musiba) na Tutarudi na Roho Zetu? (Ben R. Mtobwa)." Lugha na Fasihi katika Mshikamano wa Kitaifa na Uwiano Barani Afrika. Eldoret: Moi.
• Malugu, A. (2021) "Istiara katika Riwaya ya Kusadikika ya Shaabani Robert." Mwanga wa Lugha.
• Meinhof, C. (1915) An Introduction to the Study of African Languages. London.