AFRIKA FAHARI YETU: FUNGUO MUHIMU KATIKA FIKRA

AFRIKA FAHARI YETU: FUNGUO MUHIMU KATIKA FIKRA

Imeandikwa na: William Devis Mbakwa

1.0 UTANGULIZI
Karibu ndugu msomaji katika makala ya wazi inayolenga kuangazia dhana mbili zinazoongoza fikra, yaani: mawazo yetu sisi kama Waafrika yamefungwa ndani ya utumwa au yapo huru katika kutenda jukumu la kushughulisha ubongo.


Katika kuliangazia hili, tutaangalia mitazamo mbalimbali iliyofanyiwa tafiti na wataalamu kuhusu matumizi sahihi ya fikra huru inayopambana na utumwa wa kifikra kwa Mwafrika. Hebu kwa uchache tumulike kwa undani wa habari:

2.0 MAHUSIANO KATI YA UTUMWA WA KISASA NA UHURU WA MAWAZO KWA MWAFRIKA
Jitihada za dhati zilizofanywa na viongozi wetu wa Afrika katika kupambania uhuru wa mtu mweusi zilizaa matunda kuanzia miaka ya 1960, ambapo nchi nyingi za Afrika ziliweza kujikwamua, kama vile Tanganyika (leo hii Tanzania), Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe, na kadhalika.


Swali baada ya uhuru kutoka kwa wakoloni: nini kilifuata Afrika? Je ni uhuru wa bendera au ni uhuru wa kifikra?

Kwa mujibu wa chapisho la Hayati J.K. Nyerere (J.K. Nyerere: Jamhuri ya Plato, 2000), litakupeleka katika safari ya fikra, ambapo Plato na wenzake wanachambua haki, mifumo ya utawala, na nafasi ya elimu katika kujenga jamii iliyo bora. Kwa kutumia hadithi za jamii zinazotawaliwa na viongozi wenye hekima, Plato anasisitiza umuhimu wa maarifa, maadili, na usawa.

Maarifa yanahusu fikra iliyokatika ufikirishi wa jambo kwa undani, na hapa ndipo lile neno utumwa na uhuru wa mawazo kwa Mwafrika unachukua nafasi.

Chapisho lililoandikwa (2 Desemba 2021, Haki za Binadamu, UN) linasema:
"Ulimwengu huu leo, ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumwa, takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinasema zaidi ya watu milioni 40 duniani kote ni wahanga wa utumwa wa kisasa."


Ingawa utumwa wa kisasa haujafafanuliwa kisheria, unatumika kama neno mwavuli linalojumuisha vitendo kama vile: kazi ya kulazimishwa, utumwa wa madeni, ndoa ya kulazimishwa, na biashara haramu ya binadamu.

"Kimsingi, inarejelea hali za unyonyaji ambazo mtu hawezi kukataa au kuondoka kwa sababu ya vitisho, vurugu, kulazimishwa, udanganyifu, na kadhalika" (UN, 2021).

Sisi kama Waafrika, tunawaza nini juu ya haya?
Hayati Nelson Mandela alisema:
"Mara zote huonekana kama hakiwezekani, hadi pale kitakapofanyika. Elimu ni silaha yenye nguvu zaidi ambayo unaweza kutumia kuibadilisha dunia. Nimejifunza kwamba ujasiri haumaanishi kuwa hakuna hofu, bali ni ushindi dhidi yake. Mtu jasiri sio yule ambaye hatishiki, bali ni yule anayeshinda."

Je, uhuru wa mawazo unaonekana?


Nukuu nyingine kutoka kwa Mwalimu Nyerere inasema:
"Ni vipi tunaweza kutegemea mikopo na uwekezaji wa kigeni na makampuni ya kigeni bila kuhatarisha uhuru wetu? Ili tujenge nchi ya kujitegemea, ni lazima tuwe na viwanda vingi."
Leo hii tunasema Afrika tupo huru, lakini utumwa wa kisasa unaendelea kufora!

3.0 HITIMISHO
Funguo muhimu katika fikra, yaani mawazo na mitazamo, ni kuruhusu kwanza elimu ya vitendo ndani ya Bara letu ili itegezwe zaidi kwenye muktadha halisia wenye kuinua uchumi wa nchi na kuleta ustawi wa kimaendeleo.
Kulingana na tafiti, baadhi ya watu huamini wazo huanza kwanza (Idealism) kisha uhalisi au maumbo hufuata (Material).


