Lugha ya Kiswahili Inavyoweza Kukuza Diplomasia ya Uchumi kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Imeandikwa na: RIZATI HASSANI MMARY
1.0 Utangulizi
Makala haya yanahusu Lugha ya Kiswahili Inavyoweza Kukuza Diplomasia ya Uchumi kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Makala haya yamegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni Utangulizi, Namna Lugha ya Kiswahili Inavyoweza Kukuza Diplomasia ya Uchumi Kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Hitimisho.
Diplomasia ni maarifa na ustadi wa kuendesha na kusimamia uhusiano wa kimataifa, ni sayansi na maarifa ya kujadiliana na kufanya mapatano hususan katika masuala ya kimataifa (BAKITA, 2022:166). Aidha, diplomasia ni kanuni na utaratibu wa kuanzisha na kuendeleza uhusiano baina ya mataifa. Pia, diplomasia ni mbinu za kushughulika na watu na kuwafanya waelewane (TUKI, 2019:100).
Uchumi kwa upande wake ni mfumo wa uzalishaji mali wa nchi kwa shughuli za kibiashara, viwanda na kilimo na matumizi ya mali hizo, ni stadi inayohusiana na mapato na matumizi ya watu na ya nchi, ni pato linalotokana na shughuli za watu wa eneo fulani za uzalishaji mali (BAKITA, 2022:1020). Vilevile, uchumi ni mali iliyopatikana kutokana na amali za nchi au watu, ni mfumo wa mapato na matumizi ya watu katika nchi (TUKI, 2019:662). Diplomasia ya Uchumi inamaanisha uwakilishi wa nchi fulani nje ya nchi unaojikita katika mambo ya kiuchumi.
Lugha ya Kiswahili imekuwa nyenzo muhimu katika kuibua fursa nyingi ambazo zinaweza kutumika kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Maendeleo na matumizi ya Kiswahili katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, yamekuwa yakitofautiana kutokana na hulka ya kila nchi kuchukua hatua zake bila kushirikisha nchi nyingine hali ambayo imesababisha kukosekana kwa juhudi za pamoja katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa matumizi ya Kiswahili. Kwa mfano, nchini Tanzania, Kiswahili ni lugha ya Taifa, lugha rasmi katika shughuli za serikali na bunge, lugha inayotumika kufundisha shule za msingi na kama somo katika elimu ya juu. Kiswahili kinatumika kutoa mafundisho ya dini, makanisani na misikitini. Kiswahili ni lugha kuu inayotumika katika vyombo vya habari kama vile televisheni, redio na katika idadi kubwa ya magazeti ikiwamo mitandao ya kijamii.
Kwa upande wa Kenya, Kiswahili ni lugha ya Taifa. Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, Ibara ya 7(i), imekipa Kiswahili sura mpya ya kuwa lugha rasmi na lugha ya taifa. Aidha, Kiswahili hufundishwa na kutahiniwa shuleni na vyuoni. Fauka ya hayo, lugha hii inatumika bungeni na katika kuendesha biashara. Kiswahili ni lugha kuu ya mawasiliano wanapokutana watu wa makabila tofautitofauti. Kiswahili kinatumika katika jeshi na polisi. Ni lugha ya kuendesha kampeni za kisiasa mijini na vijijini. Vilevile, Kiswahili kinatumika katika kuendesha ibada misikitini na makanisani. Pia, vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili nchini Kenya bado ni vingi, Kiswahili kinatumika katika programu kadhaa redioni na kwenye televisheni. Aidha, Kiswahili kinatumiwa sana katika mawasiliano ya mitandao ya kijamii na blogu za watu binafsi.
