PICHA MBILI ZA AFRIKA: Umasikini na Utajiri wa Rasilimali

Imeandikwa na: Rogers Richard
Bara la Afrika linazo rasilimali nyingi sana za asili, ardhi yenye rutuba, na rasilimali watu ambao wengi wao ni vijana. Pamoja na vyote hivyo, ni bara linalotazamwa kwa taswira mbili zinazokinzana:
• Upande mmoja ni umasikini wa kupindukia unaoathiri mamilioni ya watu.
• Upande mwingine ni utajiri mkubwa unaomilikiwa na wachache.
Picha hizi mbili zinawagusa moja kwa moja vijana, ambao ni takriban asilimia 60 ya idadi ya watu barani Afrika, na hivyo wao hubeba mzigo mkubwa zaidi wa changamoto za kijamii na kiuchumi.
PICHA YA UMASIKINI BARANI AFRIKA
Kuna mambo mbalimbali yanayodhihirisha umasikini barani Afrika, kama vile:
• Ukosefu wa ajira,
• Mapato duni,
• Ukosefu wa huduma bora za afya,
• Uchafuzi na uchakavu wa miundombinu.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya Waafrika milioni 400 wanaishi katika umasikini. Hii inamaanisha sehemu kubwa ya watu hawa hawawezi kumudu chakula bora, malazi, na hata huduma nyingine za msingi za kijamii.
Katika kuchunguza umasikini wa bara la Afrika, ni wazi kuwa lazima kuzingatiwe sababu zake, ambazo baadhi zinatokana na ndani ya bara lenyewe, na nyingine zinachangiwa na sababu za nje. Sababu kuu ni pamoja na:
• Ukosefu wa ajira: Mamilioni ya vijana wanahitimu vyuo vikuu lakini wanakosa fursa za ajira. Elimu mara nyingi inawaandaa zaidi kwa kuajiriwa badala ya kujiajiri.
• Rushwa: Rasilimali nyingi za Afrika hupotea kutokana na vitendo vya rushwa, hivyo hazinufaishi wananchi.
• Athari za ukoloni na ukoloni mamboleo.
• Athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe.
PICHA YA UTAJIRI BARANI AFRIKA
Tofauti na taswira ya umasikini, Afrika pia hutazamwa kama bara tajiri lililojaa rasilimali nyingi zenye thamani kubwa duniani, zikiwemo:
• Ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo,
• Mafuta,
• Dhahabu,
• Cobalt na coltan (hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo),
• Gesi asilia,
• Nguvu kazi kubwa ya vijana.
Afrika pia ni soko kubwa linalokua kwa kasi ya ajabu, na hivi karibuni limekuwa kivutio cha nchi nyingi za Ulaya na Amerika. Vilevile, bara hili lina vivutio vingi vya utalii, kama vile Piramidi za Misri na mbuga za wanyama kama Serengeti nchini Tanzania.
Pamoja na utajiri huu, bado mamilioni ya Waafrika wanaishi katika dimbwi la umasikini. Kwa hiyo, jitihada nyingi zinahitajika ili kuondoa hali hii.
JITIHADA ZINAZOWEZA KUFANYIKA
• Kuwapa vijana fursa za kuwekeza katika kilimo cha kisasa: jambo hili linawezekana kutokana na wingi wa ardhi yenye rutuba.
• Ushirikiano wa kikanda: utasaidia kufungua fursa za ajira kwa vijana, kuvutia uwekezaji, na kupanua masoko.
• Matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na huduma.
• Kutoa elimu na kuhamasisha uwajibikaji ili kuhakikisha rasilimali zinawanufaisha wananchi wote.