Yasser Abu Maalq aandika: Kigezo cha Maendeleo ya Ustaarabu Wowote

Yasser Abu Maalq aandika: Kigezo cha Maendeleo ya Ustaarabu Wowote

Imetafsiriwa na: Saga Ashraf
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Tunapozungumzia maendeleo ya ustaarabu fulani, mara nyingi tunazingatia mafanikio yake ya kisayansi, kitamaduni, kimaumbile (miundombinu), au hata upanuzi wake wa kijeshi pamoja na udhibiti wake wa njia muhimu za biashara.
Kardashev, mwanafizikia wa Kirusi, alipendekeza kipimo maalum cha kutathmini maendeleo ya ustaarabu kulingana na uwezo wake wa kutumia nishati.
• Ustaarabu wa Aina ya Kwanza (Awamu ya Kwanza):
Ustaarabu huu una uwezo wa kutumia rasilimali zote za nishati katika sayari yake ya asili, ikiwemo nishati yote inayopokelewa kutoka kwenye nyota ya mfumo wake wa jua. Kwa sasa, ustaarabu wa kibinadamu unakaribia awamu hii. Kiasi cha nishati kinachotoka jua letu kinakadiriwa kuwa takriban 200 kuadrilioni wati (kuadrilioni = 1 ikifuatiwa na sifuri 15), huku matumizi ya nishati ya wanadamu yakiwa takriban 20 trilioni wati pekee.
• Ustaarabu wa Aina ya Pili (Awamu ya Pili):
Huu utakuwa na uwezo wa kutumia nishati moja kwa moja kutoka kwenye nyota, bila kusubiri miale kufika kwenye sayari. Hii inadhaniwa kupatikana kupitia uundaji wa miundo mikubwa inayozunguka nyota, kama vile Dyson Sphere au “Ubongo wa Matryushka.” Kwa mahesabu ya nishati, ustaarabu wa aina hii unaweza kutumia hadi 400 septilioni wati (septilioni = 1 ikifuatiwa na sifuri 24), sawa na jumla ya nishati inayotolewa na jua letu kwa sasa.
• Ustaarabu wa Aina ya Tatu (Awamu ya Tatu):
Huu unazidi hata fikra za sasa za kibinadamu. Utakuwa na uwezo wa kutumia nishati yote inayopatikana katika galaksi nzima. Kwa mfano, katika galaksi yetu ya Njia ya Milky Way, kiwango cha nishati kinachowezekana kwa ustaarabu wa aina hii kinakadiriwa kufikia andesilioni 40 wati (andesilioni = 1 ikifuatiwa na sifuri 36).
Baadaye, kipimo cha Kardashev kilipanuliwa kwa kuzingatia mawazo ya kinadharia zaidi:
• Ustaarabu wa Aina ya Nne unaweza kutumia nishati ya ulimwengu mzima.
• Ustaarabu wa Aina ya Tano unaweza kutumia nishati ya “ulimwengu mbalimbali” (multiverse).
Hata hivyo, baadhi ya wanasayansi wametoa mtazamo tofauti. Kwa mfano, Michio Kaku (mwanafizikia Mmarekani mwenye asili ya Kijapani) alipendekeza kwamba kipimo cha ustaarabu hakipaswi tu kupimwa kwa kiasi cha nishati kinachotumika, bali pia kwa ukubwa na nguvu ya “uchumi wa maarifa” unaopatikana ndani yake.