Nchini Uganda, Kiswahili kimeanza kutumika kwa mapana na marefu kutoka 2005. Kiswahili kinafundishwa na kutahiniwa katika viwango mbalimbali vya elimu, kwa mfano, Chuo Kikuu Makerere kina Idara ya Kiswahili ambayo hufundisha isimu na fasihi kwa Kiswahili. Pia, Chuo Kikuu cha Kyambogo, Chuo Kikuu cha Kampala na Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Mbale vinafundisha Kiswahili. Kiswahili ndiyo lugha ya mawasiliano ikitumiwa zaidi na askari.
Kwa upande wa Burundi, Kiswahili kinatumika sana Mashariki mwa Burundi. Kiswahili kinafundishwa katika baadhi ya vyuo, kwa mfano, Chuo cha Wanajeshi wa Bujumbura na katika Chuo Kikuu cha Bujumbura. Vilevile, Kiswahili hutumika katika Redio ya Taifa, Redio Buntu, Redio Rema, Redio Izere, Redio Bonesha, Redio Ibyizigiro, Redio Isanganiro na katika Televisheni ya Taifa ya Burundi. Baadhi ya vipindi vya redio na televisheni hizo ni kama vile habari, matangazo, vipindi vya utamaduni na mafunzo na matangazo ya mipira.
Nchini Rwanda, Kiswahili kinatumika sokoni na mijini. Aidha, kinafundishwa katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Wapo baadhi ya wananchi wanaojiandikisha kujifunza Kiswahili katika madarasa ya jioni. Vilevile, Rwanda imeanzisha Kiswahili katika mtaala wa taifa na kuongezwa katika orodha ya lugha rasmi. Redio Rwanda kuanzia mwaka 1961 imekuwa na programu za Kiswahili kama vile taarifa ya habari, matangazo ya mpira na salamu za wasikilizaji. Hivi karibuni, lugha ya Kiswahili imeanza kufundishwa katika shule zote za upili nchini Rwanda. Pia, Serikali ya Rwanda imepanga kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha za taifa za nchi hiyo.
Sudani Kusini lugha rasmi ni Kiingereza, pamoja na kutambulika kwa lugha mbalimbali za mitaa katika majimbo au miji, Kiswahili kinapangiwa kuenezwa nchini hasa baada ya Sudani Kusini kujiunga na Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kifaransa ni lugha rasmi. Kwa ujumla kuna lugha 242 hasa za Kibantu zinazozungumzwa Kongo. Kati yake lugha nne (4) zinatambulika kama lugha za kitaifa nazo ni Kikongo, Kingala, Kiluba na Kiswahili. Wakati wa ukoloni lugha hizo nne za kitaifa ziliwahi kutumiwa katika shule za msingi. Tangu mapinduzi ya 1997 sehemu za jeshi, hasa mashariki hutumia pia Kiswahili. Takriban 47% wanatumia Kifaransa kama lugha ya kwanza au lugha ya pili.
Kutokana na tofauti hizo, ilizuka haja ya kuwa na chombo kimoja kinachoweza kuunganisha nchi hizi ili kuweza kuondoa tofauti hizo. Hapo ndipo ilianzishwa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (KAKAMA) mwaka 2007 ambayo makao makuu yake ni Zanzibar. KAKAMA ilichochea mwamko wa kujifunza Kiswahili katika nchi wanachama hasa Rwanda, Burundi, Uganda, na Sudani Kusini ambazo hazina wazungumzaji wengi wa Kiswahili kama ilivyo kwa Tanzania, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo, kunatoa nafasi ya kushirikiana kwa pamoja kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuleta maendeleo ya ukuaji na ueneaji wa lugha ya Kiswahili na Uchumi kwa ujumla. Uimarishaji wa lugha ya Kiswahili utaziwezesha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufikia uchumi wa juu zaidi. Hili litawezekana zaidi endapo tutakubali kuitumia lugha ya Kiswahili kama silaha mojawapo ya kushinda au kulifikia jambo. Kiswahili ndiyo lugha ya Afrika Mashariki yenye uwezo wa kuwaunganisha watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
2.0 Namna Lugha ya Kiswahili Inavyoweza Kukuza Diplomasia ya Uchumi Kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
Lugha ya Kiswahili inaweza kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia miradi mbalimbali kama inavyofafanuliwa katika sehemu zifuatazo:
2.1.1 Kufundisha Kiswahili kwa Wageni
