Ziara ya Macron Nchini Misri: Hatua ya Kimkakati ya Kukuza Utalii na Ushirikiano wa Kitamaduni

Ziara ya Macron Nchini Misri: Hatua ya Kimkakati ya Kukuza Utalii na Ushirikiano wa Kitamaduni

Imetafsiriwa na: Ahmed El-Sayed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Katika mandhari inayoakisi kina cha mahusiano kati ya Misri na Ufaransa na kuonyesha umuhimu wa diplomasia ya kitamaduni, ziara ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, mjini Kairo, ilifungua milango mipya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hasa katika sekta ya utalii. Ziara hiyo haikuwa ya itifaki pekee, bali pia ilihusisha maeneo ya kihistoria na kitamaduni yaliyoakisi urithi wa kale wa Misri na mvuto wake wa kimataifa.

Vyombo vya habari vilijikita kuangazia vipengele vya kiishara na matangazo ya ziara hiyo, na kuifanya kuwa tukio la kuvutia sana, lenye maana kubwa katika nyanja za utalii, uchumi na utamaduni. Ziara ya pamoja ya marais Abdel Fattah El-Sisi na Emmanuel Macron katika Khan El-Khalili ilikuwa tukio muhimu kwa vyombo vya habari, ambapo Rais wa Ufaransa alionekana katikati ya mapokezi ya watu na mandhari ya kihistoria inayounganisha kale na sasa. Tukio hili liliibua mwingiliano mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa baada ya Macron kuchapisha kipande cha video kupitia jukwaa la X, akiambatisha muziki wa wimbo Helwa ya Baladi wa Dalida, mwimbaji wa Kifaransa mwenye asili ya Kimisri. Uunganisho huu wa kitamaduni kati ya Misri na Ufaransa uliwasilisha taswira hai na ya kuvutia ya Misri kama kituo cha utalii kinachobadilika.

Msomi Mohamed Fathi alieleza kuhusu ziara hiyo kuwa ilikuwa “ya kiakili mno,” kwa sababu iliwekeza katika ishara ya mahali hapo ili kuitangaza Misri kwa njia isiyo ya kawaida. Macron alianza ziara yake kwa kutembelea Makumbusho Makuu ya Misri, yenye zaidi ya vipande 50,000 vya kale, ikiwemo mkusanyiko wa dhahabu wa Tutankhamun, kuelekea uzinduzi wake rasmi mwezi Julai ujao. Ziara hii haikuwa tu ishara ya nia ya Ufaransa kwa ustaarabu wa Misri, bali pia ilichangia kulitambulisha makumbusho hayo kimataifa kama moja ya miradi muhimu ya kitamaduni ya karne ya ishirini na moja.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilibainisha kuwa ziara ya Macron katika maeneo ya kihistoria “ina mwelekeo muhimu wa kisiasa, kiuchumi na kitamaduni,” hususan katika kukabiliana na changamoto za kikanda za sasa. Kama sehemu ya shughuli za ziara hiyo, Rais El-Sisi alimpeleka mwenzake wa Ufaransa katika kituo cha kubadilishana cha Adly Mansour cha treni ya chini ya ardhi, ambapo Macron alionyesha kupendezwa na kiwango cha uboreshaji katika sekta ya usafiri wa Misri, na kusisitiza nia ya nchi yake kushiriki katika miradi ya maendeleo ya baadaye.

Aina hii ya ushirikiano inaboresha ubora wa miundombinu inayosaidia utalii, kwani maendeleo ya usafiri wa umma ni nguzo muhimu katika kuboresha uzoefu wa watalii, hususan katika jiji lenye msongamano mkubwa kama Kairo. Rais El-Sisi alisisitiza kuwa serikali “ina nia ya kuanzisha viwanda vinavyohusiana na usafiri na kuongeza asilimia ya vipengele vya ndani,” jambo ambalo ni mwelekeo wa kimkakati unaoathiri vyema sekta ya utalii na huduma kwa ujumla.

Ziara ya Macron ilienea pia katika Chuo Kikuu cha Kairo, ambapo alishiriki katika Kongamano la Ushirikiano wa Kisayansi kati ya Misri na Ufaransa, lililoshuhudia utiaji saini wa zaidi ya hati 40 za makubaliano ya kuanzisha shahada za pamoja za kitaaluma. Rais wa Ufaransa alisema: “Mtaji wa binadamu ni kipengele muhimu nchini Misri, na tunaamini katika umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kisayansi kati ya nchi zetu.”

Mipango hii haiimarishi tu mahusiano ya pande mbili, bali pia inaiweka Misri kama kivutio cha kitaaluma na kitamaduni kwa wanafunzi na wasomi wa kimataifa. Hili ni kipengele kingine cha utalii, kinachojulikana kama utalii wa elimu na kubadilishana kitamaduni, unaozidi kuwa na nafasi kubwa katika kuvutia wageni nje ya mfumo wa kawaida wa utalii.

Ziara ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, nchini Misri haikuwa tu kituo cha kisiasa cha muda, bali ilibeba ujumbe thabiti unaoikuza Misri kama eneo la utalii na kitamaduni la kimataifa. Kupitia kuunganisha historia na urithi na pia ushirikiano wa kiuchumi na miundombinu, ziara hiyo iliwasilisha upya taswira ya Misri kwa ulimwengu kwa njia ya kisasa na yenye mvuto. Athari yake muhimu zaidi ni kwamba ilifungua mlango wa shughuli zaidi za pamoja zinazoweza kuleta ustawi katika sekta ya utalii, wakati ambapo Misri inahitaji kuwekeza kila fursa ili kuimarisha nafasi yake kwenye ramani ya utalii ya kimataifa.

Marejeo
• BBC Arabic. "Ziara ya El-Sisi na Macron katika soko la kihistoria la Khan El-Khalili, mazungumzo ya mitandao ya kijamii katika ulimwengu wa Kiarabu." Kiungo
• Mamlaka ya Habari ya Serikali. "Ziara ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Cairo 2025." Kiungo