Mafunzo na Mazoezi ya Kijeshi Baharini katika Ghuba ya Guinea kwa Ushiriki wa Mataifa 32

Mafunzo na Mazoezi ya Kijeshi Baharini katika Ghuba ya Guinea kwa Ushiriki wa Mataifa 32

Imetafsiriwa na: Walaa Marey 
Imehaririwa na:  Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Nchi 32 za Afrika, Ulaya na Marekani zimeanza mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya siku nane katika maji ya Ghuba ya Guinea. Jeshi la wanamaji la Nigeria limetuma meli 10 za kivita na helikopta mbili kwa ajili ya mazoezi ya pamoja, ambayo yataanza Machi 11 hadi 18.

Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la Nigeria, Admiral Awal Gambo, alisema mwanzoni mwa zoezi hilo, lililopewa jina la "Obangam Express 2022" huko On, jimbo la Rivers, kwamba zoezi hili linalenga kuboresha usalama wa baharini katika Ghuba ya Guinea na kuimarisha ushirikiano na vikosi vya majini ndani ya anga za kikanda na nchi rafiki.

Admiral Gambo alisema zoezi hili la kila mwaka la kimataifa limetokana na haja ya jeshi la majini na walinzi wa mipakani kushirikiana kuhakikisha usalama wa baharini.

"Jeshi la wanamaji la Nigeria litapeleka meli 10, helikopta mbili na vifaa vya ufuatiliaji wa baharini, pamoja na vikosi maalum vya majini, kama sehemu ya zoezi la mwaka huu," alisema.

"Zoezi hili litakuwa na matokeo chanya katika operesheni yetu ya mapambano kupitia mafunzo, huku likiwezesha vyombo vingine husika vya majini kunufaika na ushirikiano wa mashirika mbalimbali na ushirikiano wa kimataifa," alisema.

"Zoezi la mwaka huu ni la kujenga hasa, kutokana na juhudi za serikali yetu za kuamsha makubaliano ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), ambayo yataongeza biashara ya ndani ya Afrika kwa asilimia 33," alisema Admiral Gambo.

Nchi zinazoshiriki mazoezi hayo ni pamoja na Angola, Ubelgiji, Benin, Brazil, Cabo Verde (zamani Cape Verde), Cameroon, Canada, Côte d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Denmark.

Pia kuna Guinea ya Ikweta, Ufaransa, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Guinea-Bissau, Italia, Liberia, Morocco, Namibia, Uholanzi, Niger, Nigeria, Poland, Ureno, Kongo, Sao Tome na Principe na Senegal.

Wengine ni Sierra Leone, Togo na Marekani, pamoja na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS).