Misri... Mshirika Mkuu katika Mfumo wa Kimataifa wa Kulinda Amani

Misri... Mshirika Mkuu katika Mfumo wa Kimataifa wa Kulinda Amani

Imetafsiriwa na: Zainab Ibrahim Abdelrazik
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Misri inathibitisha kila siku nafasi yake kama mhimili mkuu katika kulinda usalama na amani ya kimataifa. Ushiriki wake wenye ushawishi na ufanisi katika misheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, pamoja na uzoefu wake wa kipekee katika kuandaa vikosi kushiriki katika majukumu hayo ya heshima, unathibitisha hili.

Ushiriki wa Misri katika operesheni za kulinda amani ulianza mnamo mwaka 1960 kupitia misheni ya Umoja wa Mataifa nchini Congo. Tangu wakati huo, Misri imeendelea kushiriki katika zaidi ya misheni 37 duniani kote, na zaidi ya wanajeshi na maafisa 30,000 wa Kimasri walihusika katika majukumu yaliyotanda kutoka Afrika na Asia hadi Amerika ya Kusini na Ulaya.

Leo, Misri ni miongoni mwa nchi kumi bora zinazochangia vikosi katika misheni za ulinzi wa amani duniani, ya kwanza kati ya nchi za Kiarabu, na ya tatu kati ya nchi za Francophone, ikiwa na jumla ya takriban watu 3,000 wanaofanya kazi katika misheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa, hasa barani Afrika.

Ushiriki huu haukuwa wa namba tu, bali pia uliambatana na dhabihu kubwa. Misri imepoteza mashahidi 28 miongoni mwa watoto wake wakati wa kushiriki katika misheni hiyo, ikithibitisha tena kujitolea kwa taifa la Misri kwa thamani za kibinadamu na kazi ya pamoja ya kimataifa.

Mchango wa Misri haukukomea katika msaada wa kijeshi na polisi pekee, bali ulijumuisha pia juhudi muhimu za kitaasisi na kisiasa. Mnamo mwezi Septemba 2018, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulikubali azimio lenye kichwa “Unyonyaji na Ukatili wa Kijinsia: Utekelezaji wa Sera ya Kutokuwa na Uvumilivu”, linalolenga kulinda jamii zilizoathiriwa na ukiukwaji ndani ya misheni za kulinda amani.

Aidha, Rais Abdel Fattah El-Sisi alijiunga mnamo mwaka 2017 na mpango wa Umoja wa Mataifa uitwao “Circle of Leaders” unaolenga kuimarisha kujitolea kimaadili katika majukumu haya ya kimataifa. Mnamo mwezi Februari 2021, Umoja wa Mataifa uliichagua tena Misri kama mwandishi wa Kamati Maalum ya Operesheni za Ulinzi wa Amani, jambo linaloonyesha wazi heshima ya kimataifa kwa jukumu la Kairo katika kukuza dhana na sera za kulinda amani, na kuimarisha mahusiano kati ya juhudi za ulinzi na ujenzi, kanuni zilizoelezwa katika “Ramani ya Njia ya Kairo” katika uwanja huu muhimu.

Nafasi ya Misri imepata sifa mara kwa mara kutoka kwa maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa. Mnamo mwezi Mei 2023, wakati wa maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa operesheni za kulinda amani, Umoja wa Mataifa uliitunuku Misri kama mojawapo ya nchi zinazochangia zaidi katika kulinda amani na usalama wa kimataifa. Pia, “Elena Panova”, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Misri, alionyesha shukrani zake akisema: “Daima Misri imekuwa mshirika muhimu katika njia ya kuelekea amani ya kudumu... Tunaheshimu ujasiri na kujitolea kwa walinzi wa amani wa Kimasri.”

Mnamo mwezi Julai 2019, Polisi wa Umoja wa Mataifa walipongeza ubora wa vikosi vya Kimasri miongoni mwa wachangiaji wakuu watatu katika misheni zao. Ushirikiano huu uliambatana na Kituo cha Kimataifa cha Kairo cha Utatuzi wa Migogoro, Ulinzi na Ujenzi wa Amani, ambacho leo kinachukuliwa kuwa taa ya kikanda na kimataifa katika nyanja za mafunzo na maandalizi ya kimkakati katika operesheni za amani na usalama.

Kwa maono yake ya wazi na wajibu wake wa kimataifa, Misri inaendelea kuimarisha ushiriki wake wa kipekee katika misheni za kulinda amani, huku ikiongeza ushiriki wa wanawake na kuboresha miundo ya mafunzo kupitia programu za hali ya juu, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika. Pia, inazingatia kwa kipaumbele kusaidia suluhu za kisiasa kwa mizozo, na kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya kujenga amani endelevu.

Kwa utendaji huu jumuishi, Misri inaonesha maono yake kama taifa la amani si kwa kutuma vikosi tu, bali pia kwa kuchangia katika kuunda sera na kuhimiza thamani za kimaadili katika mazingira magumu zaidi. Hii inathibitisha tena kwamba daima imekuwa na itaendelea kuwa sauti ya busara, daraja la amani, na nguzo ya uthabiti wa kikanda na kimataifa.