Mradi wa kufundisha Kiswahili kwa wageni ni chanzo kikubwa ambacho kinaweza kuchangia katika kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mradi huu utaziingizia nchi zetu fedha ambazo zitatumika katika kukuza uchumi. Hata hivyo, mradi huu utafanikiwa pale tu nchi ambazo hazina mradi huu zitakapokubali kupokea wataalamu kutoka nchi zenye wataalamu wa lugha ya Kiswahili bila ubaguzi. Nchini Tanzania mradi wa kufundisha Kiswahili kwa wageni hutolewa na taasisi na vyuo mbalimbali kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Kituo cha MS - TCDC, Kiswahili na Utamadani (KIU), Dar Language, Evangelica Lutheran Church of Tanzania, Morogoro Language and Orientation School n.k. Mradi huu wa ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni pia unaweza kufanywa kwa kutumia njia ya mtandaoni. Njia ya mtandaoni itasaidia kuziingizia nchi zetu mapato kwa kuwa wajifunzaji watahitajika kulipia mafunzo hayo.
Katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika tarehe 7 Julai, 2022 duniani kote, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema kuwa Tanzania imejipanga vyema katika kueneza Kiswahili duniani kote. Katika kufanikisha hilo alisema kuwa atahakikisha anaziwezesha ofisi zote za kibalozi zilizoko nje ya Tanzania kuhamasisha uanzishwaji wa vituo vya kufundisha Kiswahili kwa wageni na walimu wake watakuwa vijana waliohitimu katika vyuo vyetu vikuu. Halikadhalika, katika siku hiyohiyo Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo kwamba Mabaraza ya Kiswahili yaandae mikakati mahususi ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili serikali iyawezeshe kwa kuyapatia wataalamu na kutenga fedha katika bajeti kwa ajili ya miradi ya Kiswahili ya mabaraza hayo. Kupitia mabaraza haya ni matumaini yetu kuwa vijana kutoka nchi zetu za Jumuiya ya Afrika Mashariki watanufaika na ajira hizo. Lakini pia wanaweza kufungua vituo vyao binfasi vya kufundisha Kiswahili kwa wageni na kuingiza kipato kwa nchi zetu.
Kwa hiyo, tunatoa rai kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanzisha na/au kuimarisha vituo vya ufundishaji Kiswahili kwa wageni. Aidha, ili kuweza kongeza ufanisi, tunaweza kujadiliana ili tuweze kuratibu suala hilo kwa pamoja kwani Wahenga walishasema: umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
2.1.2 Ukalimani na Tafsiri
Ukalimani na tafsiri huhusisha uhamishaji wa ujumbe kutoka lugha moja kwenda nyingine. Taaluma hizi zinaweza kusaidia kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa namna mbalimbali. Wataalamu wa ukalimani na tafsiri wa nchi za Jumuiya wanaweza kuongeza kipato kupitia kufanya ukalimani na tafsiri za lugha mbalimbali kutoka au kwenda Kiswahili. Lugha hizo ni pamoja na Kingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kichina, Kijerumani, Kireno n.k. Hii ni njia mojawapo itakayosaidia sana kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu Kiswahili kimepewa kipaumbele kutumika katika mikutano mikubwa yenye kujumuisha watu wa mataifa mbalimbali yasiyojua lugha ya Kiswahili. Hivyo, katika mikutano hiyo huwa kunahitajika wakalimani na wafasiri. Mtaalamu mwenye taaluma ya ukalimani na/au tafsiri kutoka katika nchi mojawapo ya Jumuiya anaweza kutoa utaalamu huu katika nchi nyingine ya Jumuiya. Mfano, nchini Tanzania, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ya mwaka huu, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango alitoa agizo kwamba nyaraka za mawasiliano za Wizara zote za serikali ya nchi ya Tanzania na Idara zake ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili na kwamba mikutano, warsha, semina, mijadala ya umma na dhifa ziendeshwe kwa Kiswahili. Kupitia tamko hili, ni wazi kuwa vijana wetu watapa ajira ambazo zitakuwa chanzo cha kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia, kupitia ukalimani na tafsiri tunaweza kukuza uchumi kwa nchi kupitia mafunzo yanayotolewa na taasisi zetu ya kunoa wataalamu wa ukalimani na tafsiri. Mafunzo haya hulipiwa ada ambazo ni chanzo kikubwa cha kukuza uchumi. Kama inavyofahamika, Kiswahili kwa sasa kinatambulika na kinatumika katika mikutano mikubwa ya kitaifa na kimataifa hivyo lazima kuwe na wakalimani na wafasiri wa kuweza kufanikisha mawasilisho kwenye mikutano mbalimbali. Kwa upande wa Tanzania, kuna vyuo na taasisi chache zinazotoa kozi ya ukalimani kama BAKITA, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam n.k. Hivyo, tunatoa wito kwa nchi ambazo zinahitaji kusomesha wataalamu wa ukalimani na tafsiri wawasiliane na taasisi /vyuo hivyo kwa ajili ya kuweka utaratibu wa mafunzo hayo au hata kuanzisha ushirikiano baina ya vyuo/taasisi hizo katika nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki.
2.1.3 Kubadilishana Wataalamu kwa Ajili ya Kufundisha Somo la Kiswahili katika Ngazi mbalimbali za Elimu
Kubadilishana wataalamu kwa ajili ya kufundisha somo la Kiswahili katika ngazi mbalimbali kama vile Shuleni na Vyuoni ni mradi mwingine unaoweza kutumika kama chanzo cha kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Baada ya Kiswahili kupewa kipaumbele hususan kimataifa baadhi ya nchi zimeingiza somo la Kiswahili katika mitaala yake ya elimu, kwa mfano, Afrika Kusini, Uganda, Botswana, Msumbiji, Libya n.k. Hivyo, nchi hizi zitasaidia sana kukuza uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuchukua wataalamu kutoka katika zetu na kuwapeleka katika nchi zao kwa lengo la kufundisha Kiswahili, kama alivyowahi kusisitiza Profesa Mugyabuso Mulokozi kwamba :
“Kwa kutumia Kiswahili ajira zipo nyingi sio ndani hata nje ya nchi kwani ndani ya Afrika Mashariki zipo nchi zinazohitaji wataalamu na walimu wa Kiswahili kwa mfano Sudani Kusini. Hata kipindi cha aliyekuwa Rais wa Libya Muammar Gaddaf, aliwahi kuomba walimu 1,000 kwenda kufundisha Kiswahili. Ndani ya Afrika Mashariki kuna Vyuo Vikuu karibu 130 vinavyofundisha Kiswahili. Hivyo, hizo ni fursa za ajira kwa wataalamu na walimu kwenda kufundisha na kufanya tafiti”.
Kutokana na kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili, Afrika Kusini wako tayari kufundisha Kiswahili katika shule za msingi. Kwa mfano, Tanzania na Afrika Kusini zimesaini mkataba wa makubaliano ya kufundisha Kiswahili Julai 7, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam. Baada ya Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, mwezi Julai 13, 2022, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Prof. Adolf Mkenda, alitangaza fursa za walimu kufundisha Kiswahili nchini Afrika Kusini na kwamba watakaochaguliwa ni wale wenye kujua kwa ufasaha matamshi ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Halikadhalika, tarehe Agosti 5, 2022 Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Mhe. Mohamed Omari Mchengerwa pamoja na wajumbe kutoka katika Wizara yake, walikutana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa ajili ya kujadili mkakati wa kuanzisha chuo kikuu cha Kiswahili. Chuo hiki kitatoa na shahada nyingine pia kama shahada za lugha za kimataifa, lugha za alama na taaluma ya nukta nundu. Lengo hasa la kuanzishwa kwa Chuo hiki ni kutaka kuikuza na kuiendeleza lugha ya Kiswahili. Kupitia chuo hiki, ni dhahiri kuwa diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki itakua kutokana na wanafunzi kutoka nchi mbalimbali kuja Tanzania kusoma. Pia, wataalamu watakaopatikana katika Chuo hicho nao watakwenda kufundisha katika vyuo vingine katika Jumuiya.
