Hadithi ya Mafanikio Inayowahamasisha Wafugaji wa Tanzania Kuelekea Uchumi Imara Zaidi

Imeandikwa na: Fred Onesmo
Katika miaka ya hivi karibuni, biashara ya unenepeshaji wa ng’ombe imeendelea kushika kasi nchini Tanzania, hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Kati. Biashara hii si tu inawasaidia wafugaji kuongeza kipato, bali pia inatoa mchango mkubwa katika usalama wa chakula, ajira na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Unenepeshaji wa ng’ombe ni mchakato wa kuchagua ng’ombe (hasa waliodhoofika au wasio na uzito wa kutosha) na kuwapa lishe bora na huduma sahihi kwa muda wa wiki 8 hadi 16 ili kuongeza uzito na ubora wa nyama kabla ya kuwauza sokoni. Hii inalenga kuongeza thamani ya ng’ombe kwa muda mfupi, tofauti na ufugaji wa kawaida unaoweza kuchukua miaka kadhaa kabla ya ng’ombe kuwa tayari kwa soko.
Katika maonesho ya kilimo ya Nanenane mwaka huu, hadhira ilivutiwa na simulizi ya mafanikio ya Shilla Mashauri kutoka mkoa wa Geita, ameyetumia maonesho hayo kama darasa la kubadilisha maisha yake kupitia ufugaji wa kisasa wa ng’ombe. Shilla, kutoka wilaya ya Nyang’wale, ameibuka kuwa mfano wa kuigwa baada ya kuonesha ng’ombe aliye noneshwa kwa miezi mitatu tu, na sasa anauzwa kwa zaidi ya shilingi milioni 4, ishara ya uwezekano mkubwa ulio ndani ya sekta ya mifugo endapo itafanyika kwa maarifa na mbinu bora.
Akizungumza na vyombo vya habari, Shilla alisema kuwa amekuwa mshiriki wa mara kwa mara wa maonesho ya Nanenane, na kila mwaka hujifunza mbinu mpya za ufugaji na usimamizi wa mifugo. Kwa kutumia mbinu alizojifunza, alianza mradi wa unenepeshaji: huchukua ng’ombe waliodhoofika, huwapa lishe bora kama majani ya silaji, mashudu, pumba na virutubisho vingine kwa miezi miwili hadi mitatu. Baada ya kipindi hicho, hufikia ubora unaohitajika sokoni na kuuzwa kwa bei ya juu.
Ng’ombe aliyewasilishwa mwaka huu alinunuliwa kwa bei nafuu, lakini baada ya matunzo bora sasa ana thamani ya zaidi ya milioni 4, kiasi kinachoweza kulipia ada ya chuo kikuu au hata kununua kiwanja.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Ripoti ya 2024):
• Tanzania ina zaidi ya ng’ombe milioni 36.
• Zaidi ya asilimia 95 ya mifugo inafugwa kienyeji.
• Sekta ya mifugo inachangia takriban 7.4% ya Pato la Taifa.
• Inatoa ajira kwa zaidi ya familia milioni 4.
• Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Geita, Mwanza na Shinyanga, inaongoza kwa unenepeshaji.
Hata hivyo, changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa malisho na magonjwa bado ni vikwazo. Shilla anaamini kuwa elimu anayopata kupitia Nanenane ndiyo suluhisho la changamoto hizo.
Shilla Mashauri sasa anatambulika si tu kama mfugaji, bali pia mjasiriamali anayebadilisha taswira ya ufugaji nchini. Ameanzisha mfumo wa kidigitali wa kutunza rekodi za lishe, uzito na afya za mifugo wake, na sasa anapanua mradi wake kupitia vikundi vya vijana wilayani Nyang’wale.
Biashara ya unenepeshaji wa ng’ombe ni fursa halisi kwa wafugaji na vijana wa Kitanzania. Kwa kutumia maarifa sahihi, lishe bora, huduma za mifugo na taarifa za soko, mfugaji anaweza kupata faida kubwa katika muda mfupi. Serikali na wadau wa sekta ya mifugo wanapaswa kuendelea kutoa elimu, mikopo na miundombinu ili kuongeza tija na faida kwa wafugaji wote nchini.