Mapinduzi ya Julai 23, 1952

Mapinduzi ya Julai 23, 1952

Imeandikwa na: Islam Adel

Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Mapinduzi ya Julai 23, 1952 ni mojawapo ya matukio makubwa ya kihistoria katika nchi ya Misri. Mapinduzi haya, yaliyofanywa na Maafisa Huru, yameleta mabadiliko makubwa katika nyanja za kisiasa, kijamii, na kiuchumi. Mafanikio ya mapinduzi haya pia yalileta matumaini kwa nchi nyingine zilizokuwa chini ya ukoloni na utawala wa kifalme, zikazitia moyo kuamka kutoka kwenye uvuli wa ukoloni na ufalme, na kuelekea kwenye nuru ya uhuru na demokrasia ambapo watu wanajichagulia viongozi wao wenyewe.

Mapinduzi ya Julai 23 hayakufanyika ghafla, bali yaliathiriwa na matukio mbalimbali na upangaji mzuri. Maafisa walihisi tamaa baada ya operesheni ya kijeshi iliyofanywa na baadhi ya maafisa wa kifalme wakati wa vita vya Palestina mnamo mwaka 1948,  iliyoweka jeshi la Misri katika hatari kubwa na kusababisha kushindwa kwa jeshi katika vita hivyo. Hali hii iliwachochea maafisa kuanza kuandaa mipango ya mapinduzi. Walikusudia kufanya mapinduzi hayo mnamo mwaka 1955, kama ilivyosemwa na Rais Gamal Abdel Nasser alipomwambia mwandishi wa habari wa Uingereza, David Dean Morgan.

Hata hivyo, tarehe ya mapinduzi ilibadilika baada ya mfalme kuanza kushuku uwepo wa shirika hili la siri na kujaribu kulichunguza kwa msaada wa ujasusi wa Uingereza, akitaka kuzuia mapinduzi kama yale ya Urabi yasitokee tena. Tukio la moto wa Kairo tarehe Januari 26, 1952 liliongeza shinikizo la kufanya mapinduzi. Hatimaye, waliamua kuyafanya mapinduzi hayo mapema, hasa mwezi Novemba 1952, mwezi ambao bunge lingekutana chini ya katiba. Kama kungetokea udanganyifu wowote katika katiba au uchaguzi, maafisa walikuwa tayari kwa mapinduzi kwa kisingizio cha kulinda katiba.

Maafisa Huru walitaka kubadilisha tena tarehe ya mapinduzi kutokana na hatari waliyoiona baada ya mfalme kutoa amri ya kufuta baraza la uongozi la klabu ya askari. Hatari hiyo iliwafanya wapange kufanya mapinduzi mnamo tarehe Agosti 5, 1952 badala ya tarehe halisi. Lakini baada ya majadiliano kati ya Mohammed Naguib, Mohammed Hashem, Gamal Abdel Nasser, na Abdel Hakim Amer, wakaona ni vyema kuyafanya mapinduzi mapema zaidi ili mfalme asijue jambo hilo na kuwashinda kwa gharama ya jitihada zao zote. Mfalme alipowafukuza baadhi ya askari na kumteua Hussein Sirri Amer kuwa waziri wa vita, maafisa walikubaliana kufanya mapinduzi usiku wa tarehe Julai 22, 1952. 

Ingawa muda wa kupanga na kukutanisha askari ulikuwa mfupi, hawakuwa na uchaguzi ila kutekeleza mapinduzi. Kwa kweli, maafisa huru walifanya mapinduzi, ingawa baadhi ya viungo muhimu kama Mohammed Anwar Sadat hawakujua kuwa shughuli zilikuwa zitafanyika usiku huo, na alikuwa ameenda sinema kabla ya kujiunga na maafisa huru baada ya kuanguka kwa uongozi wa jeshi mikononi mwao. Saa 7:30 asubuhi, tangazo la kwanza la mapinduzi lilisikika kwa jina la Jenerali Muhammad Naguib, na kutangazwa na Muhammad Anwar Sadat kupitia redio ya Misri.

Mapinduzi yalileta mafanikio makubwa katika nyanja za kisiasa, kijamii, kiuchumi, na kijeshi, ambapo Misri ilibadilika kutoka mfumo wa kifalme hadi mfumo wa kijamii. Kanal ya Suez, njia muhimu zaidi ya usafiri wa baharini duniani, ilitaifishwa, na hatua mbalimbali za kuleta usawa wa kijamii na maendeleo katika sekta za kilimo, viwanda, na biashara zilianza kutekelezwa. Mafanikio haya hayakuishia Misri pekee, bali yalileta athari kubwa katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiafrika. 

Misri ilichukua jukumu muhimu katika kusaidia mataifa ya Kiarabu dhidi ya ukoloni, na ilifanikiwa katika hilo, ikihamasisha mapinduzi katika mataifa ya Kiarabu na Kiafrika kujiweka huru kutoka kwa ukoloni. Misri ilichukua uongozi wa bara la Afrika chini ya rais Gamal Abdel Nasser, aliyeona kuwa uhuru wa mataifa ya Afrika kutoka kwa ukoloni ni sehemu muhimu ya kukamilisha uhuru wa Misri. Alisaidia harakati za ukombozi katika mataifa ya Afrika Mashariki na Magharibi kama vile Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Nigeria, Ghana, na Congo. 

Msaada huu wa kidiplomasia, kisiasa, na kijeshi ulisababisha uhuru wa mataifa 17 barani Afrika, na Misri ilipinga ubaguzi wa rangi uliofanyika Afrika Kusini, Zambia, na Zimbabwe. Misri haikuishia hapo, bali ilitangaza kwamba "Afrika ni kwa Waafrika" na kuhamasisha kuanzishwa kwa Shirika la Nchi za Afrika. Misri iliongoza shirika hilo, na ilitoa msaada kamili wa kiuchumi ili kukabiliana na umaskini barani Afrika, pamoja na kupeleka wataalamu na wasomi kwa ajili ya miradi muhimu kama vile uzalishaji wa umeme. Al-Azhar pia ilifanya juhudi za kueneza dini ya Kiislamu katika bara hilo, na Misri ilipeleka walimu, mitaala, na matangazo ya redio katika lugha mbalimbali za Kiafrika.

Mapinduzi ya Julai 23, 1952 yalichora historia mpya katika Misri, ulimwengu wa Kiarabu, na bara la Afrika. Yalibadilisha nchi nyingi kutoka kwenye utawala wa kikoloni na kifalme hadi kuwa nchi huru zenye mamlaka yao wenyewe. Nchi za Afrika zilianza kutumia rasilimali zao tajiri, ambazo hapo awali zilikuwa zikinyonywa kwa manufaa ya mataifa mengine, na kujijenga kama nguvu za kiuchumi za kimataifa.

 Kutokana na hayo, tunaweza kusema kuwa Gamal Abdel Nasser alikuwa kiongozi wa bara la Afrika, siyo tu kiongozi mkuu wa Misri. Athari za mapinduzi haya zimekuwa na mchango mkubwa katika kuleta uhuru na maendeleo kwa nchi za Afrika, na kusaidia kusimamisha unyonyaji wa rasilimali za bara hilo kwa manufaa ya watu wake wenyewe.