Naungana nao wote katika fikra kuwa mawazo yanayohusisha dhana ya kufikiria jambo kiundani (critical thinking ability) inaleta maumbo. Kwa mfano, muonekano wa kitu fulani unaleta uhalisi wa jambo.

Chanzo cha mafanikio yako ni fikra zako; huwezi kufanikiwa zaidi ya fikra zako zilivyofanikiwa.
Hujawahi kuona watu wakishika mamilioni ya pesa lakini baada ya muda mfupi hawajui hata zilikopotea? Watu hawa wanajaribu kumiliki fedha huku fikra zao zikiwa duni, hawawezi kumiliki chochote wala kukitunza. Kwa hiyo, kabla ya kutafuta mafanikio yoyote, shughulika kwanza na fikra zako. Ukiweza kufikiri kwa viwango vya juu, ndipo vilivyo juu vitakapoambatana na wewe (Emmanuel Minga, 2023).

Ukweli mwingi umefichwa nyuma ya tafsiri mbaya.
Na wengi tumeganda katika njia zile zile walizo naswa babu zetu, ila anapotokea mtu kutufumbua macho, wote tunamgeukia na kumuona adui.


Ukombozi wa kifikra juu ya mawazo yetu haupo katika kujinasibu na lugha za kigeni.

Kwa mfano, wengi huamini juu ya ubora wa watu wa Magharibi, jambo linalotokana na unyonge katika kutumia vilivyo vyetu (inferiority complex). Sio kweli, na ni uwongo kuamini kuwa sisi Waafrika hatuna maarifa katika fikra zetu. Hebu fikiria juu ya vitu vikubwa ambavyo babu na bibi zetu walivifanya katika kuunda picha halisi ya Afrika.

Tunaweza kubadili fikra potofu zenye utumwa wa kisasa katika mitazamo iliyo huru ikiwa tutafanya yafuatayo:
• Kutambua kusudi la MUNGU katika uumbaji, sambamba na kukubali asili yetu kama Waafrika. Kwa mfano, inasikitisha kuona baadhi ya Waafrika wakiamini msemo: "Ni afadhali kuwa mbwa Ulaya kuliko kuzaliwa Afrika." Tuache mara moja fikra potofu za namna hii.
• Kubadili mfumo wa kielimu wenye chembechembe za Kimagharibi, kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu, ili kutatua tatizo la utumwa wa kifikra. Tuchague kutumia lugha zetu za asili, mfano Kiswahili, kwa sababu kuna watumiaji wengi Afrika na inaweza kuwa funguo bora kuwarithisha ukweli wa asili yetu. Aidha, ujifunzaji na ufundishaji kwa watoto shuleni lazima uende sambamba na vitendo na njia shirikishi zinazokuza utamaduni, historia, na maendeleo ya Afrika.
• Kuhamasisha njia stahiki za kufikiri kabla ya kutenda, kuwa silaha nyingine ya kutatua changamoto zetu. Haiwezekani mtu wa nje atutatulie matatizo yetu, zaidi ya sisi wenyewe kufikiri kabla ya kutenda na kung’amua yale yanayotuhusu ndani ya Bara letu lenye utajiri wa kutosha.

Kwa pamoja, katika Umoja wetu, sisi Waafrika tunaweza kutengeneza ushirika huru bila kutegemea maamuzi ya upande usio na maslahi kwa Bara letu.

Mtazamo wangu: Jukumu la kila mmoja ni kuamua kuwa kiongozi wa fikra chanya kuhusu Afrika na uwezo mkubwa wa kimaarifa. Wazazi, walezi, na viongozi wenye dhamana wanapaswa kuelewa jukumu lao katika kuhakikisha utumwa wa kifikra unaondoka kabisa katika ardhi yetu ya Afrika.
"Mmoja kwa ajili ya wote"

MAREJELEO
• Minga, E. (2023). Matibabu ya Fikra: Ufunguo wa kufikiri zaidi ya kawaida. Dar es Salaam Publishers.
• Nyerere, J.K. (2000). Jamhuri ya Plato: Mkuki na Nyota. Publishers.