Yara Odeh... Sauti ya Uongozi wa Vijana katika Uwanja wa Kimataifa wa Amani na Maendeleo
Imetafsiriwa na: Sandy Hany Labib
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Bi. Yara Odeh ni mtaalamu anayechipua kama kiongozi katika masuala ya vijana, amani na usalama, akiwa na mchango mkubwa katika diplomasia ya kibinadamu na maendeleo ya kimataifa. Kwa sasa anahudumu kama Afisa wa Programu ya Vijana, Amani na Usalama katika Kituo cha Kimataifa cha Kairo cha Utatuzi wa Migogoro, Amani na Ujenzi wa Amani (CCCPA) cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, ambapo anaongoza juhudi za kuunganisha ajenda ya vijana na mifumo ya kikanda katika programu za usuluhishi na ujenzi wa amani.
Mbali na jukumu hilo, Yara ndiye msimamizi wa Mazungumzo ya Vijana ya Jukwaa la Aswan la Amani na Maendeleo Endelevu, na mara kwa mara huiwakilisha Misri katika majukwaa ya kimataifa kuhusu vijana na usalama.
Safari yake ya kitaaluma imempa nafasi nyingi za kimataifa. Amewahi kuchaguliwa katika mtandao wa vijana wa Afrika Wise Youth Network wa Umoja wa Afrika (2024–2027), na kuorodheshwa miongoni mwa “Vijana kwa Ajili ya Amani” wa AU. Pia alihudumu kama Regional Focal Point wa Umoja wa Mataifa, akiwakilisha kundi la SDG 16 katika mikutano ya vijana ya Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ambapo mwaka 2023 aliwasilisha hotuba mbele ya Mkutano Mkuu kuhusu tathmini ya hiari ya Saudi Arabia katika High-Level Political Forum.
Kabla ya hapo, alihudumu katika Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) akihusiana na diplomasia ya kibinadamu barani Afrika na Mashariki ya Kati. Pia alifanya kazi katika Wizara ya Mipango na Maendeleo ya Uchumi ya Misri, akiratibu uratibu wa kijamii na kiuchumi wa mpango wa urais “Haya Karima”, akisaidia kukuza ushirikiano na Benki ya Dunia na IMF ili kupunguza umasikini wa vipengele vingi kulingana na Dira ya Misri 2030.
Katika ngazi ya kikanda, Yara alihudumu kama Afisa wa Kiufundi wa Tume ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, akihusika na sera za maendeleo ya vijana ndani ya Ajenda 2063, na akawa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa mpango wa Silence the Guns.
Kielimu, Yara ana Shahada ya Uchumi na Sayansi ya Kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Kairo, alipata uzoefu wa ubadilishanaji wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Amsterdam kuhusu sera za umma na dini, ana stashahada ya masomo ya kidiplomasia, na kwa sasa anasomea Uzamili wa Utawala wa Biashara (MBA) katika Chuo cha Kiarabu cha Sayansi, Teknolojia na Usafirishaji Baharini.