Iman Al-Warraqi... Sauti ya Ukweli Dhidi ya Itikadi Kali
Imetafsiriwa na: Mohamed Yahya
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika njia ngumu za uandishi wa habari, ambapo wanaosalia ni wale tu wenye shauku na azma thabiti, ameng’aa mwandishi wa habari wa Kimasri Iman Al-Warraqi kama moja ya nyota mashuhuri katika anga ya uandishi wa uchunguzi, baada ya safari ya kitaaluma aliyoichora kwa ujasiri, bidii na mafanikio mfululizo.
Iman alihitimu kutoka Chuo cha Habari, Chuo Kikuu cha Kairo, na kuanza safari yake ya kitaaluma mnamo mwaka 2007, akihama kati ya taasisi kuu za habari za Misri kama vile Al-Dustour, Al-Karama, Al-Sabah, Youm7, na tovuti ya Aswat Masriya chini ya shirika la Reuters. Hata hivyo, hakubakia kuwa mwandishi wa habari anayeandika tu taarifa, bali alikuwa mtafutaji wa ukweli katika undani wa maelezo, akiandika kwa kalamu isiyoogopa makabiliano.
Iman alijitofautisha kwa uchunguzi uliopata mwangwi mpana, ukiwemo kampeni yake maarufu kuhusu mitaala ya Al-Azhar na walimu waliokuwa na uhusiano na makundi yenye misimamo mikali. Kazi hiyo ilichochea mjadala mkubwa wa kijamii kuhusu mageuzi ya hotuba ya kidini, na ikavutiwa hadi ngazi za juu za serikali, hali iliyosababisha Sheikh wa Al-Azhar kuunda kamati ya kupitia mitaala na kuwawajibisha waliohusika.
Alifanya kazi pia kama mtangazaji wa kipindi “Azimat Misr” kwenye kituo cha televisheni Youm7, na akatoa taarifa mbalimbali kwa ujasiri wa kitaaluma wa hali ya juu, hali iliyomfanya apate heshima na kuthaminiwa na taasisi za habari pamoja na wenzake.
Shauku yake kwa uandishi wa habari haikubakia tu ndani ya taaluma, bali ilienea pia katika kuendeleza tasnia ya habari kutoka ndani. Alizindua mpango “Mapinduzi ya Akili Bandia”, mpango wa kwanza wa Kimasri unaolenga kuwafundisha waandishi wa habari matumizi ya zana za akili bandia na kuziunganisha katika kazi za kihabari, ili kuendana na mageuzi ya kidijitali yanayoendelea kwa kasi.
Iman Al-Warraqi alipokea tuzo nyingi, zikiwemo Tuzo ya Uandishi wa Habari wa Kiarabu, Tuzo ya Ihsan Abdel Quddous kwa ubora wa uandishi, Tuzo ya Siemens, pamoja na tuzo kadhaa kutoka Chama cha Waandishi wa Habari wa Misri, jambo linaloonyesha imani ya jamii ya kihabari katika nafasi yake na uaminifu wake.
Kwa sasa anaandika kitabu kinachochambua upya maandiko ya kidini kwa mtazamo wa kimaudhui usiofungwa na misimamo ya kiitikadi, huku akiendelea kuchapisha makala na uchunguzi wenye ushawishi katika tovuti Jusoor Post, ambapo anazungumzia masuala kama vile akili bandia, mabadiliko ya tabianchi na misimamo mikali kwa mtazamo wa uchambuzi wa kina.
Kwa ujuzi wa lugha wa hali ya juu na ustadi katika utafiti na uchambuzi, Iman Al-Warraqi ni mfano wa kuigwa wa mwandishi wa habari mtafutaji wa ukweli, katika zama zilizojaa sauti zinazochanganyika.