2.1.4 Mradi wa Machapisho
Hii ni namna nyingine inayoweza kusaidia katika kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Machapisho yanaweza kuchangia kukua kwa diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuyauza nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Machapisho hayo ni pamoja na kamusi, vitabu mbalimbali vya kufundishia na kujifunzia lugha ya Kiswahili na magazeti. Machapisho hayo yanaweza kuwa kwa njia ya mtandao au njia ya nakala ngumu ili kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia. Hata hivyo, mpaka sasa, kuna baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ambazo hazina magazeti ya Kiswahili. Hivyo, hii ni fursa pekee ya nchi nyingine kutuma wataalamu kuanzisha vyombo vya habari ambavyo vitatumia lugha ya Kiswahili. Vyombo hivyo vitasaidia kuweka msingi mzuri wa kukuza lugha ya Kiswahili na diplomasi ya uchumi mingoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Halikadhalika, tunaweza kuwa maandiko ya lugha zetu hasa kamusi ambazo zinaweza kuandaliwa na kuuzwa ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kamusi hizi zitasaidia sana kukuza na kuendeleza Kiswahili lakini pia kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla kupitia kuuza kamusi hizo. Tunaweza kuwa na kamusi ya Kiswahili-Kirundi- Kifaransa, Kiswahili- Kinyarwanda- Kifaransa, Kiswahili- Luganda- Kiingereza.nk.
2.1.5 Uhariri
Uhariri ni mojawapo ya mradi wa Kiswahili unaoweza kusaidia katika kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Uhariri ni mradi ambao unafanywa na wataalamu waliosomea kozi ya uhariri. Hivyo, kupitia mradi huu diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaweza kukua kwa kuanzisha kozi za Uhariri kwa nchi ambazo hazina kozi hizo na pia kuhariri miswada ya nchi mbalimbali iliyoandikwa kwa Kiswahili.
2.1.6 Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii
Vyombo vya habari ni chanzo kingine cha kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Diplomasia ya uchumi kwa nchi hizi itakua kupitia matangazo mbalimbali ya vipindi vya Kiswahili. Matangazo hayo yanaweza kurushwa kupitia redio na televisheni. Nchini Tanzania, kuna magazeti mengi sana ya Kiswahili kama Mwananchi, Habari leo, Zanzibar leo, Mtanzania, Mzalendo, Uhuru, Mwanaspoti n.k. Katika magazeti haya, kuna wataalamu wengi ambao baadhi yao wanatoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama vile Kenya. Aidha, vyombo hivyo vya habari vina fursa zaidi kwa waandishi wa habari, wahariri wa habari, wahariri wasanifu, wasanifu kurasa na wahakiki wa lugha.
2.1.7 Kiswahili na Maendeleo ya TEHAMA
Kupitia Teknolojia ya Habari ya Mawasiliano (TEHAMA), kampuni ya Microsoft Linux imetayarisha programu za kompyuta kwa lugha za Kiafrika, Kiswahili kikiwamo. Programu hizi zitajenga ushirika wa kibiashara na kuwawezesha Waafrika wakiwamo wa Afrika Masharika kutumia komyuta zenye istilahi za Kiswahili katika kujiingizia kipato.
