Saa ya Sifuri

Saa ya Sifuri

Imeandikwa na: Esraa El-Fauomy

Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Katika kipindi cha kuondokana na ukoloni, wakati wa mabadiliko makubwa katika historia ya Misri ya kisasa, kipindi hiki kilihamisha Misri kutoka katika utawala wa kifalme hadi jamhuri. Ni mapinduzi ya ushindi wa wakulima na mapinduzi ya kurudisha haki kwa Wamisri, mapinduzi yaliyotayarisha njia kwa enzi mpya mbali na ufalme, ujamaa, na ufisadi.

Mapinduzi yalianza alfajiri ya tarehe Julai 23, 1952 chini ya uongozi wa Gamal Abdel Nasser na Luteni Jenerali Mohamed Naguib. Mapinduzi haya yaliitwa Harakati ya Maafisa Huru. Harakati hii ilianza na majadiliano na mikutano katika nyumba za baadhi ya maafisa na hii ndiyo ilikuwa mwanzo wa Harakati ya Maafisa Huru. Maafisa hao waliweka kiapo cha usiri mkubwa. Mapinduzi haya yalibuka ili kuonesha hasira ya maafisa hawa dhidi ya utawala wa kifalme na ufisadi uliokuwa umeenea nchini chini ya utawala wa Mfalme Farouk wa Kwanza.

Maafisa hao hawakukasirika tu na utawala wa kifalme bali walichukia pia ukoloni wa Uingereza  uliokuwa ukichuma damu ya Wamisri. Ufalme na ukoloni viliungana ili kuwakandamiza wakulima, wafanyabiashara, na wafanyakazi hadi vikawaathiri watu wengi. Mapinduzi yalianza kwa Maafisa Huru kudhibiti maeneo muhimu ya Kairo hadi pale Sadat alipotangaza kupitia redio kuwa wamechukua madaraka nchini na kwamba Baraza la Uongozi la Mapinduzi ndilo litakaloongoza nchi.

Enzi mpya ilianza baada ya Maafisa Huru kuchukua madaraka. Baada ya hapo, Mfalme Farouk alijiuzulu na hivyo utawala wa kifalme ukaisha na utawala wa jamhuri ukaanza. Luteni Jenerali Mohamed Naguib akawa rais wa kwanza wa jamhuri. Tangu mwanzo wa mabadiliko haya, kulikuwa na mafanikio makubwa yaliyoathiri Misri na nchi nyingi za Kiarabu zilizokuwa zimekoloniwa na zilizotafuta uhuru kama Misri. Mapinduzi haya yalisaidia harakati za uhuru katika nchi nyingi za Kiarabu.

Hali ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa ilibadilika. Utawala wa ujamaa ukaisha na sheria ya kwanza ya mageuzi ya kilimo ikatangazwa. Udhibiti wa wageni katika viwanda na biashara ukaisha na elimu ikawa bure. Hivyo, mapinduzi yakamaliza udhibiti wa mtaji. Tusiisahau mkataba wa kuondoka kwa Waingereza uliokomboa Wamisri kutoka kwa utegemezi wa wageni pamoja na harakati za uhuru ambazo zilikuwa na jukumu kubwa la kisiasa na la kimataifa. Matokeo ya mafanikio haya yote yalikuwa ni kuongezeka kwa mvutano na nchi za kikoloni kama Uingereza, Ufaransa, na Israeli, na hivyo kupelekea uvamizi wa nchi tatu dhidi ya Misri.

Mapinduzi ya Julai 23 hayakuwa mabadiliko ya kisiasa tu bali yalikuwa mwanzo wa enzi mpya ya mabadiliko makubwa katika historia ya Misri, inayoonesha uhuru, maendeleo, na ujenzi.