Mshauri Mahmoud Fawzy... Akili ya kisheria inayosindikiza taifa katika safari zake
Imetafsiriwa na: Faris Ahmed Kamal
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Mshauri Mahmoud Fawzy anachukuliwa kuwa miongoni mwa akili kubwa za kisheria nchini Misri katika miongo miwili iliyopita, kutokana na uzoefu wake mpana na hadhi yake katika nyanja za mahakama, sheria, vyombo vya habari na siasa.
Alhitimu kutoka Chuo cha Sheria mnamo mwaka 2000 akiwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza wa darasa lake, kisha akapata Shahada ya Uzamili katika sheria binafsi na za umma, na baadaye Shahada ya Uzamili ya kimataifa katika sheria linganishi kutoka Chuo Kikuu cha Indiana, Marekani mnamo mwaka 2009, jambo lililompa nafasi ya kuchanganya elimu ya kisheria ya Kimasri na uzoefu wa kimataifa.
Fawzy alianza safari yake katika Baraza la Serikali, akipanda ngazi katika vitengo vyake vyote: mahakama, sheria, ushauri na ukaguzi wa mahakama, hadi kufikia nafasi ya Makamu wa Rais wa Baraza hilo. Pamoja na kazi yake ya kisheria, aliwahi kuwa mshauri wa kisheria wa mawaziri kadhaa, kuanzia Uwekezaji, Ushirikiano wa Kimataifa, Biashara na Viwanda, Fedha, na Haki ya Mpito, vilevile mshauri wa Bunge katika nyakati nyeti.
Imani ya serikali kwa uwezo wa Fawzy ilidhihirika zaidi alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Bunge (2019–2021), baada ya kushika nafasi ya mshauri wa kisheria wa Spika wa Bunge tangu mwaka 2016. Alishiriki kwa kiwango kikubwa katika kuandaa kanuni za ndani za bunge, na aliongoza kamati muhimu kama ile ya Maadili na Katiba. Pia aliendesha kitengo cha utafiti kilichosaidia Kamati ya Kupambana na Ugaidi ya Umoja wa Mabunge Duniani, akiwa mtaalamu katika masuala ya misimamo mikali.
Baada ya kuondoka bungeni, Mshauri Mahmoud Fawzy alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Kudhibiti Vyombo vya Habari (2021–2023), kisha akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa sekretarieti ya mazungumzo ya kitaifa na mjumbe wa bodi yake ya wadhamini, katika kipindi cha kihistoria ambacho kilishuhudia mazungumzo mapana ya kijamii na kisiasa nchini Misri.
Mnamo mwaka 2023, Fawzy aliacha kwa hiari nyadhifa zake za kisheria na za usimamizi ili kujitolea kuongoza kampeni ya uchaguzi ya Rais Abdel Fattah El-Sisi, ambapo alikuwa Mwenyekiti wa kampeni na mshauri wake wa kisheria, pamoja na msemaji rasmi wa kampeni hiyo. Jukumu hili liliweka wazi nafasi yake muhimu katika siasa za Misri. Mnamo mwaka 2024, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo.
Mchango wa Fawzy haukujitokeza tu ndani ya taasisi, bali pia katika uandishi wa katiba na sheria. Alikuwa mjumbe wa sekretarieti ya kamati ya watu kumi waliotayarisha rasimu ya Katiba ya 2014, na pia alishiriki katika majadiliano ya marekebisho ya katiba ya mwaka 2019. Alijiunga na kamati zilizotunga sheria za haki za kisiasa, uchaguzi, na mgawanyo wa majimbo, na alikuwa msemaji rasmi wa kamati hizo.
Fawzy ana uzoefu mkubwa katika usuluhishi wa kimataifa, akiwa ameorodheshwa miongoni mwa wasuluhishi wa kimataifa wa Kituo cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) cha Benki ya Dunia. Pia alishiriki katika usuluhishi wa migogoro mikubwa ya kibiashara. Aidha, aliongoza sekretarieti ya kamati kuu ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, na alichangia pakubwa katika masuala ya uwekezaji.
Fawzy pia aliwakilisha Misri katika majukwaa ya kimataifa kadhaa, muhimu zaidi ikiwa mikutano ya Umoja wa Mabunge Duniani na shughuli za kupambana na ugaidi huko Geneva na Belgrade. Aliwahi kuongoza ujumbe wa juu wa bunge katika mikutano ya kikanda muhimu, jambo lililompa nafasi kubwa ya kimataifa inayoonyesha kiwango cha imani alichopewa.
Kwa safari hii ndefu na yenye upeo mpana, mshauri Mahmoud Fawzy anabaki kuwa mfano wa akili ya kisheria inayochanganya usahihi na utulivu, kati ya uwepo wenye ushawishi na kazi kimya kimya nyuma ya pazia. Aliisindikiza serikali ya Misri katika nyakati nyeti, na aliacha mchango dhahiri katika masuala ya sheria, vyombo vya habari na siasa, akithibitisha kwamba uwezo na kujitolea ndivyo msingi wa imani na mwendelezo.