2.1.8 Utalii
Utalii ni njia nyingine inayoweza kusaidia katika kukuza diplomasia ya uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Utalii ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi nchini na kuongoza kwa kuchangia pato la taifa. Kwa mfano, nchini Tanzania, mwaka 2018/19, utalii uliongoza katika kuchangia pato la Taifa kwa asilimia 17.6. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaaliwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii kama maeneo ya kihistoria, milima, mbuga za wanyama, fukwe za bahari, mito na maziwa. Watalii wengi wanaokuja katika nchi zetu za Afrika huhitaji wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha kutembelea sehemu mbalimbali wakipata maelekezo na ufafanuzi wa sehemu hizo wanazozitembelea. Nchini Tanzania, kuna waongozaji wa watalii wanaojua lugha mbalimbali za kigeni. Kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kuwa suala hili linaratibiwa kwa kushirikiana miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
2.1.9 Muziki na Filamu
Muziki na filamu zinaweza kusaidia kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia lugha ya Kiswahili. Nchi zetu zina wasanii wengi wa muziki wa dansi, bongofleva, muziki wa asili, taarabu, muziki wa injili n.k. Muziki na filamu zimekuwa na mchango mkubwa sana katika uenezaji wa Kiswahili ndani na nje ya nchi za Jumuiya. Kupitia mziki na filamu wasanii wa nchi zetu wanaweza kushirikiana na kutunga miziki au filamu kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Kupitia muziki, uchumi wa nchi zetu utakua kupitia viingilio vinavyotolewa na watu wakati wa kuingia kwenye matamasha ya muziki yanayoendeshwa na wasanii. Katika filamu pia uchumi wa nchi za Jumuiya unaweza kukua kupitia viingilio vya kuingilia katika maonesho ya filamu. Kwa upande wa tafsiri ya filamu, diplomasia ya uchumi wa nchi itakua kutokana na kufanya tafsiri ya maneno yaliyomo kwenye filamu kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Kupitia ushirikiano, diplomasia ya uchumi wa nchi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakua kutokana na kushirikiana kwa wasanii kutoka nchi zetu.
2.1.10 Biashara
Biashara zitasaidia sana katika kukuza diplomasia ya uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia lugha ya Kiswahili. Lugha ya Kiswahili imekuwa nyenzo kubwa katika kuunganisha watu wa makabila tofautitofauti. Ili biashara ziweze kufanyika vizuri, kiunganishi kikubwa kinakuwa ni lugha. Kupitia lugha ya Kiswahili, wawekezaji watazidi kuongezeka wakiwa na uhakika wa kufanya biashara zao Kutokana na uelewa wa lugha kwa wateja wao. Lugha ya Kiswahili imesaidia.....
3.0 Hitimisho
Kwa ujumla, Kiswahili kinaweza kukuza diplomasia ya uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufundisha Kiswahili kwa wageni, ukalimani, kubadilishana wataalamu kwa ajili ya kufundisha somo la Kiswahili katika ngazi mbalimbali za elimu, kuuza machapisho, kutafsiri kazi za lugha mbalimbali kwenda na kutoka Kiswahili, kuhariri, kutumia vyombo vya habari, Kiswahili na maendeleo ya Teknolojia na utalii n.k. Yote haya yatawezekana endapo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitashirikiana katika masuala mbalimbali yanayohusu lugha ya Kiswahili. Pia, mbinu mbalimbali zinatakiwa kubuniwa ili kukikuza Kiswahili na uchumi kwa ujumla. Baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na kuwa na mashindano ya wanafunzi, waandishi, na wasanii mbalimbali. Vilevile, nchi zetu zinatakiwa kuzihamasisha nchi zetu zote ziweze kukipa Kiswahili nafasi ya kutosha na kutumika katika nyanja, vyombo na asasi mbalimbali.
Marejeo
BAKITA (2022) Kamusi Kuu ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers Limited.
TUKI (2019) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la Tatu. Nairobi: Oxford University Press.